KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars Miguel Gamondi amemrejesha nyota wa Aalborg BK ya Denmark katika kikosi cha timu hiyo kitakachoingia kambini kwa mechi ya kirafiki kalenda ya FIFA dhidi ya Kuwait utakaochezwa Novemba 14 jijini Cairo, Misri.
Kelvin aliitwaa mara ya mwisho katika kikosi hicho enzi kikiwa chini ya kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ Machi 14 mwaka huu wakati wakijiandaa mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco.
Tangu hapo hakuitwa tena, licha ya kuanza vizuri msimu wa 2025/26 akiwa na kikosi cha Aalborg BK kinachoshiriki Ligi Daraja la Kwanza huko Denmark ambapo ni msimu wake wa pili mfululizo.
Chini ya Gamondi, mshambuliaji huyo ameitwa kwa mara nyingine tena akiwa mhimili mkubwa wa safu ya ushambuliaji ya Aalborg, akifunga mabao saba na asisti tatu kwenye mechi 15 alizocheza.
Kelvin ameitwa wakati nahodha wa Stars, Mbwana Samatta anayekipiga Le Havre ya Ligi Kuu Ufaransa na Simon Msuva wa Al Talaba wa Iraq wakikaushiwa kama ilivyokuwa katika kikosi cha mwisho kilichokuwa kikisaka fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Zambia.
Katika kikosi kilichotangzwa mapema asubuhi ya leo Alhamisi, kocha Gamondi amewaita makipa, Yakoub Suleiman (Simba), Hussein Masalanga (Singida BS) na Zuberi Foba (Azam FC).
Wengine ni, Bakari Mwamnyeto (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Mohamed Hussein (Yanga), Alphonce Mabula (Shamakhi, Azerbaijan), Feisal Salum (Azam FC), Morice Abraham (Simba), Abdul Suleiman (Azam FC)na Paul Peter (JKT Tanzania).
Pia kuna Mudathir Yahya (Yanga), Wilson Nangu (Simba), Novatus Dismas (Göztepe FC, Uturuki), Pascal Msindo (Azam FC), Ibrahim Abdulla (Yanga), Haji Mnoga (Salford City, Uingereza), Dickson Job (Yanga), Habibu Idd (Singida BS), Tarryn Allarakhia (Rochdale AFC, England), Charles M’Mombwa (Floriana FC, Malta), Seleman Mwalimu (Simba).