Sio kinyonge, wamewagomea wageni kimtindo

SIO kauli ngeni kusikia baadhi ya wadau wa soka wakilalamika kwamba uwepo wa wachezaji wa kigeni unafifisha nafasi ya wazawa kwenye klabu mbalimbali hapa nchini.

Kila klabu ina nafasi ya kikanuni kusajili wachezaji 12 wa kigeni, kama huna staa wa kigeni basi ni suala la mfuko wako au uamuzi wa chama lako.

Wapo wageni ambao wamekuja na viwango bora lakini wakakutana na mziki wa wazawa wabishi kisha wakawakomalia na kuwaweka nje au hata kugawana mechi nusu kwa nusu.

Hebu tuwaangalie mastaa saba ambao wamegoma kukaa benchi na kuingia kwenye vikosi vyao kibabe kisha wanafanya kweli uwanjani.

WAME 01

Ni kijana ambaye Azam FC imempika na sasa anakuja juu akiitaka nafasi kibabe ndani ya klabu hiyo akichuana na mkongwe Issa Fofana. Msimu huu Foba ameonyesha hataki kukubali unyonge, ndani ya michezo minne ya mashindano amegawana nusu kwa nusu na Fofana raia wa Ivory Coast akicheza mechi mbili ikiwemo moja ya Kombe la Shirikisho Afrika na moja ya Ligi Kuu Bara sawa na Fofana. Kama haitoshi Foba kiwango chake kimembeba akicheza bila kuruhusu bao na kuitwa mpaka timu ya taifa Stars huku Fofana akiruhusu bao moja.

WAME 02

Kama kuna mtu amestua kwenye kikosi cha Yanga msimu huu basi ni kuibuka kwa kiungo Aziz Andabwile ambaye ghafla amekuwa staa muhimu ndani ya kikosi hicho.

Andabwile ndani ya Yanga ya kocha Romain Folz alikuwa wa moto akiiteka eneo la kiungo wa kati pale chini, akimuweka nje staa ambaye alikuja kwa mbwembwe nyingi Mousa Bala Conte. Kwenye mechi tano kabla ya mabadiliko ya benchi la ufundi akija Pedro Goncalves na kuondoka Folz, Andabwile ameanza nne huku moja tu akianzia benchi lakini kama haitoshi ameshafunga mabao mawili huku akionyesha kiwango kikubwa.

WAME 03

Kipa namba moja wa Pamba ni Yonah Amoss ingawa msimu huu ameuanza kwa balaa baada ya kuumia kwenye mchezo wake wa kwanza tu dhidi ya Namungo ya Lindi.

Kiwango cha Yonah kimemfanya kuwa kipa chaguo la kwanza mbele ya Mohamed Kamara raia wa Sierra Leone ambaye aliwahi kupita klabu kubwa kama Horoya AC ya Guinea na Singida Black Stars. Kwa sasa tangu Yonah aumie ndio kumewafanya makipa wengine kucheza wakiwemo Kamara na Denis Richard kwenye mechi za ligi ambazo Pamba imecheza.

WAME 04

Nahodha msaidizi wa Azam ambaye anacheza kama kiungo wa kati chini pale kwa matajiri wa Chamazi. Zayd kuanzia msimu uliopita ameonyesha anataka heshima yake irudi akitawala kwenye kikosi cha kwanza, licha ya ujio wa kocha Florent Ibenge kiungo huyo amekuwa bado chaguo la kwanza akianza kwenye mechi zote nne.

Kiwango cha Zayd sio taarifa nzuri kwa kiungo bora kama James Akaminko raia wa Ghana ambaye amelazimika kusubiri nje kwa baadhi ya mechi.

WAME 05

JOB, BACCA, MWAMNYETO (YANGA)

Pale Yanga kuna wazawa wengine jeuri ambao ni mabeki Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na nahodha wao mkuu Bakari Mwamnyeto.

Job na Bacca wamecheza kwenye mechi nyingi huku Mwamnyeto akisotea sana benchi lakini Yanga ikaleta beki wa kwanza wa kigeni Mamadou Doumbia lakini akashindwa akaondoshwa.

Baadaye akaletwa Gift Fred, beki bora tu lakini akashindwa kupasua kwa mabeki hao wawili ambapo naye akapewa mkono wa kwaheri. Msimu huu ameletwa beki mwingine wa kigeni Frank Assinki raia wa Ghana ambaye naye kama Gift ni beki wa kazi lakini bado ameshindwa kutoboa ndio kwanza Mwamnyeto ameibuka akiitaka namba akianza kwenye mechi mbili huku mgeni akisubiri.

WAME 06

Mzawa mwingine alionyesha ubora mkubwa ni huyu Yusuf Kagoma ambaye ni kiungo wa kati aliyesajiliwa msimu uliopita akitokea Singida Fountain Gate.

Tangu Kagoma atue Simba ameonyesha uwezo mkubwa, akiwapangua wageni kwenye eneo hilo, akibadilishiwa wageni kucheza nao sambamba lakini sio kukosekana.