Dar es Salaam. Vurugu zilizotokea kwenye baadhi ya maeneo nchini kuanzia Oktoba 29, 2025, zimeacha alama kubwa ya maumivu katika uchumi wa Tanzania, hususan katika sekta zisizo rasmi, biashara ndogo na zile zinazotegemea teknolojia ya kidijitali.
Uharibifu, hofu na usumbufu wa shughuli za kila siku vilisababisha kuporomoka kwa mzunguko wa fedha, kukwama kwa usafiri na usafirishaji wa mizigo, pamoja na kupanda kwa gharama za maisha katika maeneo mengi nchini.
Vurugu hizo ambazo zilianzia Dar es Salaam na baadaye katika baadhi ya mikoa kama Arusha, Mwanza, Tarime na Mbeya na Songwe yalisababisha taharuki na madhara makubwa katika miji mikubwa.
Wafanyabiashara wengi walilazimika kufunga maduka na ofisi zao kutokana na hofu ya uporaji na uharibifu wa mali, huku wengine wakishindwa kufika kazini kutokana na barabara kufungwa.
Athari kubwa ilionekana kwa kampuni zinazotegemea huduma za mtandao katika kufanya biashara. Taarifa kutoka kwa wadau wa sekta ya teknolojia hiyo zinaonyesha kuwa, kukatika kwa mtandao wa intaneti na huduma za mawasiliano kulisababisha mamilioni ya miamala ya kifedha kushindwa kukamilika.
Baadhi ya huduma za kibenki kupitia simu, malipo ya ankara na miamala ya biashara mtandaoni zilikwama kwa siku kadhaa, hali iliyosababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
Mbali na hilo, sekta ya usafiri nayo iliathirika vibaya. Barabara nyingi katika jiji la Dar es Salaam na baadhi ya miji mikuu zilifungwa na magari ya mizigo yalishindwa kusafirisha bidhaa kutoka eneo moja kwenda jingine.
Hali hiyo ilisababisha ucheleweshaji wa usambazaji wa bidhaa muhimu kama chakula, mafuta na dawa. Wamiliki wa magari ya usafirishaji walilazimika kusitisha safari kwa hofu ya magari yao kushambuliwa au kuchomwa moto.
Upungufu wa mafuta uliibuka haraka baada ya vituo vingi kufungwa kutokana na ukosefu wa usalama. Baadhi ya vituo vilivyouza mafuta vilihudumia magari ya vyombo vya ulinzi pekee, hali iliyosababisha huduma kwa wananchi wengine kusimama. Wafanyabiashara wengi walishindwa kusafirisha bidhaa na bei ya usafiri ilipanda kwa kasi.
Huduma za bodaboda ziligeuka kuwa tegemeo kuu kwa wananchi waliolazimika kuondoka katika maeneo hatarishi, lakini nauli zake zilipanda hadi mara kumi ya kiwango cha kawaida. Safari ambayo kwa kawaida hugharimu Sh2, 000 ilifikia hadi Sh20, 000 au 30,000. Wengi walilazimika kutembea kwa miguu kwenda au kutoka kazini, huku wengine wakibaki nyumbani kwa kukosa usafiri.
“Lita moja ya mafuta ilikuwa inapatikana kwa hadi Sh15, 000 unategemea mimi nitatoza shilingi ngapi? Ilikuwa ni hatari pia kufanya safari, vikwazo vya usalama na waandamanaji vilifanya safari kuwa ngumu,” amesema mmoja wa waendesha bodaboda wa Goba maarufu kama Muha.
Madhara mengine yalionekana katika mzunguko wa bidhaa sokoni. Maduka makubwa yaliripoti upungufu mkubwa wa chakula, huku unga, mchele na sembe vikigeuka kuwa bidhaa adimu.
Mikate haikupatikana kwa urahisi na baadhi ya wauzaji walipandisha bei mara mbili hadi tatu. Katika baadhi ya maeneo, nyama ya ng’ombe ilipanda kutoka Sh10,000 hadi Sh25,000 kwa kilo, hali iliyosababisha wananchi wengi kubadili mlo wao.
Kwa upande mwingine, kuku waliendelea kuwa kitoweo nafuu na wakawa mbadala wa nyama nyingine ambazo bei zake zilipanda maradufu.
Hali hiyo ilisababisha ugumu wa maisha, hasa kwa wananchi wa kipato cha chini waliotegemea kutoka ili kupata mlo wa siku.
Sekta ya ukarimu nayo haikupona. Hoteli, migahawa, baa na maeneo ya burudani yalifungwa kutokana na ukosefu wa usalama na uhaba wa wateja.
Wafanyakazi wa sekta hiyo, hasa wale wanaolipwa kwa siku, walijikuta bila kipato kwa muda mrefu.
