Aliyeshtakiwa kwa mauaji ya bodaboda alivyonusurika adhabu ya kunyongwa

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Moshi imemuachia huru Denis Shirima, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kumuua dereva bodaboda, Juma Mwesi, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kosa na kuacha mashaka yaliyompa faidha mshitakiwa.

Hukumu hiyo ambayo imepatikana katika mtandao wa Mahakama, imetolewa Novemba 5, 2025 na Jaji Safina Simfukwe, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya mauaji yaliyotokea Desemba 13, 2021 eneo la Rau Manyele wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.

Mbele ya Mahakama hiyo, Shirima alishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu ambapo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi tisa na vielelezo sita.

Jaji Simfukwe amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imejiridhisha kuwa ushahidi wa kimazingira umeshindwa kumhusisha mshtakiwa na mauaji hayo, hivyo kumuachia mshtakiwa huru baada ya kumkuta hana hatia.

Shahidi wa tatu, Athumani Nasoro ambaye pia ni dereva bodaboda, alidai walipofika eneo eneo la tukio walimkuta Juma ameumia kichwani ambapo waliripoti Kituo Kikuu cha Polisi Moshi, kisha wakampeleka Hospitali ya Mawenzi.

Alidai mahakamani hapo kuwa Desemba 14, 2021, Juma alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambapo alifariki akipatiwa matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Awali, shahidi huyo alidai kupigiwa simu na msamaria mwema aliyemjulisha kuwa rafiki yake (Juma) alivamiwa na kuwa alielezwa kuwa rafiki yake alikuwa amebeba abiria wawili hadi eneo la Rau Manyele.

Alidai kuwa walipofika eneo hilo, mmoja wa abiria hao alijifanya kumlipa, kisha abiria mwingine alimpiga marehemu na kitu kizito kichwani kisha walichukua pikipiki, simu ya mkononi na pochi yake.

Uchunguzi wa mwili wa marehemu ulifanywa na shahidi wa kwanza, Dk Alex Mremi, ambaye alihitimisha kuwa chanzo cha kifo cha marehemu ni jeraha kubwa la kichwa.

Shahidi wa pili ambaye ni mjomba wa marehemu, Ismail Rajab alidai kushuhudia Juma akivuja damu mdomoni na puani katika hospitali ya KCMC na kuwa alikuwa miongoni mwa ndugu waliomtambua marehemu kabla ya uchunguzi wa mwili.

Shahidi wa nne, G.3869 Koplo Edward alidai pamoja na mambo mengine alipokea vielelezo mbalimbali kutoka kwa Koplo Ibagi ambaye alikuwa amestaafu, ikiwa ni pamoja na simu aina ya Samsung Galaxy J7 rangi nyeusi.

Shahidi wa tano, Athanasia Mushi alidai kuwa mshtakiwa alimuuzia simu hiyo (Samsung Galaxy J7) ambapo baada ya wiki mbili alipigiwa simu na namba asiyoijua ambapo aliogopa kukutana na mtu huyo hadi mama yake na kaka yake walipokamatwa.

Alidai baada ya ndugu zake kukamatwa alilazimika kwenda Kituo cha Polisi Mkuu na kueleza kuwa alinunua simu hiyo kwa mshtakiwa ambaye alifuatiliwa na kukamatwa na shahidi wa nane, Koplo Hans.

Shahidi wa saba, Ally Hassan ambaye ni kaka wa marehemu alidai mahakamani kuwa yeye ndiye aliyemnunulia mdogo wake (Juma) simu hiyo na kuwa baada ya kuinunua alirekodi IMEI namba ya simu hiyo.

Alidai kupitia IMEI hiyo mtaalamu wa masuala ya mtandao alifanikiwa kufuatilia simu hiyo ambayo ilipatikana eneo la Tarakea wilayani Rombo.

Shahidi wa nane ambaye ni mtaalamu wa makosa ya mtandao alisimulia mahakama jinsi alivyofanikiwa kufuatilia simu ya mkononi ya marehemu na kuikamata kwa shahidi wa tano wilayani Rombo.

