MABOSI wa TRA United wanadaiwa kumalizana na aliyekuwa Kocha wa Polisi Kenya, Etienne Ndayiragije muda mfupi baada ya kuachana na maafande hao aliofanya nao kazi kwa miezi 11 na kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya (KPL) msimu uliopita.
Kwa sasa TRA United ambayo zamani ilifahamika kama Tabora United baada ya awali kuachana na jina la Kitayosce inajiandaa kumtangaza Ndayiragije kuwa kocha mkuu na ataanza kazi hivi karibuni baada ya ligi kurejea upya tangu iliposimama.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya TRA kimeliambia Mwanaspoti kuwa kocha huyo atawasili nchini muda wowote kuanzia sasa na kuanza na majukumu haraka ili kuweza kuisaidia timu hiyo kufikia malengo iliyojiwekea mwanzoni mwa msimu huu.
“Ni kweli mambo yameenda sawa baada ya makubaliano ya pande zote mbili, hivyo huyo ndiye atakayekuwa kocha wetu mkuu na matarajio ni kujiunga na timu muda wowote kuanzia sasa ili kusukuma gurudumu tuliloanza nalo,” amesema mtu wa ndani ya uongozi wa timu hiyo:
“Kila kitu kinaenda vizuri kocha ataungana na timu na kuendelea pale tulipoishia malengo yalikuwa kujiunga na timu baada ya mchezo wetu dhidi ya Simba kutamatika lakini kwa mujibu wa mabadiliko yaliyotolewa na mamlaka atajiunga na timu na kuendelea na majukumu ikiwa ni pamoja na kuwa sehemu ya benchi mchezo wetu unaofuata.”
Kocha huyo raia wa Burundi ana uzoefu mkubwa na soka la Tanzania kwani amewahi kuzinoa Mbao FC, Geita Gold, KMC na Azam FC sambamba na timu ya taifa (Taifa Stars) kwa vipindi tofauti kabla ya kuibukia Kenya kuinoa Polisi na kuifikisha raundi ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyotolewa na Al Hilal ya Sudan.