Dk Tulia akitoa kwenye kinyang’anyiro akiacha maswali

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ametangaza kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kugombea tena nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nafasi ambayo alikuwa akiitetea.

Hata hivyo, juhudi za kumpata Dk Tulia Ackson kwa njia ya simu hazikufanikiwa, kwani hakupokea simu yake licha ya kupigiwa mara kadhaa.

Lakini, msaidizi wake binafsi, Michael Msombe amethibitisha kuwa barua ya kujiondoa kwake ni halali na kwamba Spika huyo kweli amejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Dk Tulia alikuwa akigombea nafasi hiyo akichuana na aliyekuwa Naibu Spika wake, Mussa Zungu, pamoja na Mbunge wa zamani wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele.

Mbunge huyo wa Uyole, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge Februari Mosi, 2022, kuchukua nafasi ya Job Ndugai (marehemu), aliyeng’atuka kufuatia kauli zake ambazo zilielezwa kupingana na mamlaka ya juu ya nchi.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa Spika, Dk Tulia aliwahi kuwa Naibu Spika wa Bunge la 11, nafasi aliyoshika kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka 2015 baada ya kuteuliwa kuwa Mbunge na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk John Magufuli.

Dk Tulia alirejea tena katika nafasi hiyo kwenye Bunge la 12, ambapo alihudumu kwa mwaka mmoja na miezi miwili kabla ya kupandishwa kuwa Spika.

Nyota ya mwanasheria huyo iling’ara zaidi Oktoba 23, 2023, alipochaguliwa kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), nafasi ya kihistoria ambayo anaendelea kuishikilia hadi sasa.

Kwa mujibu wa katiba ya IPU, nafasi ya Rais wa umoja huo hutwaliwa na maspika wa mabunge wanachama, hivyo kwa kujiondoa kwake katika nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia anatarajiwa kupoteza sifa ya kuendelea kuongoza chombo hicho muhimu cha kimataifa.

Hata hivyo, uamuzi wake wa kujitoa katika kinyang’anyiro cha Spika umeibua maswali kadhaa, huku vyanzo mbalimbali vikihusisha hatua hiyo na fununu za uwezekano wa uteuzi katika Baraza la Mawaziri, ingawa bado haijafahamika wazi ni nafasi gani anaweza kuteuliwa kushika endapo tetesi hizo zitathibitishwa.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Hamduni Marcel amesema kuwa ni jambo la kushangaza kujitoa kwake kwani alikuwa mtarajiwa mkubwa katika kiti hicho.

Marcel amesema kutoonekana kwake kwenye jambo hilo hakueleweki nini inashangaza ila inaweza ikawa na sababu mbili, moja anaweza akaona kama hajaheshimika na chama kwa kuwa ameongezewa watu wengine wawili wa kushindana nao, hivyo akaona haina haja ya kushindana na wenzake

Jambo la pili inaweza kuwa tofauti pengine inaweza ikawa ameahidiwa nafasi kubwa zaidi badala ya kuendelea kuvutana wakamwambia akae pembeni sababu kuna nafasi maalumu wamemwandalia.