MSHAMBULIAJI wa Coastal Union, Athuman Masumbuko ‘Makambo Jr’ ameshtukia jambo katika kikosi hicho ikiwa ni msimu wake wa kwanza, huku akisema hana furaha ya kufunga kama mabao yake hayawabebi Wagosi wa Kaya.
Makambo alijiunga na Coastal msimu huu akitokea SC Victoria 06 Griesheim ya Ujerumani alipokuwa kwa mkopo akitokea 1.FCA Darmstadt ya nchini humo na hadi sasa amefunga mabao mawili akiwa ni miongoni mwa wachezaji wanane waliopo nyuma ya vinara wa orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu, Saleh Karabaka na Paul Peter wa JKT TZ.
Mshambuliaji huyo chipukizi aliitumikia 1.FCA Darmstadt tangu Julai 25, 2024 kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Mashujaa aliyojiunga nayo msimu wa 2023-2024, baada ya kuonyesha kiwango kizuri wakati akicheza timu ya vijana ya Mtibwa Sugar U20.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makambo Jr amesema lengo lake kama mshambuliaji sio kuongoza orodha ya ufungaji mabao wala binafsi bali kuhakikisha timu inapata ushindi katika kila mechi na ameshtuka kuona mabao yake hayajaibeba Coastal hadi sasa.
“Kufunga ni jambo zuri kwa mchezaji yeyote wa nafasi yangu, lakini halina maana kama timu haishindi, tuna malengo makubwa msimu huu na ushindi wa timu ndiyo kipaumbele chetu na unaweka furaha kwa mashabiki wetu,” amesema Makambo na kuongeza;
“Kiukweli hatujaanza vizuri ligi kuu na hilo linatokana na sababu nyingi, kwanza ligi imekuwa na ushindani, sasa hivi timu yoyote inaweza kupata matokeo ugenini kama itajipanga vizuri, tunaamini kwa muda tuliopata wa kurekebisha makosa, basi utakuwa mzuri tutakaporejea tena.”
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Mashujaa amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu, akifunga mabao mawili na asisti moja katika mechi tano za Ligi Kuu Bara, lakini Coastal Union imekuwa ikipoteza pointi muhimu katika dakika za mwisho.
Katika mechi tano Coastal imeshinda moja, sare mbili na kupoteza mbili ikiwa nafasi ya 11 ya msimamo wa Ligi Kuu unaoongozwa na Mbeya City iliyopanda daraja msimu huu.
Mbeya inaongoza kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa ikiwa na pointi nane kama ilizonazo Pamba Jiji licha ya kutofautiana idadi ya mechi ilizocheza, City ikicheza sita na wenzao wakicheza tano hadi sasa.