Mbulu. Jamii ya Wahadzabe wanaoishi kwa uwindaji wa asili, kurina asali, kuokota matunda na wakusanyaji mizizi katika bonde la Yaeda Chini, Kijiji cha Domanga, kata ya Eshkesh, Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, wameomba viongozi waliochaguliwa kwenye nafasi za ubunge na udiwani kuikumbuka jamii hiyo kwa kutatua changamoto zinazowakabili.
Kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, mbunge na madiwani uliofanyika Oktoba 29, 2025 kwenye jimbo la Mbulu Vijijini, mgombea ubunge wa CCM, Dk Emmanuel Nuwas ambaye hakuwa na mpinzani, alitangazwa mshindi kwa kupata kura za ndiyo 118,665 na kura za Hapana 162.
Mwenyekiti wa Wahadzabe Tanzania, Ruben Mahaza, akizungumza Novemba 7, 2025 amesema bado jamii hiyo inakabiliwa na changamoto ya kukosa makazi rasmi na hakimiliki za ardhi, hivyo kuendelea kuhofia kupoteza maeneo yao ya asili wanayotumia kwa maisha ya kila siku.
Mahaza amesema jamii yao ni ndogo ila imekuwa ikisahaulika katika mipango ya maendeleo, jambo linalochangia wao kuendelea kubaki nyuma katika upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.
“Jamii yetu inahitaji kutambuliwa rasmi, tupatiwe ardhi na hati miliki ili tuwe na uhakika wa makazi yetu, pia, tunaomba viongozi waliopata nafasi za uongozi watupigie kelele tupate huduma kama maji, afya na elimu,” amesema Mahaza.
Ameeleza kwamba licha ya kuishi kwa kutegemea mazingira, jamii hiyo inachangia uhifadhi wa misitu na maliasili za taifa, hivyo wanastahili kupewa haki yao ya msingi ya kuishi kwa uhuru na usalama katika ardhi yao ya asili.
Mkazi wa Kijiji cha Domanga ambaye ni jamii ya Wahadzabe, Shedi Qamayu amesema eneo hilo linapaswa kutunza ili libaki la asili na siyo kutumiwa kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Amesema wanashukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali ila viongozi waliogombea na kupata nafasi watimize ahadi zao ipasavyo kwani hivi sasa wamechaguliwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakary Kuuli amesema Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa jamii hiyo hususan katika masuala ya uraia na ushiriki wa michakato ya kitaifa ikiwemo upigaji kura.
“Tulitoa elimu ya mpigakura kwa Wahadzabe na wakakubali kusitisha shughuli zao za uwindaji, kurina asali na kukusanya matunda ili kushiriki kupiga kura, hii inaonyesha mwamko na hamu yao ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo,” amesema Kuuli.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutafuta njia bora za kuhakikisha jamii hiyo inapata haki ya ardhi, huduma za kijamii na kuendelea kuhifadhi utamaduni wao bila kunyimwa fursa za kimaendeleo.