Akizungumza kuhusu athari za maandamano hayo Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Vituo vya Mafuta Tanzania (Tapsoa), Augustino Mmasi, alisema kwa sasa takribani asilimia 70 ya vituo vya mafuta nchini vimefunguliwa na vinaendelea kutoa huduma, huku juhudi zikiendelea kuhakikisha huduma zinarejea katika maeneo yote.
Hata hivyo, licha ya juhudi hizo, kuna hofu kwamba mafuta yaliyopo katika vituo hivyo huenda yakadumu kwa siku zisizozidi mbili kutokana na ukosefu wa usambazaji mpya.
Kwa sababu hiyo, wanaiomba Serikali kutoa kipaumbele kwa malori ya mafuta, ili yaweze kusafirisha mafuta kwa haraka zaidi.
“Malori yanayosafirisha chakula yameruhusiwa kufanya kazi, lakini hayawezi kufika yalikoelekezwa endapo vituo vya mafuta vitaishiwa mafuta. Tunaiomba Serikali, kuanzia kwenye maghala makuu, iyape kipaumbele malori ya mafuta na kuyasaidia kupita haraka kwenye mizani na vituo vya ukaguzi barabarani,” amesema Mmasi.
Ameongeza kuwa kwa sasa kuna ushirikiano mzuri kati yao, Wizara ya Nishati, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na wadau wengine, lengo ni kuhakikisha usafiri unarejea katika hali ya kawaida na tatizo la upungufu wa mafuta linatatuliwa.
Akizungumzia changamoto za mafuta, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, ameliambia gazeti la The Citizen, kwamba Serikali inalifanyia kazi suala hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elis Lukumay, amesema sekta ya usafirishaji imepata changamoto kuwa “si siri tena kwamba sekta nzima ya usafirishaji ipo kwenye hali ya changamoto”
“Ni lazima tuhakikishe kwamba malori yaliyokwama yanaanza tena safari mara moja ili kurejesha imani kwa wateja wa kimataifa wanaotumia bandari yetu,” amesema Lukumay.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa kadri mwaka unavyoelekea ukingoni, waagizaji wengi wamepanga kupokea shehena kwa ajili ya msimu wa sikukuu, na ucheleweshaji zaidi unaweza kuwafanya kuelekeza mizigo yao katika bandari nyingine za kanda.
“Ni lazima tuchukue hatua haraka,” amesema Lukumay na kuongeza:Wamiliki wa meli wanaweza kwa urahisi kuchagua bandari nyingine endapo watapoteza imani na Bandari ya Dar es Salaam. Kabla hilo halijatokea, tunapaswa kurejesha heshima yetu.”
Aidha, Lukumay ameonya kuwa kampuni nyingi za usafirishaji zinakabiliwa na changamoto za ukosefu wa fedha.
“Madereva hawajalipwa mishahara na mifumo ya benki imekuwa ikitatizika. Lakini lazima tuiweke nchi yetu mbele na kuhakikisha amani inatawala huku tukitafuta suluhisho la changamoto hizi,” amesema.
Kwa mujibu wa Lukumay, gharama ya lori kusimama bila kufanya kazi ni takribani dola 200 kwa siku (Sh500,000), huku gharama za kuhifadhi mizigo bandarini zikiongeza dola 50 zaidi, jambo linalomaanisha athari za kifedha zinaweza kufikia mamilioni ya shilingi.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severin Mushi, amewashukuru polisi kwa kulinda maduka na mali wakati wa kipindi cha sintofahamu, lakini amesisitiza umuhimu wa kurejesha imani ya wateja.
“Pamoja na kwamba maduka yetu yamelindwa vizuri Kariakoo, wateja wengi wa kigeni walikwama kwenye hoteli na kulazimika kulipa gharama za ziada za malazi kutokana na barabara kuzibwa. Sasa tunapaswa kufanya kazi ya kurejesha imani yao na kuhakikisha wanapokea bidhaa zao ili waendelee kufanya biashara nasi,” alisema.
Mushi pia amesisitiza umuhimu wa mawasiliano katika biashara ya kimataifa. “Kuzimwa kwa intaneti kuliwakatisha tamaa wafanyabiashara wengi waliokuwa hawawezi kuwasiliana na wasambazaji wao nje ya nchi. Miamala ya benki ilikwama, na baadhi walipoteza mikataba. Tunatumaini huduma ya mtandao itarejea kikamilifu haraka,” alisema.
Hata hivyo, Mushi amesema licha ya hali ngumu iliyokuwepo, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) liliendelea na safari zake, likiwawezesha wafanyabiashara wachache kusafiri kwenda nje ya nchi, hasa Guangzhou, China, kwa ajili ya manunuzi ya msimu wa sikukuu.