Mabadiliko ya tabianchi, shughuli za kibinadamu vyatishia uhai wa Ziwa Jipe

Mwanga. Ni safari ya zaidi ya kilomita 40.96 kutoka Kifaru wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro kwenda Butu hadi Ziwa Jipe, iliyolenga kujionea hali halisi ya mazingira ya ziwa hilo, shughuli zinazoendelea na hatima ya maisha ya wananchi wanaolitegemea.

Nilipofika eneo la mwalo la Mkisha, nilitarajia kuona mandhari nzuri ya ziwa, nikipepesa macho juu ya maji tulivu, lakini kilichoonekana ni kama msitu mnene uliotapakaa.

Sikuweza kuona maji ila magugumaji yaliyoficha kabisa taswira ya ziwa.

“Ongezeko la joto na mvua zisizo na utaratibu huongeza virutubisho kwenye maji, hivyo kuchochea ukuaji wake,” ananieleza Paul Kyando, mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi.


Anasema: “Magugu haya hupunguza oksijeni majini, huharibu ikolojia na huzalisha gesi chafu kama vile methane, hivyo kuchangia zaidi ongezeko la joto duniani.”

Niliposogea mbele, nilikutana na kundi la wanawake wakisafisha na kuchoma samaki waliotoka kuvuliwa ziwani. Ilinishangaza kuona shughuli hiyo ikifanyika karibu kabisa na njia ya kuingia ziwani.

Nilipohoji kwa nini wapo hapo, miongoni mwao, Justina Macha akasema: “Tumezoea kufanya hivi kwa muda mrefu, kwani tunapata urahisi wa kupata maji ya kusafisha samaki.”

Kuna nyakati maji machafu yaliyotumika kusafisha samaki hutiririka moja kwa moja na kuingia ziwani.


Nikiendelea kutalii ziwani, nilikutana na vinyesi vya mifugo vilivyokauka na vingine vipya kando mwa ziwa ikiwa ni ishara kwamba mifugo hufikishwa hapa kwa ajili ya kunywa maji na pia malisho.

Kinachofanyika ni kinyime cha kifungu cha 57 sehemu ya kwanza cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004 kinachosema: “Ndani ya mita 60 kutoka chanzo cha maji hakutafanyika shughuli yoyote ya binadamu ya kudumu au ambayo kwa asili yake inaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira.”

Nilipotembea kuelekea eneo ambalo boti zimeegeshwa, moja iliwasili kutoka ziwani. Ndani kulikuwa na samaki aina ya kambale wakubwa kiasi na perege waliokuwa wadogo mithili ya dagaa.

Nilipozungumza na mmoja wa wavuvi, Alexander Sanka, anasema hali ya uvuvi imezorota.


“Samaki hawapatikani,” ananieleza huku akionekana mchovu baada ya kuwa majini kwa muda mrefu.

“Tunachopata ndicho tunalazimika kuvua, hakuna namna,” anasema akijibu swali langu kuhusu uvuvi wa perege ambao wanaonekana kuwa wachanga.

Tunapoendelea kuzungumza tukiwa kando mwa boti yake, ananieleza kwa zaidi ya miaka 15 anafanya shughuli ya uvuvi katika Ziwa Jipe.

Anasema zamani uvuvi ulikuwa wenye tija, aliweza kurudi nyumbani na hadi Sh100, 000 kwa siku. Lakini sasa hali ni tofauti.

“Siku hizi unaweza kurudi na Sh30, 000 tu, wakati mwingine hata samaki wa kula tu hakuna. Uvuvi umekuwa kama ‘gombania goli’. Magugumaji yamezidi, samaki hawapatikani kama zamani,” anasema Sanka.

Kuona ni kusadiki. Nilimuomba kwa kutumia boti lake tuingie ziwani nikajionee hali halisi.

Tulipoanza safari, tulipita katikati ya magugumaji. Ni kama vile unapita kwenye msitu wa majini.

Katika eneo lenye uwazi kidogo, ilionekana kuwa limechomwa moto.

Akijibu swali langu kuhusu hali hiyo, Sanka anasema: “Wavuvi hulazimika kuchoma moto sehemu yenye magugumaji ili kupata njia ya kupita. Tungeacha, tusingefika katikati ya ziwa. Hatuna namna nyingine.”

Ingawa moto huo unaonekana kuwasaidia wavuvi, lakini unaacha maswali kuhusu usalama wa viumbe hai kama kobe, viboko, ndege na viumbe wengine wa majini wanaoishi humo.

Hakuna utaratibu wa kudhibiti moto huo wala anayefuatilia athari zake.

Licha ya mwalo huo, mingine ya Mbembe na Makuyuni hali haikutofautiana sana, isipokuwa Makuyuni ambako shughuli za uvuvi zimesimama kabisa baada ya njia za kuingia ziwani kufungwa na magugumaji.


Katika mazingira ya dunia inayoendelea kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, madhara yake yanaonekana kuchukua nafasi kubwa katika kubadili uchumi, mazingira, viumbe hai na hata maisha ya binadamu.

Ziwa Jipe ni miongoni mwa maeneo yanayoshuhudia athari hizo.

