Mtifuano wa uspika ulivyoota mizizi CCM

Dar es Salaam. Mtifuano wa nafasi ya Spika kati ya Spika wa sasa, Dk Tulia Ackson, na naibu wake, Mussa Azzan Zungu, kunaifanya nafasi ya unaibu kama hatua ya maandalizi kuelekea uspika.

Hivyo ndivyo inavyoonekana kwa baadhi ya waliowahi kushika wadhifa wa Naibu Spika, ambao baadaye walijitokeza kuwania nafasi ya Spika, kana kwamba nafasi hiyo ni hatua ya maandalizi.

Ni mtifuano, ndivyo unavyoweza kuelezea kinachoendelea baada ya Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, kuchukua fomu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania nafasi ya Spika inayoshikiliwa na “bosi” wake, Dk Tulia Ackson.

Safari ya urithi wa nafasi ya Spika imekuwa na sura tofauti, ikianzia na Spika Adam Sapi Mkwawa, ambaye Naibu Spika wake, Pius Msekwa, alirithi wadhifa huo.

Juzi, Kamati Kuu Maalumu ya CCM katika kikao chake kilichofanyika jijini Dodoma chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan, iliteua majina ya wagombea wa nafasi ya Spika na Naibu Spika kwa ajili ya Bunge la 13.

Kwa nafasi ya Spika, walioteuliwa kuwania ni Dk Tulia Ackson, Mussa Azzan Zungu na Stephen Masele

Kwa upande wa Naibu Spika, walioteuliwa kuwania ni Najma Giga, Daniel Sillo na Timotheo Mzava. Wagombea hao watapigiwa kura na Kamati ya Wabunge wa CCM kabla ya kupigiwa kura bungeni.

Msekwa licha ya kuwa Naibu Spika pia, kutokana na hali ya kiafya ya Spika Adam Sapi Mkwawa, aliongoza Bunge akiwa Naibu kwa muda mrefu.

Pia, alikuwa mmoja wa viongozi wenye uzoefu mkubwa zaidi wa utawala wa umma, Katiba na utaratibu wa Bunge.

Hivyo, alipanda na kuwa Spika katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi vya siasa, ambapo Bunge lilihitaji kiongozi mwenye uzoefu, utulivu na uwezo wa kusimamia mivutano ya kisiasa iliyokuwa imeanza.

Samuel Sitta aliongoza Bunge la Tisa kwa mwelekeo wa “Bunge la kasi na viwango” (speed and standard), akisisitiza uwajibikaji wa Serikali, huku Anne Makinda akifanya kazi kama Naibu Spika wake.

Hata hivyo, baada ya Spika Sitta kutoteuliwa kwa mara nyingine na vikao vya CCM kuwania nafasi hiyo, Anne Makinda alichaguliwa kuwa Spika.

Wakati Makinda akiwa Spika wa Bunge, Job Ndugai alikuwa Naibu Spika, akisimamia vikao na kukabiliana na wabunge wa upinzani waliokuwa wengi na wenye mijadala mikali.

Uzoefu wa Ndugai wa miaka mitano kwenye nafasi ya Naibu Spika ulimuwezesha kusimamia Bunge lililojaa mivutano na wabunge wa upinzani.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, na baada ya Job Ndugai kuapishwa kuwa Spika, alikumbwa na matatizo ya kiafya yaliyomlazimu kusafiri nje ya nchi kwa matibabu yaliyochukua muda mrefu.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, alilazimika kushika majukumu ya Spika kwa muda mrefu.

Pia, baada ya Spika Ndugai kujiuzulu, nafasi hiyo ilitakiwa kujazwa haraka. Dk Tulia Ackson alikuwa chaguo la wazi na la kimantiki kwa CCM kutokana na uzoefu wake kama Naibu Spika na uwezo wake wa kitaaluma.

Mussa Hassan Zungu alichaguliwa kuwa Naibu Spika akiwa na uzoefu wa muda mrefu wa ubunge na uongozi kama mwenyekiti wa Bunge na Kamati.

Zungu kwa sasa kuwania nafasi ya Spika inaonyesha kuwa, kwa nafasi yake, anaelewa utamaduni wa Bunge ambapo nafasi ya Naibu Spika huonekana kama nafasi ya kujiandaa kwa uspika.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Onesmo Kyauke, amesema uamuzi wa chama kuwasilisha majina ya aliyekuwa Spika na Naibu wake katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Spika wa Bunge unaonesha kuwa chama hicho hakina mgombea mwenye kipaumbele maalumu, hivyo kimeamua kuwaachia wabunge wenyewe wamchague wanayemwamini zaidi.

Kyauke amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwani inaleta ushindani wa haki na inalenga kumaliza ubishi wa kisiasa uliokuwepo miongoni mwa wanachama na wabunge.

