Wakili Mwasipu afunguka yanayomkabili Heche

‎‎Dar es Salaam. Ikiwa ni takribani wiki mbili tangu Jeshi la Polisi limkamate John Heche ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Wakili wake, Hekima Mwasipu amesema kiongozi huyo anatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi, muda wowote atafikishwa mahakamani.‎

‎Wakili Mwasipu amesema tuhuma za ugaidi zilizoibuliwa kwa mteja wake zinahusiana na fujo wakati wa maandamano yaliyotokea Oktoba 29, 2025 eneo la Kimara hadi Magomeni, jijini Dar es Salaam wakati wa uchaguzi mkuu.

Awali, Heche alikamatwa eneo la Mahakama Kuu, Dar es Salaam, Oktoba 22,2025 alipokwenda kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini inayosikilizwa na mahakamani humo.‎

‎Idara ya Uhamiaji Oktoba 18, 2025 ilieleza kuwa,  katika Kituo cha Uhamiaji cha Mpaka wa Sirari mkoani Mara, Heche aliondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na kanuni za uhamiaji zilizoundwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54.‎

‎‎Leo Jumatano Novemba 5, 2025 akizungumza na Mwananchi Wakili Mwasipu amesema baada ya kuelezwa tuhuma zake alikataa kuhojiwa hadi wawepo mawakili wake.

‎‎”Anatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi, matukio yaliyotokea Kimara Dar es Salaam hadi Magomeni, Polisi wamesema wana ushahidi anahusika na muda wowote anaweza kupelekwa mahakamani,” amesema.‎

‎Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, Chacha Heche ambaye ni mdogo wake Heche aliandika jana Jumanne kwamba Heche amefikishwa Dar es salaam.‎

‎”Inasemekana amepelekwa kwa ZCO, (Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda ya Dar es Salaam) itakumbukwa kuwa Oktoba 2025 alipokamatwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kuona hawana shtaka naye,” amesema.

‎Mwananchi mara kadhaa imemtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kujua kinachoendelea lakini simu yake ilikuwa ikiita pasina kupokewa.

‎Tuhuma hizo dhidi ya Heche zimemuibua Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi ambaye amelaani vikali hatua ya Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Taifa (DPP) kumkamata na kumfungulia mashitaka ya ugaidi kiongozi huyo.‎

‎Mwabukusi amedai hatua hiyo ni kinyume cha sheria na kwamba inalenga kukandamiza demokrasia nchini.‎

‎Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Mwabukusi amesisitiza vyombo hivyo viwili, ‘vinamwaga petroli vikidhani vinazima moto’ kwa kumhusisha Heche na makosa ya ugaidi.‎

‎”Ofisi ya Mashtaka ya Taifa (DPP) na Polisi kwa matendo yao wanamwagia petroli wakidhani wanazima moto, ni…kumtuhumu John Heche kwa ugaidi. ‎‎Hali ya usalama siyo nzuri kuendelea na desturi zenu za kupika kesi ili kubambika watu, mnatia aibu taaluma na mnakera,” ameandika Mwabukusi.‎

‎‎Kwa mujibu wa Mwabukusi kupitia,  TLS itatoa msaada wa kisheria kwa Heche, pamoja na familia zilizodhulumiwa au kujeruhiwa wakati wa maandamano yaliyosababisha vifo na majeraha kwa vijana.‎

‎Kutojulikana alipo Heche

‎‎Oktoba 23, 2025 familia ya Heche ilizungumza na waandishi wa habari kuhoji alipo ndugu yao huku ikitoa siku moja kwa Jeshi la Polisi kueleza alipo kabla hawajaamua kumtafuta  wenyewe kwa kushirikiana na wananchi.

‎‎Siku hiyo hiyo chama chake kilihoji alipo kiongozi huyo baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam na baada ya muda Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alieleza kupata taarifa kuwa kiongozi huyo alipelekwa mkoani Dodoma.

‎‎Tangu wakati huo Chadema imekuwa ikisisitiza kama kiongozi huyo ana makosa ya afikishwe mahakamani.

Wakili Mwasipu alisema kuwa mwanasiasa huyo machachari anatarajiwa kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka hayo ya ugaidi.

Hata hivyo, licha ya Mwananchi kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu jana kuangalia kama angeweza kufikishwa mahakamani hapo lakini mpaka saa 11 jioni alikuwa hajafikishwa.

Baadaye Wakili Mwasipu alisema hata yeye bado anafuatilia kwa karibu kuona kama atafikishwa mahakamani leo au kesho kwa ajili ya kumpa msaada wa kisheria.