NIFFER APANDISHWA KIZIMBANI AKIKABILIWA NA MASHTAKA YA UHAINI

MFANYABIASHARA Jennifer Bilikwija Jovin maarufu kama Niffer, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya uhaini na kula njama.

Niffer anashtakiwa pamoja na wenzake 21 ambao ni Mwalimu, Lucianus Luchius (28), Paul Malima (28), Augustino Mulwale (30), Mohamed Kondo (30), John Mmena (26), Paul Shirima (23), Ramadhani Ramadhani (21), Levi Mkute (40), Esau Ernest Maarufu ‘Duduye’ (21), Leonard Mkonyi.

Wengine ni Fadhili Nyombi, Hamisi Hamisi, Abeid Kivuyo (24), Nicholous Shiduo (27),Abati Mwadini (27) Mika Chavala (32), Fatuma Mzengo (30), Dewji Ramji (19), Ruthmelda Silaa (21), Hilda Ngulu(22) na Yusuph Hussein(22)

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani na wakili wa serikali Mwandamizi, Clemence Kato mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya alidai washtakiwa wanakabiliwa na makosa matatu mbele ya mahakama hiyo la kwanza likiwa ni la kupanga njama na mengine mawili ni ya uhaini

Wakili Kato alidai katika tarehe tofauti kati ya Aprili na Agosti 2025, katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam washtakiwa walikula njama na kupanga kwa siri kufanya kosa la uhaini.

Aliendelea kudai kuwa shitaka la pili lilimuhusisha mshitakiwa wa pili hadi 21, ilidaiwa Oktoba 29, 2025, katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wakiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliunda nia ya kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Alidai washitakiwa walifanya hivyo kwa lengo la kutishia mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na walionyesha nia hiyo kwa kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za Serikali zinazokusudiwa kutoa huduma muhimu.

Wakili Kato alidai shitaka la tatu linamuhusu Niffer peke yake ilidaiwa kati ya Agosti na Oktoba 2025, katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, akiwa chini ya utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wakiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliunda nia ya kushawishi umma kuzuiya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Alidai mshitakiwa alifanya hivyo kwa lengo la kutishia mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na walionyesha nia hiyo kwa kuhamasisha umma kununua barakoa katika biashara yake kwa ajili ya kujikinga na mabomu ya machozi katika maandamano ya kupinga Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhisiwa Hakimu kujibu kitu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza makosa ya uhaini.

Baada ya mahakama kueleza hayo jopo la Mawakili wa utetezi likiongozwa na Peter alidai anaomba hoja hizo ziingie katika rekodi Novemba 6,2025 mteja wake Niffer akiwa chini ya himaya ya jeshi la polisi katika kituo cha polisi Oysterbay alifanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo kupigwa na maofisa kadhaa ambao walimlazimisha asaini maelezo yanayosemekana kuwa ni ya onyo.

Alidai na ilikuwa hivyo kwa washtakiwa wengine kuanzia wa pili hadi wa 22 katika tarehe tofauti ambazo walichukuliwa maelezo yao, alidai aliomba ikae katika rekodi za mwenendo wa ukabidhi ili wakiibua pingamizi lolote la kisheria isionekanane kuwa hawakusema awali.

“Tunaomba mahakama hii itoe amri watakapokabidhiwa kwa uongozi wa magereza kwa sababu tunajua ina zahanati na hospitali ya serikali tunaomba wafanyiwe uchunguzi wa kitabibu juu ya majeraha hayo na ripoti hiyo chini ya uongozi wa magereza iletwe mahakamani,” alidai Kibatala.

Pia alidai kosa hilo lipo ndani ya mamlaka ya mahakama hiyo akisisitiza kuwa lilikuwepo kimakosa kwa sababukuwepo kwa sababu kuna kosa la pili na la tatu tayari, hivyo aliomba mahakama lifutiliwe mbali akisistiza hati ilikuwa na mapungufu.

Pia alidai ili mahakama iweze kufanya mwenendo wa ukabidhi unatakiwa kuwa na taarifa binafsi za washitakiwa lakini jamhuri walidai katika hati ya mashitaka zilikosekana taarifa za mshtakiwa wa 19 hadi 22, hivyo itapelekea mahakama kushindwa kuamua kwa usahihi.

Baada ya hoja hizo upande wa Jamhuri waliomba mahakama ahirisho ili kuweza kujiandaa na kuja kujibu hoja hizo za mawakili wa utetezi hapo jumatatu, Kibatala alipinga ombi hilo alidai kama ni marekebisho basi wapewe ahirisho la saa moja ili shauri liweze kuendelea na hakimu apate nafasi ya kwenda kuandika uamuzi.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili Hakimu Lyamuya alisema kuhusu umri wa washtakiwa ni wazi kuwa washitakiwa hao watano ambao taarifa zao hazipo umri ni sawa.

“Mimi niliopo hapa nipo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuwaona kuliko waliosoma umri wao hakuna mtoto hapo na nimejiridhisha kuwa hakuna hoja ya umri tena,” alisema Hakimu.

Alisema kuhusu kuchunguzwa afya za washitakiwa alihitaji majibu ya serikali kwamba mshitakiwa yeyote anayehisi anatatizo la afya atoe taarifa kwa magerezwa na achunguzwe na ripoti upande wa magereza waipeleke mahakamani ili iwe sehemu ya mwenendo wa kesi.

Pande zote zilikubaliana shauri hilo kurudi Novemba 11, mwaka huu kwa ajili ya Jamhuri kujibu hoja na itasikilizwa kwa njia ya mtandao lakini siku ya uamuzi washitakiwa wote watafikishwa mahakamani.