Mbeya. Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya limetangaza nia maalumu ya kuwaombea watu waliopoteza maisha au kujeruhiwa wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Siku hiyo, shughuli ya upigaji kura kuwachagua Rais, wabunge na madiwani, ililoambatana na maandamano na vurugu katika baadhi ya maeneo nchini zilizopelekea watu ambao idadi yao haijafahamika kuuawa, kujeruhiwa na wengine hawajulikani walipo.
Hata waliosalimika walilazimika kujifungia ndani kwa takribani siku sita huku shughuli za kijamii zikisimama.
Katika mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 4, 2025 kupitia kwa katibu wa kanisa hilo, Padri Henry Mwalyenga, parokia zote za jimbo kuu zinaagizwa kuwa na nia maalumu ya kuwaombea marehemu na majeruhi.
Maombi hayo yanatarajia kufanyika Novemba 9, 2025 ambayo ni Dominika ya 32 ya mwaka C, ambapo siku hiyo alasiri, kutakuwa na misa maalumu ya kijimbo kwa ajili ya kuwaombea waathirika hao katika Kanisa la Hija Mwanjelwa jijini Mbeya.
“Tunawaomba maparoko wote na mapadri mnaofanya utume ndani ya Dekania ya Mbeya, Mbalizi na Mporoto muwahamasishe waamini pamoja na nyinyi kufika katika misa itakayohudhuriwa na Askofu Mkuu na Askofu Msaidizi,” imesema taarifa hiyo na kuongeza:
“Wote tunaombwa kushiriki kwa wingi katika misa hiyo, tukimkabidhi Mwenyezi Mungu roho za marehemu na kuwaombea uponyaji wale wote waliojeruhiwa ili Taifa letu liendelee kuwa na amani, umoja na upendo.”
Pia, taarifa hiyo imeongeza kuwa waamini wenye mapenzi mema wanaotaka kutoa misaada kwa ajili ya ndugu waliopata madhara, wanahimizwa kuiwasilisha katika parokia zao ili ziratibiwe na ofisi za kichungaji za parokia.
Akizungumza kwa njia ya simu, Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Gervas Nyaisonga amethibitisha kuwepo maombi hayo, akieleza lengo ni kuliombea Taifa na wale waliopata madhila wakati na baada ya uchaguzi.
Amesema parokia zote zitafanya maombi hayo, lakini kwa walio karibu tukio hilo litafanyika Mwanjelwa, akiwaomba wananchi wenye nia na uhitaji wa kufanya ibada hiyo kushiriki kwa kuwa halina masuala ya kisiasa.
“Ni kweli barua ni rasmi, tumetangaziana, lengo ni kuliombea Taifa na wale waliopata madhila, kila parokia litafanya ibada hiyo na wale walio karibu na Mbeya tutafanyia kanisa la Mwanjelwa, wananchi wenye kuhitaji kushiriki wanakaribishwa,” amesema askofu huyo.
Kanisa Katoliki duniani, Novemba ya kila mwaka huwa maalumu kwa ajili ya kuombea marehemu.