Dar es Salaam. Kisukari aina ya kwanza hutokea kwa watoto mpaka umri wa kati miaka 25 mpaka 30, lakini hivi karibuni kisukari aina ya kwanza, kimeanza kujitokeza hata kwa watu wazima na mara nyingi hutambuliwa kimakosa kama kisukari aina ya pili.
Kisukari aina ya kwanza hutokea pale mfumo wa kinga ya mwili unaposhambulia seli za kongosho zinazotengeneza insulini. Kwa watoto, mchakato huu hutokea haraka.
Kwa watu wazima, uharibifu wa seli hizi huwa wa polepole, hivyo dalili huanza taratibu. Mgonjwa anaweza kuishi miezi au miaka bila kujua, akidhani anaugua kisukari aina ya pili au tatizo jingine la kiafya.
Kwa kawaida, aina hii inapojitokeza kwa watu wazima huitwa LADA, kifupi cha Latent Autoimmune Diabetes in Adults. Tatizo hilo hufanana na kisukari aina ya pili, hasa mwanzoni.
Ndiyo maana wagonjwa wengi huanza kutibiwa kwa dawa za kumeza kudhibiti viwango vya sukari na sio insulini. Ingawa dawa hizo zinaweza kusaidia kwa muda, hali huendelea kuwa mbaya kadri kongosho linavyoishiwa uwezo.
Kuchelewa kutambua hali hii kuna madhara makubwa kama mwili kuanza kutumia mafuta kama chanzo cha nishati kutokana na ukosefu wa insulin.
Sukari ikiwa nyingi mwilini hutengeneza sumu mwilini na kumfanya mgonjwa kupata kichefuchefu, kutapika, kuishiwa nguvu, kupumua kwa haraka au hata kupoteza fahamu.
Dalili zinazojitokeza mara kwa mara ni kama kiu isiyoisha, kukojoa mara nyingi, kupungua uzito bila sababu, uchovu sugu na kuona ukungu machoni dalili ambazo zinaweza kuchukuliwa kama jambo la kawaida.
Vipimo vya C-peptide na kingamwili dhidi ya kongosho vinaweza kusaidia kubaini kama ni kisukari aina ya kwanza au aina ya pili. Vipimo hivyo vinasaidia kuonyesha kama mfumo wa kinga umeanza kushambulia seli zinazozalisha insulini.
Kama ikithibitishwa kuwa mgonjwa ana kisukari aina ya kwanza, matibabu ya insulini yanaanza mara moja ili kulinda viungo vya mwili na kupunguza hatari ya kupoteza viungo kama macho na figo
Nchini Tanzania, changamoto ya uelewa wa kisukari aina hii bado ipo, hasa vijijini ambako huduma za vipimo ni chache. Watu wanaopata kisukari aina ya kwanza hukosa elimu sahihi na hujikuta wakilaumu chakula, msongo au uchovu wa kazi. Kisukari aina ya kwanza si ugonjwa wa kula vyakula fulani, bali ni tatizo la kinga ya mwili.
Jamii inapaswa kutambua kuwa kisukari aina ya kwanza si cha watoto pekee, yeyote anaweza kupata kisukari aina ya kwanza iwe mtoto, kijana au mtu mzima.
Ni muhimu kupata elimu ya mapema, vipimo sahihi na matibabu ya insulin. Pia kuhudhuria kliniki, kusikiliza na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na lishe.