Simulizi ya mganga aliyehukumiwa kunyongwa kwa mauaji ya muuguzi mstaafu KCMC -1

Moshi. Ni simulizi ya kushtua ya mganga wa jadi, Omary Rang’ambo, aliyemuua kikatili muuguzi mstaafu wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Patricia Ibreck (66) na kumzika kisha akadanganya amechukuliwa na mizimu.

Mauaji hayo yalitikisa mji wa Moshi na vitongoji vyake, ikizingatiwa kuwa awali, miongoni mwa waliokuwa wanashikiliwa kwa mahojiano ni mtoto wa marehemu, Wende Mrema, ambaye baadaye ilionekana hakuhusika.

Ni mauaji yaliyotokea tarehe na mwezi usiofahamika mwaka 2021 katika eneo la Rau Mrukuti, nje kidogo ya mji wa Moshi, lakini ilieleza mama huyo yuko India kwa matibabu, kabla ya kugundulika baadaye kuwa aliuawa na kuzikwa pembeni mwa nyumba yake.

Mwili wake ulifukuliwa Januari 9, 2022 ikiwa ni baada ya mwaka mmoja tangu auawe. Ndani ya shimo alipozikwa, kulikutwa jambia lililotumika katika mauaji, shuka lililotumika kufunika mwili wake na sidiria ikiwa kifuani mwa marehemu.

Baada ya Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi kusikiliza mashahidi 13 wa Jamhuri na kupokea vielelezo vinane, kisha kusikiliza utetezi wa mganga huyo na kupima ushahidi katika mizania, amemtia hatiani mshtakiwa.

Katika hukumu aliyoitoa Novemba 5, 2025 na kupatikana katika tovuti ya Mahakama (TanzLII), Jaji Simfukwe amemhukumu mganga huyo kunyongwa hadi kufa kwa kuwa ndiyo adhabu pekee ya kosa la kuua kwa kukusudia.

Simulizi hii itaegemea katika ushahidi uliotolewa na mashahidi 13 wa Jamhuri, akiwamo binti wa marehemu, Wende na  utetezi wa mshtakiwa na uchambuzi wa Jaji kuhusu ushahidi na adhabu yenyewe.

Aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Moshi (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Leons Mwamunyi alieleza mwaka 2021 kulikuwa na taarifa za kutoweka kwa Patricia alizopokea kutoka kwa ndugu na uongozi wa Kijiji cha Rau.

SP Mwamunyi aliyekuwa shahidi wa 11 wa Jamhuri, aliieleza mahakama kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo alitembelea nyumbani kwa Patricia alikomkuta mtoto wake wa kike, Wende aliyekuwa akiishi na mama yake.

Alipomuuliza mama yake yuko wapi, alimweleza kuwa hakuwepo nyumbani kwa zaidi ya miezi tisa, lakini alitilia mashaka majibu yake akaamua kumchukua na kwenda naye Kituo Kikuu cha Polisi Moshi kwa ajili ya kufanya mahojiano naye.

SP Mwamunyi alieleza katika maelezo yake ya kwanza, Wende aliwaeleza Polisi kuwa mama yake alikuwa amekwenda India kwa matibabu, lakini maelezo yake ya pili akasema kuna vijana wawili walimchukua na kwenda naye Tanga kwa matibabu.

SP Mwamunyi aliiambia mahakama katika uchunguzi wao walibaini Patricia hakuwa nje ya nchi na kwa kuwa Wende aliwataja watu wawili, Waziri na Omary kuwa wanahusika na kutoweka kwa mama yake, uchunguzi rasmi ulianza.

Kwa mujibu wa SP Mwamunyi, Desemba 31, 2021 mtu aitwaye Waziri alikamatwa Korogwe, mkoani Tanga na kupelekwa Moshi. Alipohojiwa alimtaja Omary, ambaye anaishi Bomang’ombe kuwa ndiye anajua alipo Patricia Ibreck.

Timu ya wapelelezi ilikwenda kwa Omary kwa kuongozwa na Waziri, lakini hawakumkuta. Walijulishwa amehamia Kigamboni, Dar es Salaam.

Shahidi huyo alieleza aliwasiliana na Polisi Temeke ili wasaidie kukamatwa kwa Omary.

Januari 2, 2022, shahidi huyo alijulishwa kuwa Omary amekamatwa, hivyo alituma makachero wawili kwenda kumchukua. Katika mahojiano ya mdomo, mtuhumiwa huyo alikiri kumuua Patricia na kumzika kwenye shimo la takataka.

