Fadlu: Sikieni, Simba hii inatoboa CAF

SIMBA inaendelea na maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Bara ikitarajiwa kuvaana na JKT Tanzania, lakini kuna kocha aliyewahi kuinoa timu hiyo aliyepo Uarabuni amevunja ukimya na kuitabiria kufika mbali zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika  msimu huu.

Simba iliyocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco imetinga makundi ikipangwa Kundi D sambamba na timu za Esperance y Tunisia, Petro Atletico ya Angola na Stade Malien ya Mali.

Kupangwa kundi hilo lkumemfanya kocha wa zamani wa kikosi hicho, Fadlu Davids aliyepo Raja Casablanca ya Morocco aliyeifikisha Simba fainali ya CAF kushindwa kujizuia na kusema anaiona ikifika mbali zaidi katika michuano hiyo.

Kauli hiyo ya Fadlu imeungwa mkono pia na straika mpya wa timu hiyo, Jonathan Sowah aliyesema licha ya kupangwa na vigogo, lakini wachezaji wamejipanga kuhakikisha wanaondokana na jinamizi la kukwamia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Fadlu aliyeinoa Simba kwa msimu mmoja uliopita kabla ya kurejea Raja, amesema kwa namna anavyoiangalia na wapinzani iliopangwa nao kundi moja anaamini kabisa itatoboa kutoka makundi ya Ligi ya Mabingwa na kufika mbali zaidi.

Amesema Simba ni timu iliyokomaa kimataifa na uzoefu ilioupata katika Kombe la Shirikisho msimu uliopita utaipa nguvu zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa.

“Ninaamini kabisa kwa Simba kutokana na ubora wa wachezaji niliowaacha… ni wachezaji wenye ubora wa kimataifa na mashabiki ambao mara zote wamekuwa nyuma ya timu. Ninaamini watapita hatua ya makundi kwenda mbali zaidi,” amesema Fadlu.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini ameongeza: “Uzoefu wa kupambana na timu za Afrika Kaskazini ndio utakaokuwa silaha kubwa kwa Simba, hasa ikizingatiwa watakutana na Espérance de Tunis, Petro de Luanda na Stade Malien katika Kundi D.”

Fadlu alisema kama watakomaa kwa kila mechi hasa za nyumbani, basi itaenda kuwapa heshima ya kufika mbali zaidi ya ilivyozoeleka katika Kombe la Shirikisho.

Fadlu anakumbukwa vyema na mashabiki wa Simba kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata ndani ya muda mfupi.

Aliiongoza timu hiyo kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita hatua ambayo ilikuwa ya kihistoria kwa klabu hiyo na soka la Tanzania.

Katika fainali hiyo Simba ilipoteza kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane ya Morocco baada ya kufungwa 2-0 kwenye mechi ya kwanza nchini Morocco na kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye marudiano yaliyofanyika Zanzibar.

Fadlu alisema anatambua changamoto za makundi, lakini alisema Simba inaweza kupenya ikiwa itaimarisha nidhamu ya mchezo na umakini katika mechi za ugenini.

“Kinachohitajiwa ni nidhamu ya timu na kuamini katika mpango yao. Timu kama Espérance ni ngumu, lakini Simba inaweza kuwashangaza,” amesisitiza kocha huyo.

Kwa upande wa Sowah aliyetua msimu huu kutoka Singida Black Stars ameliambia Mwanaspoti kuwa sio kundi gumu walilopangwa, lakini wanahitaji kujipanga na kuwasikiliza makocha na viongozi wa klabu yao.

“Hatuna wasiwasi kutokana na ubora wa kikosi chetu kimekamilika. Kitu muhimu ni kuendelea kuimarika kwa kuwa tulikuwa tunaendelea kuzoea na kujifunza mbinu za kocha,” amesema Sowah na kuongeza:

“Simba ina kikosi kipana na wapo wachezaji wenye uzoefu na michuano ya kimataifa, hivyo presha haitakuwa kubwa kwa upande wetu.”

Simba imepangwa kuanza mechi za makundi nyumbani dhidi ya Petro du Luanda kabla ya kuvaana na Stade Malien ndani ya mwezi huu wa Novemba kabla ya kuvaana na Esperance ya Tunisia mapema mwakani.

Mechi za awali zimepangwa kupigwa kati ya Novemba 21 hadi 23 na zile za raundi ya pili zitapigwa Novemba 28 hadi 30 na mechi za mwisho za makundi zitapigwa kati ya Februari 13 hadi 15.