Mbeya/Dodoma. Itabaki historia. Ndivyo wanavyosema baadhi ya wananchi wa Jiji la Mbeya wakielezea misukosuko na taharuki waliyopitia wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025. Wanasema hali waliyokutana nayo haipaswi kujirudia katika chaguzi zijazo.
Kwa siku sita mfululizo, kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 3, 2025, wananchi wengi walijikuta wakijifungia ndani kwa hofu ya usalama wao, wakisubiri hali irejee kuwa ya kawaida.
Hatua ya utulivu ilirejea baada ya Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania na kutoa maelekezo kwa Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku bila woga.
Sintofahamu siku ya uchaguzi
Siku ya kupiga kura, baadhi ya Watanzania walitimiza haki yao ya kikatiba kwa kuwachagua Rais, wabunge na madiwani. Hata hivyo, utulivu huo uliharibiwa na hali ya vurugu zilizotokea katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Mbeya.
Awali, mazingira yalionekana kuwa tulivu, lakini kuanzia saa 4 asubuhi hali ilianza kubadilika baada ya kuanza kusambaa kwa taarifa zikieleza kuwa maeneo ya Isanga, Ilemi, Uyole, Kabwe, Mwanjelwa na Soweto yalikuwa yamevamiwa na makundi ya watu waliokuwa wakifunga barabara, kuchoma matairi na kuharibu mali za raia.
Jeshi la Polisi lilifika kudhibiti hali hiyo kwa kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya watu hao. Hatua hiyo ilisababisha taharuki kubwa huku shughuli za kijamii na kiuchumi zikisimama kwa muda, wananchi wakijifungia majumbani na wengine wakikimbia ovyo wasijue wanaelekea wapi.
Kwa mujibu wa mashuhuda, vurugu hizo zilienea hadi nje ya jiji, zikiathiri wapigakura, wasimamizi wa vituo na makarani wa uchaguzi waliolazimika kukimbia kuokoa usalama wao. Baadhi ya masanduku ya kura yalivamiwa na kuchomwa moto, huku vituo vya kupigia kura katika maeneo ya Soweto, Kabwe, Ilemi, Isanga, Mama John, Isyesye, Itezi na Uyole vikiharibiwa.
Wakati hali ya utulivu ikirejea taratibu, wananchi waliripoti kukosa huduma muhimu kwa siku kadhaa kutokana na hofu ya kutoka nje. Biashara zilisimama, vyakula vilipungua majumbani na mitandao ya mawasiliano ikawa dhaifu, jambo lililoongeza wasiwasi.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wamesimulia kuwa matukio hayo yataendelea kubaki katika kumbukumbu zao kwa muda mrefu.
Samira Mwashilindi, mfanyabiashara wa soko la Soweto, amesema alilazimika kuacha mizigo yake baada ya kusikia milipuko ya risasi kati ya polisi na waandamanaji.
“Nilichokumbuka ni mtoto wangu niliyekuwa namnyonyesha. Nilimkimbilia nyumbani. Mume wangu, dereva wa daladala, alinipigia simu kuniambia nijifungie ndani. Mpaka sasa hajarejea, ingawa tunawasiliana. Kwa kweli, hii ni historia isiyosahaulika,” amesema kwa huzuni.
Naye Titus Gasper, dereva wa bajaji, amesema alitelekeza chombo chake baada ya vurugu kuzuka na kuomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha hali kama hiyo haitokei tena.
“Watu wamepoteza maisha, wengine wamebaki walemavu. Uchumi umeporomoka, wiki nzima tumekuwa majumbani bila kufanya kazi. Wengine tunategemea mapato ya kila siku kulipa madeni. Hii hali ni somo kwa wote,” amesema Gasper.
Ameongeza kuwa, tofauti na kipindi cha janga la Uviko-19, safari hii changamoto kubwa ilikuwa kukosa huduma za mawasiliano.
“Hakukuwa na intaneti. Simu zetu zilibaki kama tochi. Tuweke akili zetu sawa, Serikali na wananchi, tusirudie makosa kama haya,” amesema.
Kwa upande wake, Veronica Njema amesema ingawa kiuchumi familia nyingi zilipata hasara, baadhi ya wanandoa walitumia muda huo kuimarisha uhusiano wao.
