Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, amefungua mashtaka dhidi ya mwanamume aliyempapasa hadharani wakati akizungumza na wafuasi wake karibu na Ikulu ya Kitaifa, jijini Mexico City.
Tukio hilo lilitokea Jumanne, na linasambaa sana mitandaoni kupitia video za simu za rununu ambazo zinaonyesha Rais Sheinbaum akizungumza na wananchi kabla ya mwanamume mmoja kumkaribia kutoka nyuma, kujaribu kumbusu shingoni na kumshika mwilini.
Sheinbaum alionekana kushituka na kuondoka haraka, huku mmoja wa wasaidizi wake akiingilia kati kumlinda. Polisi walimkamata mtuhumiwa muda mfupi baadaye.
Baada ya tukio hilo, Rais Sheinbaum ametoa wito wa unyanyasaji wa kijinsia kutambuliwa kama kosa la jinai kote nchini Mexico, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayeweza kuvunja heshima ya mwanamke, awe raia wa kawaida au kiongozi wa nchi.
Mashirika ya kutetea haki za wanawake yamepongeza hatua hiyo, yakisema tukio hilo limeonesha kwa uwazi ukubwa wa tatizo la unyanyasaji wa kijinsia na dhana ya ubabe wa kiume nchini humo.
Ripoti zinaonyesha kuwa asilimia 98 ya mauaji ya kijinsia nchini Mexico hayaadhibiwi, hali inayoibua hofu kuhusu usalama na usawa wa kijinsia katika taifa hilo.
Related
