Kocha JKT Tanzania kiroho safi Taifa Stars

KOCHA wa JKT Tanzania, Ahmad Ally aliyeteuliwa kuwa msaidizi wa Miguel Gamondi wa Singida Black Stars kuinoa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ amesema ni fursa na hatua nyingine kwake kuendelea kujifunza vitu tofauti.

Kocha Gamondi na Ally wamepewa jukumu hilo la kuinoa Stars katika michuano ya Afcon itakayoanza Desemba kukabiliana na Uganda, Nigeria na Tunisia, huku aliyekuwa kocha Mkuu Hemed Moroco akipigwa chini na wataanza kibarua Novemba 14 dhidi ya Kuwait watakaovaana nao mechi ya kirafiki itakayiopigwa jijini Cairo, Misri.

Akizungumzia uteuzi huo, kocha Ally amesema ni fursa kubwa kama kijana wa Kitanzania kulitumikia taifa lake na inampa nguvu ya kuendelea kujifunza vitu vingi ili kufanya makubwa katika mpira wa miguu ndani na nje. 

“Falsafa ya maisha yangu kujifunza haijalishi mtu nimemzidi ama kanizidi, lazima kutakuwa na jambo ambalo litazaliwa jipya kwangu, hivyo kwenda kukutana na Gamondi lazima kutakuwa na vitu vya ziada,” amesema Ally aliyewahi kuiongoza timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars katika michuano ya Kombe la Mapinduzi msimu uliopita visiwani Zanzibar aliyeongeza:

“Nimefarijika kupata fursa ya kulitumikia taifa langu kama kijana wa Kitanzania, nimeitwa nikiwa na JKT Tanzania hivyo hii ni hatua yetu wote nikimanisha na timu ninayoifundisha.”

Mbali na hilo alizungumzia mechi dhidi ya Simba inayochezwa leo Jumamosi kuanza saa 1:00 usiku amesema: “Haitakuwa mechi rahisi, Simba ni kati ya timu bora Afrika, lakini tumejipanga kuhakikisha tunapambania pointi tatu.”