Mwenye asili ya Uganda ashinda umeya New York

New York. Jiji la New York limemchagua Zohran Kwame Mamdani (34), mzaliwa wa Kampala nchini Uganda, kuwa meya mpya wa jiji hilo, hatua inayoweka rekodi ya kihistoria katika medani za kisiasa na kijamii nchini Marekani, huku akimtahadharisha Rais wa nchi hiyo kupitia kwake kwa jambo lolote kabla ya kuwafikia wananchi wa eneo hilo.

Mamdani alizaliwa mwaka 1991 mjini Kampala katika familia yenye asili mchanganyiko inayoanzia katika nchi za India, Uganda na Tanzania.

Baba yake, Profesa Mahmood Mamdani, ni msomi mashuhuri barani Afrika ambaye aliwahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka sita katika miaka ya 1970, baada ya kukimbia utawala wa Idi Amin nchini Uganda.

Mama yake, Mira Nair, ni mtayarishaji na mwongozaji maarufu wa filamu kutoka India, anayejulikana duniani kwa kazi zilizopata sifa kubwa kama Monsoon Wedding na The Namesake.

Familia hiyo ilihamia Marekani wakati Zohran akiwa na umri wa miaka saba, lakini historia na uhusiano wao na Afrika Mashariki  ikiwemo Tanzania, ambako wazazi wa babu na bibi zake walizaliwa vimeendelea kuwa sehemu muhimu ya utambulisho na maisha yake.

 “Mimi ni Mmarekani nilyezaliwa Afrika,” aliwahi kusema wakati wa kampeni, akisisitiza undugu wa kihistoria unaounganisha Kampala, Dar es Salaam, na New York.

Zohran anakuwa Meya kijana zaidi ndani ya karne moja na Muislamu wa kwanza kuongoza jiji hilo kubwa kuliko yote nchini Marekani.

Ushindi huo unaweka kilele cha safari yake ya kisiasa yenye kasi ya ajabu, kutoka kuwa mbunge mdogo wa jimbo mwaka mmoja tu uliopita hadi kuwa mmoja wa wanasiasa wanaozungumziwa zaidi nchini humo.

Zohran  ambaye pia aliishi Afrika Kusini katika sehemu ya ujana wake, ni mwanasiasa wa chama cha Democratic mwenye misimamo ya kisoshalisti.

Akihutubia maelfu ya wafuasi wake Jumanne usiku, Zohran alianza kwa kumtaja moja kwa moja Rais wa Marekani, Donald Trump.

“Basi Donald Trump, najua unatazama. Nina maneno manne kwako: ongeza sauti,” alisema muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi.

Amesema New York itakuwa taa ya matumaini katika kipindi hiki cha giza la kisiasa akiahidi kupinga vikali sera za Rais Trump, hususan zinazohusu uhamiaji.

“New York itaendelea kuwa jiji la wahamiaji, jiji lililojengwa na wahamiaji, linaloendeshwa na wahamiaji na kuanzia leo, litaongozwa na mhamiaji,” amesema huku umati ukishangilia.

“Nisikilize Rais Trump ninaposema hili. Ili umfikie yeyote kati yetu, utalazimika kupita kwetu sote,” amesema Zohran.

Katika kipindi cha kampeni, Trump ambaye jina lake limejikita katika historia ya New York, alitishia kukata ufadhili wa shirikisho na “kulichukua jiji hilo” iwapo Zohran angechaguliwa.

Imeandikwa na Hunda Mitanga kwa msaada wa mtandao.