TIMU ya JKU, imesitisha mkataba na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Seif Bausi Nassor kwa makubaliano ya pande mbili, ikiwa ni baada ya kuiongoza katika mechi saba za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu huu 2025-2026.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Novemba 7, 2025 na Katibu Mkuu wa JKU, Khatib Shadhil Khatibu, imesema: “Jeshi la Kujenga Uchumi Sports Club (JKU) limesitisha mkataba na kocha mkuu wa timu ya mpira wa miguu, Seif Bausi Nassor (Kocha Bausi).
“Makubaliano ya kusitisha yamefanyika kwa pande zote mbili kwa upande wa JKU SC (mwajiri) na Kocha Bausi (mwajiriwa).”
Pia, taarifa imeeleza kuwa timu hiyo imemuondoa kocha Msaidizi, Msellem Sultan Hemed katika kikosi cha wakubwa na kumpa majukumu ya kuendelea kulelea vipaji katika Akademi ya JKU.
Wakati hayo yakitokea, JKU imeanza mchakato wa kutafuta makocha watakaojaza nafasi hizo haraka iwezekanavyo.
Kabla ya kuondoshwa, Kocha Bausi aliiongoza JKU inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, msimu huu kucheza mechi saba, kati ya hizo imeshinda moja, sare nne na kupoteza mbili na kuvuna alama saba ikiwa imefunga mabao matano.