“Kwa muda wote tulikuwa nyumbani. Mimi na mume wangu tulitumia nafasi hiyo kuwa karibu zaidi na watoto. Tulipika, tulicheka, na tulipumzika pamoja. Japo tulipoteza kipato, tulipata utulivu wa kifamilia,” amesema Veronica.
Kuanzia Oktoba 29, 2025, Jiji la Mbeya lilijikuta likipoteza huduma za usafiri wa ndani na nje kutokana na vurugu zilizozuka kipindi cha uchaguzi mkuu. Wananchi wengi walilazimika kutumia mbinu binafsi kufika walikotaka kwenda, huku usafiri wa pikipiki ukibaki tegemeo pekee.
Kwa waliokuwa na vyombo vya moto, hasa waendesha bodaboda, huu ulikuwa wakati wa kupata faida kubwa, kwani nauli ilipanda zaidi ya mara tano. Safari zilizokuwa zikigharimu Sh2,000 zilifikia kati ya Sh15,000 na Sh20,000, huku safari za Mbeya–Chunya zikifikia Sh10,000 kutoka Sh4,000 ya awali.
Huduma za usafiri zilisimama kwa wasafiri wa maeneo ya Mbarali, Kyela na nje ya jiji la Mbeya, ambapo hakuna aliyesafiri kuanzia Oktoba 28 hadi Novemba 4. Wakati huo huo, wananchi walikumbwa na ongezeko kubwa la bei za bidhaa sokoni na madukani.
Bidhaa muhimu zilipanda ghafla: kilo 20 za mchele kutoka Sh45,000 hadi kati ya Sh58,000 na Sh60,000, sabuni kutoka Sh4,000 hadi Sh4,500, mafuta ya kupikia hadi Sh55,000 kwa lita tano, nyama kutoka Sh10,000 hadi Sh15,000, na mbogamboga zikafikia Sh1,000 kwa fungu. Hali hiyo ilifanya maisha kuwa magumu zaidi, kwani bidhaa nyingi muhimu pia ziliadimika sokoni.
Wananchi na wito wa amani
Wananchi wengi wametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, vyombo vya ulinzi na usalama, na wananchi kwa ujumla kujifunza kutokana na yaliyotokea.
Wamesema amani ni msingi wa maendeleo, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa mstari wa mbele kuilinda.
“Tumeumia, tumejifunza. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha amani inatawala katika kila uchaguzi,” amesema mmoja wa wazee wa jiji hilo.
Wakati Mbeya ikipambana na ukosefu wa huduma, Jiji la Dodoma lilishuhudia saa 72 za taharuki, vilio na hofu. Baada ya kumalizika kwa upigaji kura Oktoba 29, kundi la watu wasiojulikana lilivamia barabara eneo la Dodoma Inn na kuwasha matairi huku wakiimba “Tunataka mabadiliko”.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Jeshi la Polisi lilifika haraka na kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji. Hata hivyo, milio ya risasi na mabomu iliendelea kusikika kwa siku mbili, jambo lililosababisha utulivu wa jiji hilo kutoweka.
Wafanyabiashara walipata hasara kutokana na kushindwa kuuza bidhaa zinazoharibika haraka.
“Nilishusha mzigo wa nyanya na hoho, sasa zimeoza, hakuna anayenunua,” amesema Helena Mbilinyi, maarufu Mama Nyanya.
Kwa upande mwingine, baadhi ya waendesha bodaboda akiwamo Samson Eliah, amesema amepata faida isiyotarajiwa kutokana na uhaba wa usafiri.
“Safari ya kwenda kwa Sh5,000 nilimpeleka abiria kwa Sh12,000,” amesema dereva huyo.
Amesema si kwamba alipenda kupandisha bei, bali kutokana na bei ya mafuta kupanda baada ya vituo vyote kufungwa na kuwalazimu kununua mafuta kwenye vidumu.
Mbali na bei ya usafiri kupanda, bei za bidhaa mbalimbali za vyakula nazo zilipaa. Eliaman Lyimo, mfanyabiashara wa bidhaa kwa bei za rejareja, amesema alilazimika kuuza kilo moja ya sukari kwa Sh4,000 kutoka Sh2,800 na unga wa sembe kwa Sh3,000 kutoka Sh1,700.
Hata hivyo, Daniel Mrisho, mkazi wa Dodoma, amesema vurugu hizo zimewaachia Watanzania somo moja kuu kwamba, “amani ni nguzo ya uchumi, na pasipo utulivu, gharama za maisha hubebwa na mwananchi wa kawaida.”
