MWANDISHI WA HABARI MANENO SELANYIKA AFARIKI DUNIA


::::::

Mwandishi wa habari , Maneno Selanyika aliyefariki dunia Oktoba 29, 2025, wakati akiwa njiani kuelekea dukani karibu na makazi yake, baada ya kukumbana na vurugu zilizozuka eneo hilo kwa siku hiyo.

 Taarifa kutoka kwa familia na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC) zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea ghafla na kusababisha kifo chake papo hapo.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya familia, mwili wa marehemu haujapatikana hadi sasa, hivyo uamuzi umefikiwa kusafirisha msiba bila mwili kuelekea Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, kesho Novemba 7, 2025, kwa ajili ya kuanua tanga na kufanya ibada maalumu ya kumuombea.

Uongozi wa DAR-PC umesema umeupokea msiba huo kwa huzuni na masikitiko makubwa, ukimwelezea marehemu kama mwandishi mwenye weledi, umakini na uadilifu mkubwa katika kuripoti habari za mahakama, elimu, kijamii na jinsia. Enzi za uhai wake, marehemu Maneno alihudumu katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo gazeti la Mtanzania.

Aidha, marehemu alikuwa mwanachama hai na mwenye kujituma ndani ya DAR-PC, akichangia kikamilifu katika shughuli na malengo ya klabu hiyo. 

Uongozi wa DAR-PC umetuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na wanahabari wote walioguswa na msiba huu, ukimuombea 

Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.