SIMBA inapiga hesabu ndefu za namna gani itaingia katika mechi sita za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, ili itoboe tena kwenda robo fainali, lakini makali ya kikosi hicho kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita yakamshtua beki mmoja wa Waarabu akisema kwa Wekundu hao kazi watakuwa nayo si kitoto.
Simba iliyopoteza fainali ya CAF mbele ya RS Berkane ya Morocco, msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa Kundi D lenye timu za Esperance de Tunis ya Tunisia, Petro de Luanda ya Angola na Stade Malien ya Mali.
Wekundu hao wataanzia nyumbani dhidi ya Petro de Luanda kisha itaifuata Malien na baadaye Esperance lakini utamu zaidi ni Wekundu hao watamalizia mechi za makundi nyumbani.
Beki Ibrahima Keita anayeichezea Esperance, ameiambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kwamba kundi hilo sio rahisi wala gumu sana, lakini presha yake ipo kwa Simba.
Keita raia wa Mauritania mwenye asili ya Mali, amesema ukiacha Petro de Luanda, Simba ndio mpinzani mtata ambaye rekodi yake inawafanya kuwa makini kukabuliana nao.
Beki huyo ambaye aliwahi kuhitajiwa na Yanga akiwa TP Mazembe, amesema timu yao lazima ishinde vizuri nyumbani kabla ya kwenda kurudiana na Wekundu hao ugenini.
Keita amesema, Simba ina rekodi ngumu ikiwa nyumbani na kama watafanya makosa ya kutoshinda kwenye mechi mbili za kwanza za ugenini wakitangulia kutoka kuwafuata Petro de Luanda kisha Simba itawatibulia hesabu zao.
Ratiba inaonyesha Simba itakutana na Waarabu hao Januari 23, 2026 katika mechi ya kwanza ikianzia ugenini nchini Tunisia, kisha kurudiana Januari 30, 2026 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Hakuna shida ya ratiba ambayo imetoka, huwezi kusema rahisi sana au itakuwa ngumu, tuna timu nzuri, timu ambazo tutakutana nazo zinatofautiana kwa ubora kulingana na rekodi zake,” amesema Keita ambaye ni beki anayejua kukaba na kupandisha mashambulizi.
“Naijua Stade Malien, lakini kukabiliana na timu kama Petro na Simba haitakuwa rahisi hasa hao Simba, ukiangalia rekodi zao hasa wakiwa nyumbani tunatakiwa kujipanga sana kama tukitaka kushinda hapo.”
Beki huyo ameongeza; “Nimekuja Tanzania mara kadhaa lakini nilikutana na Yanga wakati nikiwa Mazembe, ilikuwa ngumu sana lakini ukiuliza unaambiwa Simba ndio wagumu zaidi kupoteza nyumbani.
“Bahati nzuri tutaanzia nyumbani, itakuwa ngumu wao kushinda hapa lakini tukiwafuata kwao tutatakiwa kuwa makini sana lakini tutaanzia kutoka kwenda Angola, tutajipanga tuanzie kufanya vizuri huko.”
Aidha Keita ameongeza kwamba nguvu ya mashabiki wao wakiwa Tunisia haitofautiani na ya mashabiki wa Simba wakiwa nyumbani.
Kwa rekodi za msimu uliopita katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ilicheza mechi saba za nyumbani ikishinda sita na kutoka sare moja tu dhidi ya Berkane katika fainali, huku kwa mechi zote 14 za jumla kwa msimu huo kuanzia raundi ya pili hadi fainali, ilicheza 14, ikishinda saba, sare nne na kupoteza tatu zote zikiwa za ugenini.