Tamwa yatoa pole kwa waathirika wa vurugu

Dar es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimeeleza huzuni na kutoa pole kwa Watanzania wote waliopata madhila kutokana na vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Vurugu hizo zilitokea wakati uchaguzi ukiendelea nchini jambo lililosababisha uharibifu wa mali za umma, binafsi pamoja na vifo.

Taarifa iliyotolewa leo Novemba 5, 2025 kwa umma na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk Rose Reuben, imeeleza kuwa pole maalumu zinatolewa kwa familia zote zilizopoteza wanawake, watoto, na wanahabari, pamoja na wale wote walioumia au kuathirika kwa namna yoyote kutokana na matukio hayo ya kusikitisha.

“Wakati Taifa likipitia katika kipindi kigumu katika hali hii, tunaiunga mkono familia na jamii zote zinazojitahidi kuijenga upya hali ya utulivu, mshikamano na amani nchini,” imeeleza taarifa hiyo ya  Dk Reuben.

Chama hicho kimeendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda utu wa binadamu, kuheshimu haki za kila mmoja na kudumisha mazungumzo ya amani kama nguzo muhimu ya Taifa.

 Tamwa inasisitiza kuwa, kulinda amani na mshikamano ni jukumu la kila Mtanzania, ili kuondoa hofu na kuimarisha mshikamano wa kijamii.

“Tunaendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda utu, kuheshimu haki za binadamu na kudumisha mazungumzo ya amani kama nguzo ya Taifa letu,” amesema Dk Reuben kupitia taarifa hiyo.