TEC yaiomba Serikali iwazike waliofariki kutokana na vurugu

Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeiomba Serikali kutenga eneo la maziko kwa watu waliopoteza maisha Oktoba 29 kutokana na vurugu zilizotokea maeneo mbalimbali nchini.

Vurugu hizo zilianza kutokea Jumatano Oktoba 29, 2029  hadi Oktoba 2, 2025 katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne, Novemba 4, 2025 Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa ameiomba Serikali iweke wazi majina na idadi kamili ya waliopoteza maisha.

“TEC tunaiomba Serikali wale waliouawa kwenye maandamano wazikwe kwa heshima, ili ndugu zao waione miili na tuwe na idadi kamili. Kwa sasa idadi haijulikani tunategemea zaidi kauli ya Serikali sababu hatuwezi kuhesabu,” amesema Mhashamu Wolfgang Pisa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji, Dk Moses Matonya amesema kilichotokea kimewasikitikisha.

“Kuna watu wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa na wapo ambao hawakuwa kwenye maandamano wala vurugu zile na wamepoteza maisha, lazima tupeane pole,” amesema.

Dk Matonya amesema upo uharibifu mkubwa wa mali za Serikali na za watu binafsi lakini  miundombinu ya watu binafsi na ya Serikali pia.

Amesema Watanzania wanapaswa kupeana ole kwa matukio yote yaliyotokea.

“Tunatoa pole kwa yaliyotokea, baada ya pole na haya yote ndipo tuseme tunafanya nini, hadi sasa tuna hali ya kulaumiana, kunyoosheana vidole, hatupaswi kuwa hivyo, kwa muda huu tunapaswa sote kwa pamoja, tukae chini na tuangalie nini kimetokea na kwa nini, kupitia meza ya mazungumzo,” amesema kiongozi huyo.

Amesema viongozi wa dini wapo tayari kuratibu mazungumzo baina ya Serikali na viongozi wa kisiasa, pamoja na vijana ili kutatuliwa kwa mambo yanayolalamikiwa.

Amesema kama ilivyofanyika kupitia kikosi kazi, ni muhimu kuangalia matakwa ya kundi la vijana ambao kwa kiasi kikubwa wapo mtaani baada ya kuhitimu vyuo, wengi wao wakilalamikia ukosefu wa ajira.

Hata hivyo, suala la maridhiano alilitaja Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiapishwa Novemba 3,2025 jijini Dodoma.

Rais Samia alisema ataendelea na juhudi alizoanzisha za kusaka maridhiano na mageuzi chini ya falsafa yake ya “4Rs”.  yaani Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).

“Niwasihi Watanzania, tuchague hekima badala ya ghadhabu, busara badala ya mihemko, upendo badala ya chuki, uvumilivu badala ya vinyongo, umoja badala ya mgawanyiko na amani badala ya vurugu,” alisema kwa msisitizo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum, amesema Tanzania imeingia kwenye mtihani mkubwa na hivyo inapaswa kusimama imara kuupokea mtihani huo na kuutafutia majibu haraka.

“Changamoto imetokea tuone namna ya kurejesha hali tuliyoizoea, sio jambo la busara kuharibu nchi ni busara viongozi wa dini na serikali kukaa kwa lengo moja la kuifanya Tanzania irejee katka hali yake ya amani na utulivu,” amesema.

Sheikh Salum amewataka viongozi kuwa na sikio la usikivu kwa kusikiliza malalamiko ya wananchi na wananchi kujifunza kufuata utaratibu na kutii mamlaka zilizopo.

“Kwa pamoja kila mtu akishika ncha yake, Tanzania itarudi mahali ambapo tulitarajia, haya tuliyopitia tupokee kama tulipitia. Tulidhani haiwezekani kwenye nchi yetu, lakini Mungu akatuonyesha inawezekana, kwa hiyo tusidharau haya yanayotokea, tuyafanyie kazi kwa kufuata utaratibu ili tuwe salama wote,” amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema yaliyotokea yatufunze umuhimu wa amani na umuhimu wa utulivu.

“Yaliyotokea yatufunze umuhimu wa kutatua changamoto na kutafuta haki bila kuleta fujo, sababu haki inaweza kutafutwa bila fujo, maana tulichokishuhudia ni fujo na vurugu, hata tafsiri ya maandamano haionekani hata kidogo,” amesema.

Sheikh Mataka amesema watu wenye lengo la kuandamana, huwa wanajipanga na kuelekea maeneo wanayotaka kufikisha ujumbe si hivi ilivyofanyika kwa watu waliosema wanaandamana kuanza kuvamia vituo vya mafuta, kuchoma moto vituo vya polisi.

“Hayo si maandamano hizo ni ghasia, hili litufunze. Ndani yake kulionekana dhuluma unapokwenda kuvamia gari ya mtu na kupora mali zake, yeye ni sehemu gani ya hayo unayoyadai wewe, tujifunze umuhimu wa kutafuta haki bila fujo. Unapodai haki yako lazima uchunge haki za mwingine,” amesema Sheikh Mataka.

Wito huo wa viogozi wa dini unakuja wakati tayari Rais Samia amepishwa Oktoba 3,2025 kushika muhula mwingine wa uongozi baada ya kuibuka na ushindi kwa kupata kura milioni 31 sawa na asilimia 97.6 za kura zilizopigwa.

Matokeo hayo yanampa nafasi Rais Samia aliyechukua madaraka kwa mara ya kwanza 2021, baada ya kifo cha mtangulizi wake, Dk John Magufuli, muhula mwingine wa pili wa kuiongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.