Dar/Mikoani. Wakati Samia Suluhu Hassan akila kiapo cha kuwatumikia Watanzania kwa miaka mitano ijayo, mambo 10 mahususi yanamsubiri katika utawala wake katika kipindi chake cha pili.
Samia ameapishwa kuwa Rais, Novemba 3, 2025 na Jaji Mkuu, Profesa George Masaju, katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Gwaride, Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Anakuwa Rais wa kwanza mwanamke kuchaguliwa na Watanzania kuwa Rais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025. Alishinda kwa kupata kura milioni 31 sawa na asilimia 97.6 ya kura milioni 32 zilizopigwa.
Waliomtangulia ni Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli. Mwalimu Nyerere, Mwinyi, Mkapa na Magufuli wameshafariki dunia kwa nyakati tofauti.
Miongoni mwa mambo yanayomsubiri Rais Samia ni kutuliza joto la hali ya demokrasia na vumbi la uchaguzi lililomalizika kwa kuacha vilio na machungu, kuhakikisha usalama wa raia baada ya hofu kutanda kutokana na madai ya watu kutekwa na kupotea, ukamilifu wa miradi mikubwa, hususan ya ujenzi wa miundombinu kama Reli ya Kisasa (SGR).
Aidha, anatakiwa kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana, ambao kila mwaka wanaongezeka mitaani huku nafasi za ajira zikiwa finyu, pamoja na kupokea wahitimu wa elimu ya msingi wakiwa kwa mara ya kwanza katika makundi mawili la sita na la saba wakati elimu ya sekondari ni ya lazima chini ya mtaala mpya.
Mambo mengine ni kutekeleza ahadi za ilani ya CCM alizozitoa katika maeneo mbalimbali, hususan ahadi ya Katiba mpya, bima ya afya kwa wote, na kupambana na udumavu wa watoto pamoja na uanzishaji wa kongani za viwanda.
Jambo lingine linalomsubiri kiongozi huyo mkuu wa nchi ni kuendeleza heshima kwenye michezo, ambapo baada ya kuwa miongoni mwa wenyeji wa michuano ya CHAN, Tanzania inatarajia tena kuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Katika mashindano hayo, Tanzania itashirikiana na mataifa jirani ya Uganda na Kenya kuandaa michuano hiyo kwa mara ya kwanza, jambo ambalo Watanzania wanasubiri kwa hamu, wakiamini litachangia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa Taifa kwa ujumla.
Jambo la tisa, Rais Samia anapaswa kuendelea kusimamia mazingira bora kwa wafanyabiashara, hususan katika masuala ya kodi yanayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili kodi ilipwe bila kutumia mabavu.
Jambo la kumi ni suala la Katiba mpya, ambalo limekuwa likipigiwa kelele na wadau mbalimbali wakiwamo vyama vya upinzani, wanaoamini kwamba kuwepo kwa mabadiliko ya Katiba mpya kutaleta uwiano miongoni mwa Watanzania.
Katiba mpya inatajwa kuwa sehemu muhimu ya kuweka maridhiano yanayohitajika baada ya kuondoa baadhi ya vifungu ambavyo havijawekwa sawa, na kuweka vipengele vinavyohitajika kwa mustakabali wa Taifa.
Aidha, suala la Muungano ni eneo nyeti linalomsubiri Rais Samia, ambapo wengi wanatarajia kuona usawa na uwiano kwa wananchi wa Visiwani na Bara katika kudumisha Muungano wa pande mbili.
Maeneo mengine yanayosubiriwa katika utawala wa Rais Samia ni kuhakikisha uchumi jumuishi kwa kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja kupitia fursa za sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na viwanda, ili kumpa nafasi Mtanzania kujiajiri, kuajiri na kuajiriwa.
Suala la demokrasia na haki pia ni sehemu ya changamoto zinazomsubiri kiongozi huyo, kwani baadhi ya vyama vya siasa, hasa vya upinzani, vinaona bado hakuna usawa katika utekelezaji wa haki za kisiasa na kijamii.
Pamoja na hayo, jambo jingine muhimu ni kuunda Baraza la Mawaziri na kumpata Waziri Mkuu mpya, ambao watakuwa wasaidizi wake wa karibu katika kutekeleza majukumu ya Serikali kwa Watanzania.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, George Kahangwa, amesema Rais Samia analazimika kuteua wasaidizi wenye uwezo wa hali ya juu kiweledi, kizalendo na kiutendaji.
“Asiteue Waziri Mkuu ilimradi, aunde Baraza la Mawaziri makini watupu. Kila atakayemteua, yafaa ampe vigezo vya wazi vya upimaji wa utendaji wake (KPIs). Awapime kwa muda mfupi na mrefu,” amesema Profesa Kahangwa.
Mhadhiri huyo amesema mkuu huyo wa nchi afanye ushirikishaji wa kipekee wa makundi yote ya kijamii, ili Taifa lote liende pamoja na kuziba kila ufa.
“Utekelezaji wa miradi kwa ukamilifu unahitaji fedha nyingi, na kwa hiyo uchumi imara. Hakuna muujiza bila uchumi imara. Lazima awe na mikakati dhabiti ya kuhakikisha uchumi unakua kwa kasi,” amesema.
