Zikiwa zimesalia siku mbili pekee kufungwa kwa zoezi la upigaji kura za kuwatafuta wanariadha bora duniani kwa mwaka 2025, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limewaomba wadau kumpigia kura nyota wa mbio ndefu, Alphonce Simbu, ili kuweka historia mpya kwa taifa.
Simbu ameweka rekodi ya kipekee kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kufuzu katika hatua ya mwisho ya tuzo za mwanariadha bora wa dunia katika kipengele cha mbio za nje ya uwanja, zinazotolewa na Shirikisho la Ridha Duniani (WA).
Safari yake imefika hatua ya fainali akichuana na Mkenya, Sebastian Sawe, mshindi wa mbio maarufu za London Marathon na Berlin marathon.
Kwa upande wa Simbu, umahiri wake ulionekana wazi baada ya kuibuka mshindi katika marathoni ya dunia iliyofanyika Septemba 2025, Tokyo, Japn, hatua iliyompa nafasi ya kuingia kwenye orodha ya majina makubwa duniani.
Rais wa RT, Rogath John Stephen Akhwari, amesema ni muda wa Watanzania kusimama pamoja kumlinda na kumuinua shujaa wao, akisisitiza kuwa kura za Watanzania zina uzito mkubwa wa kumfanya Simbu kushinda.
“Hii ni nafasi adhimu kwa taifa, Simbu sio tu ameiwakilisha Tanzania, bali ameipeleka kwenye ramani ya dunia, tunaomba Watanzania wote ndani na nje ya nchi kumpigia kura, tunaamini kabisa Simbu ana uwezo na nafasi ya kushinda,” amesema Akhwari.
Zoezi la kupiga kura kwa nyota waliotinga fainali lilianza Novemba 4, 2025 kupitia tovuti ya shirikisho la riadha la dunia na linatazamiwa kukamilika Novemba 9, 2025 ambapo washindi watatangazwa kwenye usiku wa tuzo ambazo zitafanyika Novemba 30, 2025 jijini Monaco, Ufaransa.
Katika makundi mengine ya tuzo hizo, wapo wanariadha waliopenya kama vile bingwa wa dunia kuruka vihunzi mita 400, Femike Bol wa Uholanzi na bingwa wa dunia mita 400, Sydney McLaughlin-Levrone wa Marekani wanaowania tuzo za mwanariadha bora wa mbio za uwanjani wanawake.
Wengine ni mshindi wa dunia mita 200, Noah Lyles (Marekani), Emannuel Wanyonyi (Kenya), mshindi wa dunia mita 800, upande wa wanaume.
Wapo pia bingwa wa dunia kuruka mbali, Tara Davis- Woodhal (Marekani), bingwa wa dunia kuruka juu, Nicola Olyslagers (Australia) katika tuzo za mwanariadha bora wa fani za uwanjani wanawake, bingwa wa dunia kuruka kijiti, Mondo Duplantis (Sweden) na bingwa wa dunia kuruka mbali, Mattia Furlani wa Italia, upande wa wanaume.
Upande wa mwanariadha bora wa kike wa mbio ndefu nje ya uwanja wapo Peres Jepchirchir kutoka Kenya ambaye ni bingwa wa marathoni wa dunia, pia bingwa wa dunia wa mbio za kutembea, mbio za kilomita 20 na 35, Maria Perez wa Hispania.