Kijiografia, Ziwa Jipe linapatikana mpakani mwa Kenya na Tanzania. Upande wa Kenya liko kusini mwa Kijiji cha Nghonji na upande wa Tanzania liko Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Ziwa lina ukubwa wa kilomita za mraba 46, ambazo 30 ziko upande wa Kenya na 16 zipo Tanzania. Ziwa Jipe limewahi kujulikana kwa wingi wa samaki, ndege wa majini, viboko, mamba, mimea ya ardhioevu na vinamasi vinavyozunguka ukanda wa ziwa.

Pia ni chanzo cha maji kwa shughuli mbalimbali za wakazi wa vijiji vinavyolizunguka, ikiwamo matumizi ya nyumbani.

Maji kutoka Ziwa Jipe hulisha Bwawa la Nyumba ya Mungu, ambalo hutumika kuzalisha umeme na kuendeleza uvuvi wa kambale na perege.


Kwa mujibu wa Kifungu cha 56 cha Sheria ya Mazingira, Waziri anapaswa kutangaza eneo lolote kuwa ardhioevu na mamlaka husika kuisimamia. Vilevile, Kifungu cha 57 cha sheria hiyo kinakataza shughuli yoyote ya binadamu ndani ya mita 60 kutoka kingo za mito, mabwawa au maziwa.

Hata hivyo, ukweli unaoonekana Ziwa Jipe ni tofauti na kilichoandikwa kwenye sheria.

Mtendaji wa Kijiji cha Jipe, Uzia Mndeme, anakiri wazi wananchi wamekuwa wakikiuka sheria, wapo wanaoendelea kupeleka mifugo kunywesha ziwani na wakati mwingine kuwalisha pembezoni kwenye maeneo yenye majani. Pia, wavuvi wanaingia ziwani licha ya makatazo yaliyowekwa.

Vumilia Msemo, mkazi wa Jipe, anasema familia yake imekuwa ikitumia maji ya ziwa hilo kwa muda mrefu, licha ya kuwa na asili ya magadi.

“Maji ya bomba au visima yanapopata changamoto, tunalazimika kutumia maji ya ziwa ila tukifika tunakuta vinyesi vya wanyama. Tunalazimika kuingia na boti katikati ili kupata maji masafi,” anaeleza.

Matamko, kuliko utekelezaji

Machi 26, 2017, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba, aliahidi kutoa tangazo la Serikali kulitambua eneo hilo kuwa nyeti kimazingira na kuweka masharti ya matumizi.

Septemba 21, 2021, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Hassan Chande, aliutaka uongozi wa Wilaya ya Mwanga kudhibiti kilimo kisicho endelevu kando mwa ziwa, kinachosababisha mmomonyoko wa udongo na kuathiri mazingira ya ziwa. Licha ya matamko hayo, hali halisi haijabadilika.

Ofisa Mazingira Wilaya ya Mwanga, Elineema Paranjo anaeleza kuwa athari za shughuli za kibinadamu zinaendelea kuhatarisha maisha ya viumbe majini, mifugo na binadamu.

“Kilimo kinapofanyika milimani, mvua inaponyesha, maji hubeba kemikali za mbolea na tope kuingia ziwani, hivyo kuchafua maji na kuongeza tope ndani ya ziwa,” anasema.

Ofisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Haruna Kalekwa, anasema Ziwa Jipe lina mialo mitatu ambayo ni Mkisha (Kata ya Butu), Mbembe na Makuyuni. Hata hivyo, mwalo wa Makuyuni hautumiki kutokana na magugumaji.

Anatoa tathimini ya uvuvi kwa miaka mitano akisema: “Uvuvi unaofanyika Ziwa Jipe sasa ni asilimia 20 tofauti na miaka iliyopita. Sababu kubwa ni magugumaji.”

Halmashauri imesajili wavuvi 36 na vyombo 23 kwa uvuvi wa Jipe, wakati nguvu kubwa ya uvuvi imehamia Bwawa la Nyumba ya Mungu, ambako uvuvi unafanyika kwa asilimia 80.

Haruna anasema halmashauri imekuwa ikiandika maombi kwa Wizara ya Mazingira kuhusu hali ya magugumaji, kwani kiwango kilichofikiwa kimevuka uwezo wake wa kuyashughulikia.

“Inahitaji gharama kubwa kuondoa magugumaji ikiwamo kemikali au njia zitakazotumika. Tunahitaji msaada wa wizara,” anasema.

Rashid Mbwana, Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa Taka, anasema wanatoa elimu ya kuzuia uchafuzi ndani ya mita 60 kutoka ziwani, lakini ukiukaji unaendelea.

Anasema wachafuzi hutozwa faini za kijiji na ukizidi huchukua hatua kwa sheria za halmashauri.

Hata hivyo, Elineema anaeleza wanazingatia sheria za mazingira na kutoa elimu, lakini changamoto inaendelea.

Kwa upande wa Kenya, hali inaonekana kutokuwa mbaya kama Tanzania. Swali likiwa, ikiwa sehemu ya ziwa ni mpaka kati ya mataifa mawili, je, Tanzania inasubiri mpaka ziwa litoweke?

Athari hazipo kwa mazingira pekee. Kuna hatari za usalama, uvamizi wa wanyama hatari na uwezekano wa eneo hilo kutumika kama maficho ya wahalifu.

Ziwa Jipe si tu chanzo cha maji na kipato ni ngao ya ikolojia. Kusuasua kwa hatua za kukabiliana na magugumaji leo, kunamaanisha kesho huenda kukawa hakuna cha kulinda.

Imeandaliwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Gates Foundation