Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetoa hati ya wito wa kufika mahakamani hapo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) na wenzake watano, kuhusiana na sakata la kushikiliwa kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, John Heche.
Mahakama hiyo imetoa wito huo kufuatia shauri la maombi lililofunguliwa mahakamani hapo na mawakili wa Chadema kwa niaba ya Heche, wakiomba amri ya Mahakama kuwataka wajibu maombi kumfikisha mahakamani kiongozi huyo au limwachie kwa dhamana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Wakili Gaston Garubindi, shauri hilo limesajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na limengiwa kusikilizwa na Jaji Obadia Bwegoge.
Katika shauri hilo ambalo mwombaji ni Heche mwenyewe, wajibu maombi ni IGP ambaye ndiye mjibu maombi wa kwanza na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu (Dar es Salaam -ZCO).
Wajibu maombi wengine ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (RCO), Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG ).
“Kesi imepangwa kusikilizwa kesho (Ijumaa Novemba 7, 2025) saa 4:00 asubuhi,” amesema Wakili Garubindi alipoulizwa na Mwananchi, baada ya kupata hati za wito wa Mahakama kwa ajili ya wajibu maombi.
Kabla ya kufungua maombi hayo Mahakama Kuu Dar es Salaam, awali mawakili hao walifungua maombi hayo Mahakama Kuu Dodoma, ambako Heche alikuwa akishikiliwa kwa siku kadhaa.
Hata hivyo, maombi hayo hayakuwahi kusajiliwa katika mfumo wa Mashauri wa Mahakama kutokana na changamoto ya kimtandao.
Baadaye Heche alisafirishwa kurudishwa Dar es Salaam, ndipo nao wakafungua maombi haya ambayo yamesajiliwa rasmi leo Novemba 6, 2025 na kupangiwa jaji wa kuyasikiliza.
Heche anashikiliwa na Polisi tangu Oktoba 22, 2025 alipokamatwa nje ya geti la Mahakama Kuu Dar es Salaam, alipokuwa akienda mahakamani hapo kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini.
Baada ya kukamatwa, awali chama hicho kilitoa taarifa kwa umma kuwa Jeshi la Polisi Dar es Salaam liliwaeleza kwamba mwanasiasa huyo amesafirishwa kupelekwa Tarime, Mara, lakini familia na ndugu zake walipomtafuta katika vituo vya Polisi Tarime na Musoma hawakumpata.
Hata hivyo, baadaye ilifahamika kuwa alipelekwa Dodoma ambako alikuwa anashikiliwa katika kituo cha Polisi Mtumba, bila kumpatia dhamana wala kumfikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hata hivyo, katika taarifa iliyotolewa na Wakili Hekima Mwasipu juzi, Novemba 4, 2025, Heche alisafirishwa tena siku hiyo kurejeshwa Dar es Salaam ambapo alifikishwa katika kituo cha Polisi Mburahati, Mkoa wa Polisi Kinondoni na kuhojiwa kwa tuhuma za vitendo vya ugaidi.
“Amepewa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kigaidi kutoka Kimara mpaka Magomeni na kujihusisha na vitendo vya kigaidi maeneo ya Msewe na Extenal,” alisema Wakili Mwasipu katika taarifa yake hiyo.
Wakili Mwasipu alisema baada ya kutakiwa kuandika maelezo ya onyo Heche alitumia haki yake ya kisheria ya kukataa kuandika maelezo na kwamba atatumia haki hiyo baada ya kupelekwa mahakamani.
Wakati maombi hayo yamesajiliwa leo, Mahakama Kuu na kupangiwa kusikilizwa kesho, taarifa zilizomo ni kwamba Heche anatarajiwa kufikishwa mahakamani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, kusomewa mashtaka hayo.
Tangu asubuhi hali ya ulinzi imeimarishwa katika eneo la Mahakama ya Kisutu ambapo askari polisi waliovaa sare na wengine kiraia wamesambaa maeneo mbalimbali ndani na nje ya viwanja vya mahakama hiyo.
Hata hivyo mpaka saa 10 jioni ya leo hajafikishwa mahakamani lakini taarifa ambazo Mwananchi limezipata zinaeleza kuwa, hati ya mashtaka yake haijasajiliwa katika mfumo wa Mahakama kutokana na changamoto ya mtandao.