Rais Samia amuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemwapisha Hamza Johari kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Johari ameapishwa leo Jumatano, Novemba 5, 20254, Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.

Johari ameapishwa baada ya kuteuliwa na Rais Samia Novemba 3, 2025, saa chache baada ya Samia kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania.

Rais Samia aliapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju. Sherehe hizo zilifanyikia Uwanja wa Gwaride, Ikulu ya Chamwino.

Uapisho huo uliofanyika baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumtangaza Samia mshindi wa urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kwa kupata kura milioni 31 sawa na asilimia 97.6 ya kura zote milioni 37 zilizopigwa.

Johari ameapishwa kuendelea na wadhifa huo baada ya kuwa kuteuliwa kwa mara ya kwanza Agosti 15, 2024 kuchukua nafasi ya Dk Eliezer Feleshi ambaye aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Kabla ya uteuzi huo, Johari alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

Baada ya kuapishwa, Johari alipata fursa ya kuzungumza mbele ya viongozi mbalimbali akiwamo Rais Samia akiahidi kutekeleza majukumu yake na kufanya uamuzi kwa kufuata Katiba, sheria, kanuni, taratibu, mila na desturi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Sitatoa shinikizo linalokiuka sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika utendaji kazi za umma,” amesema Hamza.