Himid Mao mzuka umepanda Azam FC

KIUNGO mkabaji wa Azam FC, Himid Mao amesema kikosi cha timu hiyo ukiondoa ubora iliyonayo, lakini anafurahia kuona kimekomaa kiushindani na ana matarajio makubwa katika michuano ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika kuendeleza rekodi.

Kiungo huyo mkongwe na mtoto wa nyota wa zamani wa kimataifa aliyewahi kutamba nchini na klabu tofauti na timu ya taifa, Taifa Stars, Mao Mkami ‘Ball Dancer’ amerejea Azam msimu huu baada ya kuuzwa huko Misri na kuzitumika klabu tofauti nchini humo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Himid amesema wana hatua ngumu zaidi kuendelea walipoishia kimataifa, lakini kwa ligi ya ndani kutokana na ubora wanaouonyesha wanatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa timu pinzani.

“Haitakuwa rahisi lakini najivunia kuwa sehemu ya kikosi ambacho kimeandika historia kimataifa na  ubora mkubwa unaoonyeshwa na wachezaji ni ukomavu walionao baada ya kukosa kwa misimu mingi, naona kikosi kikiimarika,” amesema Himid na kuongeza;

“Wachezaji waliopo wana ukomavu wa hali ya juu hapa tulipofika itabaki historia na bado tunahitaji kuwa na mwendelezo bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuona Azam FC siku moja inaleta taji la Afrika hili linawezekana tumesahau yaliyopita tumerudi kwenye ushindani mpya.”

Himid amesema kurudi kwa ligi ni sehemu sahihi kwao kurejesha furaha kwa mashabiki wao, lakini jamii inayopenda mpira wao kama wachezaji matarajio yao ni kuendelea walipoishi kwa kuwa na muendelezo wa ushindi kwenye kila mchezo ulio mbele yao.

HIMI 01


“Furaha ya kufuzu hatua ya makundi tumeshaisahau tunarudi ligi kuu kusaka nafasi ya uwakilishi kimataifa msimu ujao ili kuendelea kujijengea uhakika wa kupata uwakilishi na hatimaye kutwaa mataji ya Afrika,”

“Tunafahamu ugumu uliopo kwenye ligi kutokana na sajili bora zilizofanywa na wapinzani, lakini hilo halituondoi kwenye malengo, tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha mambo yanaenda kama tulivyopanga.”

Akizungumzia droo ya Kombe la Shirikisho Afrika amesema wamepangwa kundi bora na matarajio ni kuona wanafanya vizuri kwa kupata nafasi ya kutinga hatua inayofuata.

HIMI 02


“Timu zote ni bora na shindani na ndiyo maana zimefika hatua hiyo. Hakuna mteremko mipango imara na ubora wetu ndiyo utaamua ni timu gani itaenda hatua inayofuata. Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kuipambania nembo ya klabu,”

“Ukizingatia tupo na benchi bora la ufundi ambalo lina uzoefu mzuri na michuano ya mikataifa imani yetu ni kubwa tutakuwa bora na kutinga hatua inayofuata bila kuangalia tunashindana na nani sisi tunaamini katika kujiandaa vyema na kutumia kila nafasi tutakayotengeneza ili kufikia malengo.”

Himid ni mmoja ya nyota waliotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa na Azam msimu wa 2013-2014 na kubeba Kombe la Kagame 2015 kabla ya Januari 2018, mwaka ambao timu hiyo ilibeba tena taji hilo na kuuzwa Petrojet ya Misri.