“Ingawa ni vigumu kisiasa kutabiri nani ataibuka mshindi, lakini ninavyoona, huenda Zungu akapata nafasi hiyo. Ni mtu mcheshi, mwenye uzoefu na umri umeenda, jambo ambalo linaweza kumfanya awe chaguo sahihi kwa wabunge wengi vijana wanaohitaji kiongozi mwenye busara na uwezo wa kuhimili changamoto za Bunge,” amesema Kyauke.

Hata hivyo, ameeleza kuwa hoja ya umri inaweza pia kuleta mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo, kwani baadhi wanaweza kutaka kiongozi kijana mwenye nguvu na maarifa mapya ya kushindana na wabunge vijana katika mijadala mbalimbali.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Hamduny Marcel, amesema katika kinyang’anyiro cha uspika wa Bunge, Dk Tulia ana nafasi kubwa ya kushinda licha ya mpinzani wake, Zungu, kuwa si mnyonge kisiasa.

Kwa mujibu wa Marcel, Zungu ni “mtoto wa mjini” na mzoefu katika shughuli za Bunge, lakini nguvu ya Tulia ipo kwenye ujuzi wa sheria, sifa na hadhi alizonazo kimataifa.

“Sababu za Tulia kushinda ziko wazi. Kwanza, ni mjuzi wa masuala ya sheria, lakini pia ni Rais wa Muungano wa Mabunge Duniani (IPU), nafasi ambayo anaiwakilisha vyema nchi na inaweza kuwa turufu kwake,” amesema Marcel.

Ameongeza kuwa uwezekano wa wanawake kumchagua mwenzao ni mkubwa, ingawa wakati mwingine hali hiyo inaweza kubadilika kutokana na mienendo ya kisiasa.

“Ni kweli wanawake wanaweza kumpa kura mwenzao, lakini si rahisi kutabiri msimamo wao kwa uhakika. Hata hivyo, mazingira ya sasa yanaonesha wengi wao wanashika nafasi za juu, jambo linaloweza kumpa nguvu zaidi Tulia,” amesema.

Marcel amesema kuwa ingawa Zungu ana sifa za ujasiri na uzoefu, changamoto kwake inaweza kuwa taswira ya kisiasa iliyoibuka kwamba wanawake kwa sasa wanapewa nafasi kubwa katika uongozi.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Enzi Talib, amesema katika kipindi cha sasa, Bunge la Tanzania linahitaji kiongozi mwenye maarifa ya kina katika masuala ya sheria na ujasiri wa kiuongozi kama Dk Tulia, ambaye ameonesha weledi mkubwa katika kulitumikia Taifa kupitia nafasi yake ya Spika.

Akizungumza kuhusu mwenendo wa uongozi wa Bunge, Enzi amesema licha ya mpinzani wa Dk Tulia kuwa na uzoefu katika shughuli za Bunge, bado Dk Tulia ana sifa zinazomtofautisha kutokana na elimu yake ya kisheria na uzoefu mpana wa kimataifa.

“Tulipofikia sasa, kiongozi wa Bunge letu anapaswa kuwa na uzoefu wa ndani na nje ya nchi. Dk Tulia ni mtu sahihi kwa nafasi hiyo, tofauti na Zungu ambaye ana uzoefu wa siasa za ndani pekee, hivyo hawezi kuliinua Bunge katika masuala ya kimataifa,” amesema Enzi.

Licha ya Kanuni za sasa kueleza wazi kuwa Naibu Spika huchukua nafasi ya Spika anapokuwa hayupo, bado kuna haja ya kuimarisha ofisi hiyo kwa majukumu yanayojitegemea.

Kwa sasa, majukumu ya Naibu Spika yamefungwa katika kanuni inayosema kuwa yeye hutekeleza majukumu na mamlaka ya Spika pale Spika anapokuwa hayupo au anaposhindwa kutekeleza majukumu yake. Hii inajenga dhana kwamba ofisi ya Naibu Spika ni kivuli tu cha ofisi ya Spika.

Kama kingeongezwa kifungu maalumu kwenye Kanuni za Bunge au Katiba, kingeongeza thamani na mamlaka ya ofisi hiyo kwa kumpa Naibu Spika jukumu la kipekee la kuongoza moja kwa moja Kamati Maalum au za kudumu ambazo zinahusisha masuala muhimu ya Bunge.

Mfano, kuwa kiongozi wa Kamati ya Maadili ya Wabunge au Kamati ya Utawala na Rasilimali za Bunge. Kutofautisha majukumu kutasaidia kutofautisha ofisi yake na kazi za Spika, akifanya kazi sambamba na Spika na siyo tu kumsubiri Spika aondoke.

Pia, Naibu Spika anaweza kupewa mamlaka ya kusimamia moja kwa moja utendaji wa Idara Maalum au Kurugenzi ndani ya Ofisi ya Bunge (kutoka kwa Katibu wa Bunge), kama vile Kurugenzi ya Utafiti, Kurugenzi ya Mafunzo kwa Wabunge, au Kurugenzi ya Mawasiliano ya Bunge.