Gamondi awapa masharti nyota watatu Pamba Jiji

WAKATI Singida Black Stars ikijiandaa kuikabili Pamba Jiji, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amewaruhusu wachezaji watatu walio kwa mkopo kucheza ili kutaza viwango vyao.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara itachezwa kesho Jumamosi Novemba 8, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni.

Singida Black Stars ina wachezaji watatu imewapeleka kwa mkopo katika Klabu ya Pamba Jiji, ambao ni winga, Yonta Camara aliyepo hapo tangu dirisha dogo msimu uliopita, na viungo Kelvin Nashon na Najimu Mussa waliojiunga na Pamba dirisha kubwa lililofungwa Septemba 2025.

Akizungumza leo Ijumaa Novemba 7, 2025 jijini Mwanza, Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amesema Gamondi ametoa ruhusa hiyo baada ya uongozi wa Pamba Jiji kutuma maombi ya kuwatumia nyota hao katika mechi ya kesho.

Amesema wameamua kutoa ruhusa kwa Pamba kuwatumia wachezaji hao ili Kocha Gamondi atazame viwango vyao hususan katika kipindi hiki cha kuelekea dirisha dogo litakalofunguliwa Desemba 15, 2025.

‎”Ombi limekuja tukamshirikisha Gamondi na yeye akatoa ruhusa wacheze ili aangalie viwango vyao kwa sababu Januari inakaribia na kocha awe na uwanja mpana wa kufanya uamuzi,” amesema Massanza.

Ameongeza kuwa; “Wachezaji hawa tumewaruhusu na kesho Pamba wana uhuru wa kuwatumia, nasi tunaamini kesho wataonyesha uwezo wao na kuna kitu watamuonyesha kocha Miguel Gamondi.”

Kwa upande wake, Gamondi akizungumzia mechi hiyo, amesema kikosi chake kiko tayari na wachezaji wana njaa ya kucheza na kufanya vizuri ili kuwa na mwendelezo wa matokeo mazuri kwa timu yao.

“‎Hakuna mechi rahisi kwangu lakini kiuhalisia dhidi ya Pamba utakuwa mchezo mgumu, tutatumia kile tulichojifunza mazoezini kufanyia kazi uwanjani, hivyo tutapambana kadri tuwezavyo kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Gamondi.

‎kuhusu ubora na mwendelezo wa kikosi chake, amesema; “Siku zote nawaambia wachezaji wangu kwamba Kila mazoezi tunayofanya ni nafasi kwao ya kuimarika na kuboresha kazi yao. ‎Nami nashukuru nina kundi la wachezaji wanaojituma na kutamani kufanya vizuri kila siku, hiyo ndiyo siri yetu.”

‎Nahodha wa timu hiyo, ‎Kennedy Juma, amesema mwenendo mzuri waliouanza kwenye ligi na michezo ya kimataifa inawapa motisha ya kutamani kufanya vizuri katika kila mechi iliyo mbele yao.

“Mchezo wetu wa kesho utakuwa mgumu, Kila timu inataka pointi tatu lakini maamuzi yote yako ndani ya dakika 90 ndizo zitaamua. Kwenye soka presha ni kitu cha kawaida, muhimu ni kuishinda hiyo presha, hivyo tumeshajiwekea mawazo ya kushinda na tunaamini tukipambana basi tutafanya vizuri,” amesema Juma.