Unguja. Wakati Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ikiteua wajumbe wa viti maalumu wa Baraza la Wawakilishi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) nayo inatarajiwa kutoa orodha hiyo wakati wowote kuanzia sasa.
Tayari Rais Samia Suluhu Hassan, kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amewaita bungeni wabunge wateule kuanzia Novemba 8, 2025 kwa ajili ya kuanza kikao cha kwanza cha Bunge la 13.
Kwa mujibu wa Ibara ya 78 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi, kwa kufuata utaratibu uliowekwa, vitapendekeza kwa INEC majina ya wanawake kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa uwakilishi baina ya vyama vilivyoshinda uchaguzi katika majimbo na kupata viti bungeni.
Ibara hiyo inafafanua INEC ikiridhika kuwa mtu yeyote aliyependekezwa anazo sifa za kuwa mbunge, itamtangaza kuwa amechaguliwa kuwa mbunge na masharti ya ibara ya 83 ya Katiba yatatumika kuhusu kuchaguliwa kwa mtu huyo kuwa mbunge.
Majina ya watu waliopendekezwa na INEC yatatangazwa kama matokeo ya uchaguzi baada ya kuridhika kwamba masharti ya Katiba na Sheria yanayohusika yamezingatiwa.
Orodha ya majina ya wagombea wanawake iliyowasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi na kila chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu ndiyo itakayotumiwa na Tume ya Uchaguzi baada ya kushauriana na chama kinachohusika, kwa madhumuni ya kujaza nafasi husika.
Ni muhimu kufahamu kwamba kabla chama hakijapewa mgawanyo wake, ni lazima kitimize baadhi ya masharti ikiwemo kushiriki uchaguzi mkuu na kupata angalau asilimia tano ya kura halali katika uchaguzi wa wabunge.
Vilevile, ni lazima chama kipendekeze majina ya wagombea katika mpangilio wa upendeleo kwa Tume ya Uchaguzi. Waliopendekezwa wanatakiwa kujaza fomu za uteuzi na kuziwasilisha kwa Tume.
Chama lazima kiwasilishe mapendekezo ya majina ya wagombea kwa Tume siku 30 kabla ya uchaguzi. Chama kitapata idadi ya wabunge kwa kuzingatia uwiano wa jumla ya kura ambazo kimepata katika uchaguzi.
Baada kukamilika kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), imeteua wajumbe wa viti maalumu katika Baraza la Wawakilishi.
Kati ya wajumbe 20 walioteuliwa na ZEC, wajumbe 16 wanatokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) na wanne wanatokana na ACT Wazalendo.
ZEC imeteua wajumbe 16 kutoka CCM na wajumbe wanne kutoka ACT Wazalendo kunatokana na asilimia ya viti vya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walivyopata katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Katika uchaguzi huo, mgombea urais wa CCM, Dk Hussein Mwinyi alishinda kiti cha Rais kwa asilimia 74.8 dhidi ya washindani wake 10 baada ya kupata kura 448,892.
Katika kinyang’anyiro hicho, alifuatiwa na mgombea wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman aliyepata kura 139,399 sawa na asilimia 23.22 ya kura zote.
Kwa mujibu wa ZEC, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 717, 557 lakini waliopiga kura walikuwa 609, 096 sawa na asilimia 84.88. Kati ya kura hizo zilizoharibika ni kura 8,863 sawa na asilimia 1.46.
Kwa upande wa wawakilishi, CCM kimeshinda majimbo 40 kati ya 50 ya uchaguzi yaliyopo Zanzibar.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Novemba 4, 2025, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amesema uteuzi huo umefanyika chini ya masharti ya kifungu cha 67(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kifungu cha 55 (3) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018.
Walioteuliwa kwa upande wa CCM ni Zainab Khamis Shomari, Rahma Kassim Ali, Tabia Maulid Mwita, Fatma Ramadhan Mandoba, Riziki Pembe Juma, Maryam Said Khamis, Chumu Khamis Kombo, Lela Muhamed Mussa, Khadija Salum Ali na Zainab Abdalla Salum
Wengine ni Anna Athanas Paul, Aza January Joseph, Salha Moh’d Mwinjuma, Hudhaima Mbarak Tahir, Mwanaidi Kassim Mussa na Salma Mussa Bilali.
Na upande wa ACT Wazalendo, Jaji Kazi amewatangaza walioteuliwa kuwa ni Moza Mohamed Khamis, Jabu Makame Juma, Farida Amour Mohamed na Nassra Nassor Omar.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, Zanzibar inaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), vyama vinavyounda Serikali hiyo ni chama kilichoshinda na kinachofuatia kwa kupata zaidi ya asilimia 10 ya kura.
Kwa mantiki hiyo, Othman Masoud Othman anastahiki kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa katiba hiyo, Rais akiapishwa, ndani ya siku saba ateue Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Dk Mwinyi aliapishwa Novemba Mosi, 2025 katika uwanja wa New Amani Complex, mjini Unguja.
