Mzize apasuliwa goti, kuwakosa Simba, Waarabu

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize amefanyiwa upasuaji wa goti na anatarajia kuwa nje ya uwanja kwa wiki nane hadi kumi ambayo ni takribani miezi miwili huku akitarajiwa kuzikosa mechi kadhaa ikiwemo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Waarabu na Dabi ya Kariakoo.

Mzize ambaye alikuwa kinara wa mabao kwa wachezaji wazawa ndani ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga 14, huku akimaliza wa pili nyuma ya Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga 16, alipata majeraha wakati Yanga ikiichapa Wiliete SC ya Angola mabao 3-0 kwenye mechi ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika, Septemba 19, 2025.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa baada ya mshambuliaji huyo kutonesha jeraha ambalo lilimuweka nje kwa wiki tatu, uongozi ulifanya uamuzi wa kumfanyia upasuaji na tayari jambo hilo limefanyika.

“Ni kweli Mzize amefanyiwa upasuaji wa goti ambalo kwa mujibu wa daktari atakaa nje ya uwanja kwa wiki nane hadi kumi hivyo hatutakuwa na huduma ya mchezaji huyo kwa muda huo.

“Upasuaji huo umezingatia vipimo vikubwa alivyofanyiwa, haikuwa rahisi mchezaji kukubaliana na hilo, lakini msaada mkubwa wa wanasaikolojia na namna alivyojengwa na madaktari bingwa imechukua siku tatu kufanikisha jambo hilo baada ya mchezaji kukubali.”

Mtoa taarifa huyo alisema wanatambua umuhimu wa mchezaji huyo kwenye kikosi chao na hata timu ya taifa, hivyo wanaamini baada ya upasuaji huo kama atafuata taratibu zote mara baada ya wiki nane hadi kumi atarejea uwanjani na kuendelea na majukumu yake kama kawaida.

Akithibitisha hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema: “Mara ya mwisho tuliwajulisha kuhusu hali ya majeraha ya Clement Mzize. Mzize ndiye mchezaji pekee kwenye kikosi chetu ambaye alikuwa akisumbuliwa na majeraha. Mara ya baada ya ushauri wa jopo la madaktari wakishirikiana na benchi la ufundi, na mchezaji mwenyewe tulifikia kukubaliana kuwa afanyiwe upasuaji.

“Mzize alikuwa anapona kidogo lakini baada ya muda mfupi anapata tena maumivu. Hivyo iliridhiwa mchezaji huyo afanyiwe upasuaji wa goti ambao tayari umekishafanyika hapahapa nchini na anaendelea vyema.”

Upasuaji huo utamfanya Mzize kuzikosa mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga itacheza nyumbani dhidi ya AS FAR ya Morocco kati ya Novemba 21 na 23, 2025, na ile ya ugenini nchini Algeria dhidi ya JS Kabylie kati ya Novemba 28 na 30, 2025.

Mzize pia atazikosa mechi nne za Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC (Novemba 9, 2025), Namungo (Desemba 4, 2025), Coastal Union (Desemba 10, 2025) na Simba (Desemba 13, 2025).

Mshambuliaji huyo pia atakosekana kwenye michuano ya AFCON 2025 itakayofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 ambapo Tanzania imepangwa Kundi C na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda.