Simba, Yanga kuaga mwaka kwa dabi

WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likisogeza mbele kuanza kwa mechi za msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), wababe wa ligi hiyo Simba na Yanga zenyewe zitauaga mwaka 2025 kwa kuvaana katika Dabi ya Kariakoo Desemba 28.

Awali ligi hiyo iliyozinduliwa mwezi uliopita kwa mechi za Ngao ya Jamii, ilipangwa kuanza jana Alhamisi, lakini sasa imetangazwa imesogezwa mbele hadi Novemba 14 kwa kupigwa michezo minne, huku mbili za raundi ya kwanza zikipangwa Desemba 8.

Mechi ya watetezi wa taji la Ligi hiyo, JKT Queens waliokuwa wanaanze Novemba 8 dhidi ya Bunda Queens mechi hiyo imewekwa kiporo hadi Desemba 8 kutokana na muingiliano wa ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayonza Misri wakiwa ni washiriki.

Kwa mujibu wa ratiba mpya ni kwamba mechi za Novemba 14 zitachezwa nne zote zikipigwa kuanzia saa 10 jioni, Geita Queens ikiikaribisha Ceasiaa Queens Uwanja wa Nyamkumbu, Simba Queens dhidi ya Bilo Queens (KMC), Alliance Girls na Fountain Gate (Nyamagana), Ruangwa Queens vs Yanga Princess (Majaliwa).

Pambano la kwanza la watani wa jadi, Simba Queens dhidi ya Yanga Princess limepangwa kupigwa Desemba 28, ikiwa ni siku tatu kabla ya kuagwa kwa mwaka 2025 na kukaribishwa 2026.

Katika msimu uliopita mechi ya mwisho baina yao iliisha kwa Yanga kushinda bao 1-0 lililofungwa na Jeannine Mukandayisenga siku ya Machi 19.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mkuu wa Alliance Girls, Sultan Juma alisema wanaendelea na maandalizi jijini Mwanza na asilimia kubwa kila kitu kimekamilika wakisubiri kumalizia dakika 90 uwanjani.

“Tumekuwa na pre season nzuri msimu huu nimekuwa na timu muda mrefu, msimu uliopita hatukuanza vizuri kwa sababu tulikosa muda wa kujiandaa huu tumefanya marekebisho kwenye maeneo tofauti hasa la golikipa ambalo lilionekana kuwa na udhaifu,” alisema Sultan.

Kocha wa Mashujaa Queens, Ally Ally alisema wana muda wa kutosha kujiandaa na ligi na atatumia kipindi hiki kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika ngao ya jamii na mechi za kirafiki.

“Tuna muda wa kutosha kujiandaa na ligi sisi mechi yetu Desemba 8 hivyo muda huo tutautumia vizuri kurekebisha makosa na kuongeza umakini wa wachezaji wetu, kila mmoja ana ari kubwa na naamini tutaanza msimu tukiwa kwenye kiwango bora zaidi.”