Alidai mshtakiwa alikamatwa Februari 19, 2022 huko Tarakea na kuwa baada ya kuhojiwa, alikiri kuuza simu hiyo ya mkononi kwa shahidi wa tano ila hakueleza alikoipata simu hiyo.

Aidha, akihojiwa na wakili wa utetezi, shahidi huyo alieleza pamoja na mambo mengine hakuandika katika maelezo yake kwamba Denis aliuza simu kwa Atanasia.

Katika utetezi wake mahakamani hapo, mshtakiwa huyo alidai kosa hilo lilitengenezwa dhidi yake baada ya kushindwa kutoa rushwa kwa askari polisi mmoja wa Tarakea, kama walivyokubaliana.

Pande zote mbili ziliwasilisha mawasilisho yao ya mwisho kwa njia ya maandishi ambapo upande wa mashtaka ulidai shahidi wa tano alinunua simu kwa mshtakiwa Januari Mosi, 2022 kwa Sh170,000.

Kwa upande wa utetezi, uliwasilisha notisi ya utetezi wa kutokuwepo eneo la tukio (Alibi) na kuwa dereva bodaboda (Amani Watson) ambaye anadaiwa kumtambua mshtakiwa akiwa amebebwa na Juma hakuitwa mahakamani kama shahidi.

Wakili wa utetezi alidai kuwa mahakama ilikosea kutoa uamuzi kwamba mshtakiwa alikuwa na kesi ya kujibu, licha ya upande wa mashtaka kushindwa kuanzisha kesi ya awali kama inavyotakiwa.

Aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitoa utetezi thabiti kwamba siku ya tukio alikuwa eneo la Majengo kwa Mtei na aliondoka kwenda kutengeneza gari lake hadi saa 8 mchana aliporudi.

Aliongeza kuwa mshtakiwa huyo anahusishwa na kesi hiyo ya uongo kwa sababu alikataa kutoa rushwa kwa mmoja wa askari wa kuzuia magendo kutoka Kituo cha Polisi Tarakea.

Wakili huyo aliukosoa upande wa mashtaka kwa kushindwa kumchukulia shahidi wa tano kama mshukiwa wa tukio hilo.

Jaji Simfukwe amesema katika kesi za jinai upande wa mashtaka una wajibu wa kuthibitisha kosa pasipo kuacha shaka.

Amesema mahakama hiyo ina wajibu wa kuamua iwapo ushahidi wa kimazingira katika kesi hii unatosha kuthibitisha kuwa marehemu aliuawa na mshtakiwa pamoja na iwapo mshtakiwa alimuua marehemu kwa nia mbaya.

Jaji amesema kwa kuanzia suala la pili, ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ni kuwa marehemu alipigwa na kitu kizito kichwani.

“Kichwa ni miongoni mwa sehemu za mwili zilizo hatarini. Kwa hiyo, haijalishi ni nani aliyemuua marehemu, mauaji hayo yalifanywa kwa nia mbaya (uovu uliotangulia),” amesema Jaji.

Kuhusu suala la ushahidi wa mazingira, Jaji amesema ili ushahidi wa kimazingira utegemewe lazima uzingatie mambo manne ikiwemo mazingira hayo kuwa lazima yathibitishwe kwa uthabiti bila shaka yoyote na kuwa mshtakiwa ndiye alitenda kosa hilo.

Jaji amesema kwa kukosekana ushahidi ikiwemo wa Amani ambaye alidaiwa kumuona mshtakiwa akiwa amebebewa kwenye pikipiki ya Juma (marehemu kwa sasa) na kuwa ushahidi huo ungeondoa mashaka yote kwa upande wa mashtaka.

Jaji amesema ushahidi wa kimazingira katika kesi hiyo unaweza kutoa tafsiri zaidi ya moja na kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi ya mauaji dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka kama inavyotakiwa na sheria.

Jaji alihitimisha kuwa Mahakama hiyo inamuona Denis hana hatia ya kosa la mauaji, hivyo kumuachia huru.