ACT-Wazalendo kuingia SUK? | Mwananchi

Dar/Unguja. Wataingia ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) au watasusia? Hilo ni swali linalogonga vichwa vya viongozi na wanachama wa ACT- Wazalendo visiwani humo kwa sasa.

Hadi sasa bado viongozi wa ACT- Wazalendo, hawajatoa kauli yoyote wala mwelekeo kuhusu kuingia au kutoingia ndani ya SUK, licha kuwa na sifa zinazowawezesha kuunda Serikali pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Licha ya viongozi waandamizi wa ACT- Wazalendo kuketi katika vikao vilivyojadili uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, hadi sasa hawajatoka hadharani kuueleza umma na wanachama wao kuhusu msimamo wao.


Mwananchi inafahamu vikao hivyo vilifanyika kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali ikiwamo ofisi za ACT- Wazalendo, Vuga mjini Unguja.

Hata baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, viongozi hao wamekuwa kimya, ingawa Oktoba 31, 2025 baada ya ibada ya Ijumaa, Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Othman Masoud Othman aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, alitembea kwa miguu mitaa ya darajani na kuwasilimia wananchi huku akisema uchaguzi umekwisha.

Safari hiyo ilimfikisha hadi ofisi za Vuga alipozungumza na wanachama wa ACT- Wazalendo, akiwaambia licha ya kutokubaliana na matokeo hayo, hawana budi kuwa watulivu na hakuna uamuzi watakaoufanya pasipo baraka za wanachama.

“Kama ambavyo kila kinachofanyika tunakuwa kwenu kuwaomba ridhaa, hata hili hakuna uamuzi utakaotolewa na viongozi, lazima tutakuja kwenu nyinyi mtakachoazimia ndio tutakachotekeleza,” amesema Othman.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud akisalimiana na wanachama wa chama hicho, Pemba baada ya kuwasili kwa ziara ya kichama ya siku saba kuanzia leo Novemba 6,2025.



Katika Uchaguzi Mkuu ulifanyika Oktoba 29, 2025  ulioshindaniwa na wagombea 11, mgombea urais wa CCM, Dk Hussein Mwinyi alishinda kiti hicho kwa kura 448,892 sawa asilimia 74.8 akifuatiwa na Othman aliyepata kura 139,399 sawa na asilimia 23.22.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 717, 557 lakini waliopiga kura walikuwa 609, 096 sawa na asilimia 84.88. Kati ya kura hizo zilizoharibika ni kura 8,863 sawa na asilimia 1.46.

Kutokana na kura alizozipata Othman ambaye ni Makamu wa Rais wa Zanzibar anayemaliza muda wake, ana sifa zote za kurejea katika wadhifa huo atakaoutumikia kwa miaka mitano ijayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka, 1984 kupitia marekebisho ya mwaka 2010, ibara ya 39 (3), kifungu kidogo (1), Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, atateuliwa iwapo chama chake kitapa asilimia 10 au zaidi ya kura za urais.

Ingawa ACT -Wazalendo haijatoa mwelekeo kuhusu SUK, taarifa kutoka chanzo cha ndani ya chama hicho zinaeleza wataingia na kuunda Serikali hiyo kwa awamu ya tatu, baada ya mwaka 2015 kususia uchaguzi.

Dalili za ACT- Wazalendo, zimeanza kuonekana baada ya uongozi kuwaruhusu wawakilishi wao 10 walioshinda kuingia katika Baraza la Wawakilishi kwenda kujisajiri ili kukamilisha taratibu za kuwatumikia wananchi wa majimbo yao.

Leo Alhamisi Novemba 6, 2025 wakati wa mchakato wa kumpata Spika wa Baraza la Wawakilishi la 11, wawakilishi 14 wakiwamo wa viti maalumu wa ACT- Wazalendo walionekana wakishiriki mchakato huo, ambao Zubeir Ali Maulid aliibuka kidedea kwa mara nyingine.

Mbali na kushiriki mchakato huo, wawakilishi hao wamekula kiapo cha kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa miaka mitano ijayo.

Pia, viongozi waandamizi wa ACT-Wazalendo wakiongozwa na Othman pamoja na Ismail Jussa (Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Zanzibar), wameanza ziara ya siku saba Pemba.

Inaelezwa kuwa, lengo la ziara hiyo ni kuzungumza na wanachama na viongozi wa ACT- Wazalendo wote wa majimbo na mikoa ya chama hicho, kuhusu uchaguzi na msimamo wa chama kuhusu SUK.

Lengo jingine ni kuimarisha mshikamano wa wanachama na kufufua ari ya kisiasa ndani ya chama hicho.

ACT-Wazalendo imekuwa na utaratibu wa kukusanya maoni ya wanachama na viongozi wao kabla ya kuingia SUK kama ilivyofanya mwaka 2020, chini ya uenyekiti wa Maalim Seif Shariff Hamad (marehemu).

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ACT- Wazalendo iliulalamikia mchakato huo, ikidai ulighubikwa na kasoro mbalimbali zikiwamo za wagombea wao kuenguliwa, kura kuibwa, viongozi kujeruhiwa na wengine wakipoteza maisha.

Hata hivyo, baada ya kukaa chini na kutafakari kupitia vikao mbalimbali, ikiwamo kufanya ziara ya mashauriano na viongozi na wanachama wao Pemba na Unguja, chama kilituma jina Maalim Seif aliyeteuliwa na Mwinyi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Akizungumza kwa mara ya kwanza leo Alhamisi Novemba 6, 2025 tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu na wanachama na wafuasi wa chama hicho eneo la Gombani wilayani Chakechake, Othman amesema huu ni wakati wa Wazanzibari kusimama imara ili kulinda heshima na utu wa Zanzibar.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud akisalimiana na wanachama wa chama hicho, Pemba baada ya kuwasili kwa ziara ya kichama ya siku saba kuanzia leo Novemba 6,2025.



Othman amesema ACT-Wazalendo, itaendelea kusimama kidete kudai uchaguzi huru, haki na ushirikishwaji wa kweli wa wananchi katika uamuzi unaohusu mustakabali wa Taifa.

“Tunataka Zanzibar yenye uwazi, usawa na uadilifu, tunataka demokrasia inayojengwa juu ya misingi ya heshima na haki kwa wote. Huu ndio urithi tunaoutaka kwa vizazi vijavyo,”amesema.

Othman pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru wanachama kwa kuendelea kuwa na imani na chama, akiwataka kuendeleza juhudi za kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa umoja, maendeleo na uadilifu wa kisiasa.

Ziara ya Othman Masoud inatarajiwa kuendelea katika mikoa minne ya kichama kisiwani Pemba, atakapokutana na viongozi, wanachama na wananchi kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kujadili mustakabali wa siasa za Zanzibar.