Matunda ni zawadi muhimu kutoka ardhini; rangi zake za kuvutia, ladha tamu na uchachu wake vimekuwa kivutio kikubwa kwa binadamu tangu enzi za mababu.
Si chakula cha starehe pekee, bali pia ni ngome ya afya inayolinda miili yetu dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Katika dunia inayoshuhudia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na saratani, wataalamu wa lishe wanasisitiza umuhimu wa kuingiza matunda kwenye kila mlo.
Na si matunda peke hata maganda ya baadhi ya matunda, yamegundulika kuwa na hazina kubwa ya virutubishi vinavyofaa mwilini.
Matunda ni kundi mojawapo la vyakula sita vinavyounda mlo kamili. Yamejaa aina tofauti tofauti hapa nchini kama vile papai, pera, pesheni, nanasi, peasi, chungwa, chenza, tikiti, parachichi, ndizi mbivu, stafeli, topetope, fenesi, pamoja na matunda ya porini kama ukwaju, zambarau, ubuyu, furu na mabungo.
Matunda haya yanabeba vitamini na madini muhimu kama Vitamin A, Vitamin C, potassium, folate na sodium.
Kwa mujibu wa Ofisa lishe na mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Elizabeth Lyimo, matunda si tu yanakuza kinga ya mwili, bali pia yana nyuzinyuzi au makapimlo zinazosaidia kushibisha, kupunguza ulaji kupita kiasi na hivyo kuzuia unene.
“Kwa wastani, mtu anatakiwa kula angalau gramu 400 za matunda na mbogamboga kwa siku. Hata hivyo, kazi nyingi za kitafiti zinaonyesha Watanzania wengi hawatimizi kiwango hiki,” anasema.
Tahadhari ulaji wa maganda
Pamoja na faida lukuki, swali linaibuka: Je, ni salama kula maganda ya matunda?
Lyimo anabainisha kuwa maganda yana faida kubwa kiafya, ila si kila ganda linafaa kuliwa. Hii ni kwa sababu matunda mengi hupuliziwa dawa za kuua wadudu shambani.
“Kama mtu analima matunda yake mwenyewe bila kutumia dawa za kemikali, anaweza kula na ganda lake baada ya kuyasafisha vizuri. Lakini kwa yaliyopuliziwa dawa, maganda yake yanaweza kuwa hatari,” anasema.
Kuzenza Madili, Mratibu wa Uhaulishaji Teknolojia kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kigoma, anakazia hoja hii.
Anasema kila dawa ina utaratibu wa muda wa kusubiri kabla ya kuvuna, lakini baadhi ya wakulima huzingatia faida ya haraka na kuvuna kabla ya muda huo, hivyo kuhatarisha afya za walaji.
“Ukila matunda yaliyovunwa mapema baada ya kupuliziwa dawa, unaweza kupata sumu mwilini au vimelea vya magonjwa hata kama madhara hayajitokezi mara moja,” anasema.
Kwa upande wake, Mtafiti wa afya ya jamii, Aloisia Shemdoe, anashauri walaji kuyaosha matunda kwa maji yenye chumvi kabla ya kuyatumia. Anaongeza kuwa maganda ya ndizi mbivu na nanasi ni mazuri iwapo yatachemshwa na kusagwa.
Virutubishi katika matunda
Vitamini huwezesha mwili kufanya kazi zake, kuimarisha kinga na kupunguza hatari ya maradhi. Vitamin A hupatikana kwenye matunda ya rangi ya njano/orange, huku Vitamin C ikipatikana kwenye matunda yenye uchachu.
Madini ya Potassium husaidia kudhibiti msukumo wa damu, sodium hutunza afya ya moyo, na folate husaidia utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu, muhimu hasa kwa wanawake wajawazito.
Makapimlo yanarahisisha usagaji chakula, kuzuia choo kigumu, kupunguza lehemu na hatari ya magonjwa ya moyo.
Moja, epuka kunywa maji mara tu baada ya kula matunda kwa sababu ya tindikali nyingi.
Mbili, usihifadhi matunda kwenye joto kali au baridi sana; yaweke sehemu yenye hewa ya kutosha.
Tatu, maganda ya baadhi ya matunda kama chungwa na ndimu hayatakiwi kuliwa, ila mengine kama embe na tikiti yanaweza kuliwa kulingana na usalama wake.