Shahidi huyo alimjulisha mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro, akamuomba afanye utaratibu wa kufanyika uchunguzi wa kisayansi. Januari 8, 2022, Omary alirejeshwa mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, yeye alipata fursa ya kumhoji Omary ambaye alimweleza alimuua Patricia kwa kutumia jambia na kwamba baadaye alimzika karibu na mti ulio karibu na nyumba ya marehemu na alikubali kuonyesha alipomzika.

Omary ambaye alikiri tuhuma wakati huo na sasa amehukumiwa kunyongwa hadi kufa, aliwapeleka makachero hadi eneo alipomzika Patricia, lakini kwa kuwa ilikuwa saa 4:00 usiku hawakuweza kufanya lolote, hivyo eneo liliwekewa ulinzi.

Siku iliyofuata baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria, mwili wa Patricia ulifukuliwa mbele ya daktari wa KCMC aliyekuwa shahidi wa 10, wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi, mwenyekiti wa kijiji na baadhi ya ndugu wa marehemu.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, walipata mabaki ya mwili wa Patricia ukiwa umeoza, kulikuwa na jambia ndani ya shimo hilo, shuka lililotumika kumfunika marehemu na nguo za ndani ikiwamo sidiria.

Mabaki ya mwili huo yalipelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako sampuli za vinasaba (DNA) zilichukuliwa kutoka kwenye mifupa na meno, udongo lilipopatikana jambia na mwili ulipozikwa, pia sampuli kutoka kwa washukiwa.

Sampuli hizo zilitumwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi na ilithibitishwa kuwa mabaki ya mwili ule ulikuwa ni wa Patricia.

Shahidi wa saba wa Jamhuri alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Jumanne Kimu, aliyeeleza namna alivyopokea simu kutoka kwa RCO Kilimanjaro ili kumtafuta Omary.

RCO Kilimanjaro alimjulisha shahidi huyo kuwa mtuhumiwa alikuwa anajulikana kama Omary Mahmoud na alifika Kilimanjaro kwa ajili ya kumtibu Patricia na kwamba mwanamke huyo alikuwa ametoweka.

Polisi Kilimanjaro walimhitaji mtuhumiwa huyo ili aeleze mahali alipo Patricia kwa kuwa ndiye mtu wa mwisho aliyekuwa naye, hivyo alimpigia simu Omary na kujifanya wao ni watu wenye shida ya kupata huduma yake ya uganga.

Mtuhumiwa aliwapokea vizuri kwenye simu na kuwaelekeza eneo analopatikana kuwa ni Vijibweni, Kigamboni, mkoani Dar es Salaam. Walikwenda wakiwa timu ya makachero wakamkamata mganga huyo.

Shahidi wa tatu, Inspekta Sunday Nzari, alieleza namna yeye na askari mwenzake walivyosafiri kutoka Moshi hadi Dar es Salaam kumfuata mtuhumiwa huyo na walipofika walimfanyia mahojiano na akakiri alimuua Patricia wakati anamtibu.

Omary aliwaeleza yeye ni mganga wa jadi na kwamba baada ya kumuua Patricia, alichimba shimo na kumzika nje ya nyumba yake mkoani Kilimanjaro.

Baada ya kupata mahali alipokuwa anaishi huko Kigamboni, alieleza yeye na makachero wenzake walikwenda kufanya upekuzi wakapata nguo mbili, hirizi, pembe mbili, mkia na vitu vingine ikiwamo televisheni na Sh502, 950.

Shahidi wa tano wa Jamhuri, Lutengano Mwanginde ambaye ni mkemia kutoka Idara ya Uchunguzi wa Kisayansi ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, alielezea namna alivyoshiriki shughuli ya kufukua mwili wa Patricia Ibreck.

Kama ilivyokuwa kwa SP Mwamunyi, shahidi huyo alielezea vitu gani vilipatikana katika ufukuaji wa mwili na kueleza aina ya sampuli walizochukua kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara kuthibitisha mabaki ya mwili kama ni wa Patricia.

Kwa upande wake, shahidi wa kwanza, Khadija Mwema, ambaye ni mkemia wa Serikali alieleza namna alivyopokea sampuli kutoka ofisi ya RCO Kilimanjaro kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa DNA ambayo ilithibitika mwili ni wa Patricia.

Usikose mfululizo wa simulizi hii kesho Novemba 8, 2025 ambapo tutakuletea ushahidi wa mtoto wa marehemu ambaye alikuwa na mama yake siku anauawa.