Mahakama yamtaka IGP, wenzake kuwasilisha utetezi wa kumshikilia Heche

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imewataka Mkuu wa Jeshi la Polisi  (Inspector General of Police – IGP) na wenzake wengine watano, kuwasilisha utetezi wao katika la  kushikiliwa kwa Makamu Mwenyekiti wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara John Heche, kufikia Jumapili.

Mahakama hiyo imetoa amri hiyo leo Ijumaa, Novemba 7 , 2025 wakati shauri hilo lilipotajwa kwa mara ya kwanza.

Shauri hilo la maombi lilifunguliwa mahakamani hapo  mawakili wa Chadema  kwa niaba ya Heche, wakiomba amri ya Mahakama kuwataka wajibu maombi kumfikisha mahakamani kiongozi huyo au kumwachilia huruma kwa dhamana (Habeous Corpus).

Katika shauri hilo  ambalo mwombaji ni Heche mwenyewe, wajibu maombi ni  IGP ambaye ndiye mjibu maombi wa kwanza na  Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu (Dar es Salaam -ZCO).

Wajibu maombi wengine ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (RCO) Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serilali (AG ).

Wakati shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Obadia Bwegoge lilipotajwa Heche amewakilishwa na jopo la mawakili wanne lililoongozwa na Mpale Mpoki, akisaidiwa na Mawakili Edson Kilatu, Seleman Matauka na Paul Kisabo.

Kwa upande wa wajibu maombi wamewakilishwa na jopo la mawakili wa Serikali watano lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Agatha Pima.

Wakili Mpoki ameieleza Mahakama kuwa wajibu maombi wote wameshapatiwa hati za wito wa kufika mahakamani lakini akaiomba mahakama iwasikilize maombi yao ya upande mmoja.

Wakili Pima amekiri wajibu maombi wote kupokea hati za wito kwa wajibu maombi hao kufika mahakamani na kwamba ndio maana wao wamefika mahakamani.

Hata hivyo amesema kuwa kwa kuwa tayari pande zote wamefika mahakamani hapakuwa na haja ya kusikiliza maombi ya mwombaji ya nafuu za upande mmoja badala yake akapendekeza wasikilizwe pande zote.

Pia, wakili Pima ameomba muda kwa wajibu maombi kuwasilisha kiapo kinzani (utetezi wao).

Akisisitiza hoja yake wakili Mpoki amesema kuwa hilo ni shauri la  maombi lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, linalohusu haki ya uhuru wa mtu ambaye ameshikiliwa na polisi kwa zaidi ya  wiki mbili.

Hivyo amesisitiza kusikilizwa upande mmoja na akionesha hofu kuwa kama ombi la Jamhuri litakubaliwa la muda wa kuwasilisha kiapo kinzani huenda shauri hilo likafika Jumatano Juma lijalo kabla ya kusikilizwa.

Amedai kuwa anasema hivyo kwa kuwa hakuna uwezekano wa wajibu maombi kuwasilisha kiapo kinzani leo isipokuwa mpaka Jumatatu.

“Kama wanadhani ana kesi basi wampelekee mahakamani kwani kinachoendelea kwa sasa ni kinyume cha Sheria,  kwa hiyo tunaomba aachiliwe huru.

Jaji, Bwegoge baada ya kusikiliza hoja za pande zote  ameelekeza wajibu maombi wawasilishe kiapo kinzani kabla au kufikia Jumapili Oktoba 9, na akaelekeza shauri lisikilizwe Jumatatu, Oktoba 10, 2025.

“Kwa hiyo shauri hili litasikilizwa pande zote Jumatatu Oktoba 10, 2025, saa 4:30, asubuhi,”amesema Jaji Bwegoge.

Heche amekuwa akishikiliwa na Polisi tangu  Oktoba 22, 2025 alipokamatwa nje ya geti la Mahakama Kuu Dar es Salaam, alipokuwa akienda mahakamani japo. kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini.

Baada ya kukamatwa awali chama hicho kilitoe taarifa kwa umma kuwa Jeshi la Polisi Dar es Salaam liliwaeleza kuwa mwanasiasa huyo kusafirishwa kupelekwa Tarime, Mara, lakini familia na ndugu zake walipomtafuta katika vituo vya Polisi Tarime na Musoma hawakuweza kumpata

Hata hivyo baadaye ilifahamika kuwa alipelekewa Dodoma ambako alikuwa anashikiliwa katika kituo cha Polisi Mtumba, bila kumpatia dhamana wala kumfikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria za nchi.

Hata hivyo katika taarifa iliyotolewa na Wakili Hekima Mwasipu kuzi, Novemba 4, 2025,  Heche alisafirishwa tena siku hiyo kurejeshwa Dar es Salaam ambapo alifikishwa katika kituo cha Polisi Mburahati, Mkoa wa Kinondoni na kuhojiwa.

“Amepewa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kigaidi kutoka Kimara mpaka Magomeni na kujihusisha na vitendo vya kigaidi maeneo ya Msewe na Extenal,” alisema Wakili Mwasipu katika taarifa yake hiyo.

Hata hivyo Wakili Mwasipu alisema kuwa  baada  ya kutakiwa kuandika maelezo ya onyo Heche alitumia haki yake ya kisheria ya kukataa kuandika maelezo na kwamba atatumia haki hiyo mara baada ya kupelekwa mahakamani.

Hata hivyo wakati maombi hayo yalisajiliwa jana Mahakama Kuu, na kupangiwa kusikilizwa kesho, Jana Heche alikuwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, maarufu kama Mahakama ya Kisutu, kusomewa mashtaka hayo.

Tangu asubuhi hali ya ulinzi imeimarishwa katika eneo la Mahakama ya Kisutu ambapo askari polisi waliovaa sare na wengine kiraia wasambaa maeneo mbalimbali ndani na nje ya viwanja vya mahakama hii.

Hata hivyo mpaka saa 12 jioni alikuwa hajafikishwa mahakamani kwa kuwa hati ya mashtaka yake ilikuwa haijasajiliwa  katika mfumo wa Mahakama kutokana na changamoto ya mtandao.

Kutokana na hali hiyo leo, Ijumaa Oktoba 7, 2025 alitarajiwa kufikishwa mahakamani hapo mapema na kama kawaida haki ya ulinzi iliimarishwa na askari wa Jeshi la Polisi tangu asubuhi mapema.

Hata hivyo mpaka shauri la maombi yake Mahakama Kuu lilipoitwa Heche alikuwa bado hajafikishwa mahakamani alikuwa alikuwa hajafikishwa mahakamani.

Mpaka mchana saa 7:40 bado alikuwa hajafikishwa mahakamani huku mawakili wake wakiendelea kusubiria kujua hatima hiyo.