Dar es Salaam. Upatikanaji wa huduma kwa wananchi katika ofisi za serikali za mitaa za Tarafa ya Kibamba na Magomeni umekwama, baada ya ofisi hizo kuchomwa moto wakati wa vurugu na maandamano ya Oktoba 29, 2025.
Tukio hilo pia, limekwamisha shughuli za urasimishaji wa ardhi na hatimaye ugawaji wa hatimiliki kwa wananchi, kutokana na kuungua kwa nyaraka za urasimishaji zilizokuwemo katika ofisi hizo za serikali za mitaa.
Vurugu na maandamano hayo, zilifanyika Oktoba 29, 2025 zikihusisha watu mbalimbali waliokuwa wakishinikiza kutofanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kutokana na maandamano hayo, vituo vya polisi, ofisi za serikali za mitaa, vituo vya mafuta, maduka na magari binafsi ya watu yameunguzwa moto na waandamanaji.
Hayo yameelezwa leo, Alhamisi Novemba 6, 2025 na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kibamba, Sembuli Mgendi alipozungumza na wanahabari, wakati wa ziara ya makatibu tarafa wa maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam, iliyolenga kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu hizo za siku ya uchaguzi.
Amesema imekuwa vigumu kutoa huduma kwa wananchi, kwani kila nyaraka na vifaa muhimu vya kufanyia kazi vimeungua pamoja na ofisi.
Miongoni mwa huduma zilizokwama, amesema ni utoaji wa barua za utambulisho, ugongaji mihuri na upatikanaji wa nyaraka za urasimishaji ardhi uliokwamisha upatikanaji wa hati mmiliki kwa wananchi.
“Ukiacha vilivyokwama, pia hatuna ofisi ya kutolea huduma, vitendea kazi vimeungua, kwa ujumla hatuna namna ya kutoa huduma,” amesema.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Stop Over, Alex Msuka amesema wafanyabiashara wengi wamepata hasara kwani mbali na vituo vya mafuta katika moja ya maduka ya kuuza pikipiki wamechukua zaidi ya pikipiki 30, wamevunja kituo cha kuoka mikate na wamechukua majokofu.
“Ni vema wananchi kama wana changamoto waje tuonane na viongozi wa serikali za mitaa, lakini masuala ya kuharibu mali za wananchi si sawa,” ameeleza.
Exaud Malya ni mmoja wa wananchi katika mtaa huo, amesema kila huduma inayohitaji serikali ya mtaa imesimama na hata viongozi ndio kwanza wameanza kuwaona jana.
“Hawakuwepo kwa sababu ofisi imeungua watakaa wapi. Tumeanza kuwaona leo (jana) na hawana muhuri, barua wala nyaraka zozote. Vyote vimeungua, imetukwamisha,” amesema.
Justine Mrema, ni mmiliki wa gari lililochomwa moto katika eneo la Mbezi, amesema aliliegesha gari hilo karibu na kituo cha upigaji kura na siku hiyo ya tukio hakuondoka nalo nyumbani kwa sababu lilikuwa na pancha, hivyo alitarajia kesho yake angeenda kulirekebisha.
Amesema cha kushangaza siku iliyofuata alikuta gari limechomwa moto na waandamanaji pamoja na kusambaratishwa kwa kituo cha upigaji kura.
Ameeleza hatua hiyo imemtia hasara ya Sh17 milioni ambayo ni thamani ya gari yake, lakini atashindwa kufanya baadhi ya safari kwa kuwa chombo hicho cha usafiri ndicho alichokuwa akikitumia kwa kazi zake.
Meneja wa Kituo cha Mafuta cha Rupeez, Merkezedeki Maganga amesema katika kituo hicho kulikuwa na magari 36 yaliyoegeshwa, sita yamechukuliwa na waandamanaji na mengine yamechomwa moto.
“Ni hasara kwetu, lakini hasara kwa wateja wetu na watu walioegesha magari yao hapa. Hakuna namna tunayoweza kufanya kwa sababu ndio yameshachomwa moto,” amesema.
Kwa upande wake Katibu Tarafa ya Kibamba, Beatrice Mbawala amesema bado Serikali haijafanya tathmini ya jumla kujua thamani halisi ya fedha kwa miundombinu iliyoathiriwa.
Amesema hadi sasa bado viongozi hao hawana maeneo ya kufanyia kazi na utaratibu unaendelea kuhakikisha inapatikana eneo la kutoa huduma kwa wananchi.
Mbali na ofisi hizo, amesema vituo vidogo vinne vya polisi vimechomwa moto kikiwamo kituo kipya cha Tegeta A kilichojengwa kwa nguvu za wananchi.
Katika eneo hilo, amesema darasa la Shule ya Msingi Mbezi na vituo vyote vya mabasi yaendayo haraka vimechomwa moto, akisisitiza kilichofanyika ni uharibifu ulioliza wananchi na sio maandamano ya kudai haki kama inavyoelezwa.
Katibu Tarafa wa Magomeni, Grace Kiando amesema kutokana na hali hiyo, wananchi wamekuwa wakihangaika kupata huduma kwa sababu ofisi nyingi za mitaa zilichomwa moto sambamba na vituo vya polisi.