Profesa Kahangwa ameongeza: “Rais wetu atahitaji kwa kiasi kikubwa wataalamu wa nyanja mbalimbali (Taifa linao), ili uamuzi wake wote uwe na taarifa toshelezi na utaalamu sahihi.”
Kuhusu hoja ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Governance Links, Donald Kasongi, amesema Waziri Mkuu ajaye ni lazima awe mkali katika kusimamia shughuli zote za Serikali, kwa kuwa ndiye anayejibu hoja za Serikali bungeni.
“Yeye ndiye kiranja mkuu wa mawaziri wote, hivyo ni lazima awe mtu mwenye misimamo katika kufuatilia shughuli zote za Serikali zisiyumbe, kwa sababu asipofanya hivyo, walio chini yake hawatatekeleza majukumu yao,” amesema Kasongi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Erasto Kano, amesema Waziri Mkuu anayetakiwa kwa wakati huu ni yule mwenye uwezo wa kusimamia shughuli zote za Serikali kwa umakini na ukali wa hali ya juu.
“Tunataka Waziri Mkuu ambaye akizungumza, sauti yake iwe na mamlaka, na kila analolisimamia lifanikiwe kwa kiwango kikubwa, si mtu mpole ambaye atashindwa kusimamia majukumu yake,” amesema Dk Kano.
Aidha, amesema ni wakati mzuri sasa kwa Rais Samia kupanga safu yake ya uongozi vizuri, akiwemo Waziri Mkuu mchapa kazi atakayemsaidia kutekeleza majukumu ya kila siku.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. John’s cha Jijini Dodoma, Dk Assad Kipanga, amesema wanamtaka Waziri Mkuu ambaye hana kashfa yoyote kuhusu mwenendo wake wa maisha ya kawaida na hajawahi kutuhumiwa kwa rushwa.
“Bado tuna viongozi wazuri kwenye nchi yetu ambao wanaweza kutuvusha katika hali tuliyonayo na kutupeleka kwenye hali bora zaidi. Tunamtaka Waziri Mkuu ambaye ataponya majeraha ya wananchi badala ya kuyaendeleza,” amesema Dk Kipanga.
Kwa upande wake, mdau wa elimu jijini Mbeya, Charles Ernest, amesema licha ya Serikali kujenga shule nyingi za msingi na sekondari, bado kuna uhaba wa walimu, akishauri Rais aone namna ya kuongeza ajira za walimu.
Amesema wazazi na walezi wamejitahidi kupeleka watoto shule, ila michango imekuwa tatizo, huku idadi ya wanafunzi ikiwa haina uwiano sawa na walimu, jambo linaloathiri ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.
“Binafsi nashauri Rais Samia aangalie upande wa walimu, kwa kuwa upande wa miundombinu ya shule amefanikiwa, lakini idadi ya wanafunzi ni kubwa. Michango iishe ili tuthibitishe maana halisi ya elimu bure,” amesema Ernest.
Naye Selina Mathias amesema kilio kikubwa kwa wananchi wa maeneo ya mjini na vijijini ni huduma ya maji safi, akiomba awamu ijayo ilitazame zaidi.
“Maji ndiyo uhai wa binadamu, tunaomba Rais Samia aelekeze mamlaka zake kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi, hali ni mbaya,” amesema Selina.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, amesema licha ya kwamba tayari Rais Samia ameanza utekelezaji, anashauri kuunganisha Taifa kuwa moja na kuendeleza maridhiano kupitia falsafa yake ya 4R’s.
Amesema miradi iliyoanza na kuendelea kutekelezwa inapaswa kukamilika, kwani ameonyesha sura ya maendeleo. Ameomba Watanzania waungane kuhakikisha Taifa linasonga mbele kimataifa na kudumisha amani na mshikamano.
“Sehemu ya maridhiano ameshaonesha njia. Mambo ya uchaguzi sasa yapite, tuungane kumuunga mkono katika kutekeleza ilani ya chama chake na kutuletea maendeleo Watanzania.
“Ipo miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake, tumeona namna anavyopambana kuikamilisha, na mingine imekamilika tayari. Sasa jukumu letu ni kumuombea aweze kutupa mwelekeo mpya,” amesema kiongozi huyo wa Kamati ya Amani mkoani Mwanza na kuongeza;
“Kumbuka, huyu Rais alipokea kijiti katika hali ya dharura sana, lakini kwa uweledi wake amejitahidi kuunganisha Watanzania kupitia falsafa yake ya 4R’s. Kwa maana hiyo, tunatarajia kwa miaka mitano yake rasmi atatuvusha zaidi.”
Mchungaji wa Kanisa la Mlima Moto lililopo Mafinga, mkoani Iringa, John Mgina, amesema Rais Samia ni vyema akaweka mkazo katika kuunganisha makundi yote ya kijamii ili kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Amesema ni muhimu viongozi wote wa dini na wananchi kwa ujumla kuendelea kuiombea nchi na uongozi wake kwa ajili ya amani, umoja na maelewano ya kitaifa.
“Kuna haja ya Serikali kuendelea kuboresha huduma muhimu kama barabara na afya, hususan maeneo ya vijijini, ili kuleta maendeleo ya usawa kwa Watanzania wote. Kwa kipindi kilichopita, tumeona kasi ya maendeleo aliyofanya,” amesema Mchungaji huyo.