Zanzibar yatoa punguzo la asilimia 80 tozo ya bidhaa za chakula, sababu yatajwa

Unguja. Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) limetangaza kutoa punguzo la asilimia 80 ya tozo ya aridhio (Wharfage) kwa bidhaa zote za chakula zinazoingia nchini kupitia bandari zote zinazohudumiwa na shirika hilo na eneo la ngalawa (Dhowshed) linalosimamiwa na Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT).

Uamuzi huo umeidhinishwa na ZPC ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa muhimu lililojitokeza baada ya uchaguzi mkuu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu punguzo hilo leo Novemba 7, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa ZPC, Akif Ali Khamis amesema punguzo hilo linahusisha bandari zote chini ya usimamizi wa shirika la bandari.

“Hii inajumuisha bandari ya Malindi, Mkokotoni, Mkoani, Wete pamoja na eneo la Dhowshed linalosimamiwa na ZMT. Hatua hii inalenga kutoa nafuu kwa wafanyabiashara wa bidhaa za chakula, kuimarisha upatikanaji wa bidhaa hizo sokoni na hatimaye kusaidia wananchi kupata chakula kwa bei nafuu,” amesema Akif.

“ZPC inatambua wajibu wake katika kusaidia uthabiti wa uchumi wa nchi kupitia sekta ya bandari. Punguzo hilo la tozo ni sehemu ya mchango wetu kuhakikisha bidhaa muhimu za chakula zinawasili kwa gharama nafuu na zinawafikia wananchi bila mzigo wa ziada wa bei,” amesema Akif.

Amesema utekelezaji wa punguzo hilo utadumu kwa wiki mbili kuanzia Jumatatu Novemba 10 hadi Novemba 24, 2025.

Amesema Shirika la Bandari Zazibar linaendela kushirikiana na taasisi zote za Serikali na sekta binafsi kuhakikisha bandari za Zanzibar zinabaki kuwa kiungo muhimu cha kukuza uchumi, biashara na ustawi wa jamii.

Hatua hiyo inakuja baada ya kusitisha safari kwa siku tano kutokana na machafuko yaliyotoka siku ya uchaguzi.

Hata hivyo, amesema punguzo hilo linahusu bidhaa za vyakula vinavyozalishwa ndani ya nchi na sio bidhaa zinazotoka nje ya nchi kwani wafanyabiashara wa bidhaa hizo tayari walipunguza asilimia 100 ya uhifadhi wa bidhaa zinazotoka nje kwa siku ambazo hakukuwa na usafiri.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Akif Ali Khamis akizungumza kuhusu punguzo la tozo ya bidhaa za vyakula vinavyoingia na kutoka Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu



Kwa mujibu vipimo vya malipo, mita za ujazo (CBM) moja sawa na dola 1.12 sawa na Sh2760.80.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, mmoja wa wafanyabiashara Mohamed Mansoor amesema itasaidia kuingiza bidhaa nyingi za vyakula kusaidia pengo lililotokea wakati ambapo hakukuwa na usafirishaji.

Wakati huohuo, Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) imeelekeza wadau wote wa sekta ya usafiri baharini na wananchi kwa ujumla kutumia vitambulisho halali wakati wa ukataji wa tiketi za safari za baharini.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha ulinzi na usalama wa abiria pamoja na mali zao, sambamba na kuhakikisha mifumo ya usafiri inakuwa salama, yenye ufanisi na inayozingatia taratibu za kitaifa za utambulisho.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Novemba 5, 2025 na Mamlaka hiyo ikiwa imesainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa ZMA, imelekeza kila abiria atatakiwa kuonyesha kitambulisho halali kinachokubalika kabla ya kukata tiketi.

Katika taarifa hiyo ambayo pia imethibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa ZMA, Mtumwa Said Sandali leo Novemba 7, 2025 wakati akizungumza na Mwananchi, amesema kampuni zote za usafiri baharini zimetakiwa kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa agizo hilo.

“Vitambulisho vinavyokubalika kwa ajili ya ukataji wa tiketi ni, kitambulisho cha Taifa (NIDA), kitambulisho cha Mzanzibari (ZAN ID), Pasipoti (Passport), Leseni ya Udereva (Driving Licence), kitambulisho Maalumu cha Diaspora,” taarifa hiyo imeeleza.

Mamlaka imesisitiza kuwa utekelezaji wa agizo hilo ni wa lazima na ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ZMA katika kudumisha utulivu, usalama na uwajibikaji katika huduma za usafiri baharini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mamlaka inahimiza wananchi kufuata maelekezo hayo ili kuepuka usumbufu wakati wa ukataji wa tiketi na kuhakikisha huduma bora kwa wote.

“Tunataka kuona abiria wote wanatambulika rasmi, hii itasaidia kuongeza usalama na kurahisisha utoaji wa huduma kwa ufanisi zaidi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Nao baadhi ya wananchi wamesema agizo hilo sio jipya kwani ndio utaratibu wa kila siku ispokuwa wapo baadhi ya watendaji wa kampuni kukiuka masharti hayo na kufanya kazi kwa mazoea.

“Kiutaratibu lazima uwe na kitambulisho na siku zote huwa ipo hivyo ila changamoto kuna wakati watu wanafanya mazoea kukatisha tiketi bila kitambulisho, nadhani sasa wanataka kuhakikisha sheria inasimamiwa kama inavyotakiwa,” amesema Aroun Ali Ali.