Kocha Uhamiaji afichua siri Ligi Kuu Zanzibar

KOCHA Mkuu wa Uhamiaji, Abdul Saleh Mohammed, amesema timu hiyo imefanya mabadiliko makubwa msimu huu wa 2025-2026 na ndio siri ya kupata matokeo mazuri katika mechi zinazoendelea za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).

Licha ya kumaliza nafasi ya sita msimu uliopita, timu hiyo haikuwa bora sana kama inavyoonekana kipindi hiki kwa kucheza soka la kuvutia zaidi ikitoa ushindani ambapo katika mechi tano kabla ya leo Alhamisi jioni Novemba 6, 2025 kupambana na Zimamoto, imevuna alama 13 ikishinda nne na sare moja, huku ikifunga mabao 13 na kuruhusu matatu.

Kocha Abdul amesema matokeo hayo hayakuja kirahisi bali amefanya mabadiliko makubwa kwa kuwajenga wachezaji kisaikolojia akilenga kuwarudisha kucheza soka la ushindani na kuvitumia vipaji vyao inavyostahili.

“Baada ya kumaliza vibaya msimu uliopita, wachezaji wengi hawakuwa sawa kisaikolojia, nilitumia mbinu mbadala za kuwafanya warudi mchezoni kufanya vizuri,” amesema Abdul.

Mbali na hilo, kocha huyo amesema msimu huu wamesajili vijana wenye vipaji zaidi na wamekuwa chachu ya mabadiliko kwao na matunda yanaonekana kwani viongozi na mashabiki imani yao imerudi kwa kasi kubwa kwa timu hiyo.

UHA 01


Kabla ya kucheza na Zimamoto leo jioni, Uhamiaji haijapoteza mechi yoyote msimu huu kwenye ligi ambapo kocha Mohamed amesema nidhamu iliyopo katika safu ya ulinzi imekuwa ikiwabeba zaidi na kuwafanya wapinzani kushindwa kulifikia kirahisi lango lao.

Mbali na hilo, amefichua kwamba amekuwa na kawaida ya kuangalia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na kundi kwa lengo la kuwaweka vizuri.

Licha ya hayo yote, kocha huyo amesema anakutana na changamoto kubwa katika upangaji wa kikosi kinachoanza katika mechi mbalimbali kwani anaona kila mchezaji anastahili kuwamo.

UHA 02


Sambamba na hilo, amewataka mashabiki wa timu hiyo kufika uwanjani kwa wingi kushuhudia burudani inayotolewa na Uhamiaji.

Msimu huu Uhamiaji ndio timu inayoongoza kwa mabao katika Ligi Kuu Zanzibar ikicheka na nyavu mara 13 baada ya mechi tano, ikifuatiwa na Malindi yenye 11 ikishuka dimbani mara sita.

Uhamiaji ilianza msimu huu kwa rekodi mbili ambazo ni mchezaji wake Adam Issa kuonyeshwa kadi nyekundu ikiwa ndiyo ya kwanza msimu huu, huku Mohamed Mussa akifungua pazia la kufunga bao la kwanza la msimu katika mechi iliyochezwa Septemba 25, 2025 kwenye uwanja wa Mao A, Mjini Unguja dhidi ya Polisi iliposhinda 1-0.