Unguja. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura) imetangaza kupanda kwa bei za mafuta isipokuwa mafuta ya taa pekee.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa leo Novemba 8, 2025 kwa vyombo vya habari na kitengo cha uhusiano Zura, bei mpya zinaanza kutumika kesho Novemba 9, 2025.
Katika taarifa hiyo ambayo kitengo cha uhusiano kimemnukuu Mkurugenzi Mkuu wa Zura, Omar Ali Yussuf, imesema lita moja ya petroli kwa Novemba itauzwa Sh2,868 kutoka Sh2,809 ya Oktoba sawa na ongezeko la Sh59.
Pia, bei ye dizeli itakuwa Sh3,004 kutoka Sh2,944 sawa na ongezeko la Sh60 huku mafuta ya taa pekee yakisalia kwenye bei yake ya Sh3,000.
Katika taarifa hiyo imeeleza kupanda kwa mafuta ya ndege kutoka Sh2,343 ya Oktoba hadi kufikia Sh2,405 sawa na ongezeko la Sh62.
“Sababu za kupanda kwa bei za mafuta kwa Novemba inatokana na kupanda kwa gharama za uingizaji wa bidhaa za mafuta kutoka soko la Dunia hadi kufika Zanzibar,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Bei hizo zinapanda wakati ambapo Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) limepunguza asilimia 80 ya tozo ya aridhio (wharfage) kwa bidhaa zote za chakula zinazoingia nchini kupitia bandari zote zinazohudumiwa na Shirika hilo.
Punguzo la kwango hicho ni kuweka uhimilivu wa bei za bidhaa hizo ambazo zinatajwa kuvurugika kutokana na machafuko yaliyotokea siku ya upigaji kura Oktoba 29, 2025.
Kwa takribani siku tano, usafiri na usafirishaji vilisitishwa kuingia na kutoka Zanzibar, ikikumbukwa kuwa bidhaa nyingi za vyakula zinazotumika Zanzibar zinaingizwa kutoka Tanzania bara.
Hata hivyo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana Novemba 7, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa ZPC, Akif Ali Khamis alisema punguzo hilo linahusu bidhaa za vyakula vinavyotoka Tanzania n sio nje ya nchi.
Alisema hilo ni kutokana na kile alichodai kwaba tayari walitoa asilimia 100 ya Uhifadhi wa bidhaa kutoka nje ya nchi kwa siku zile ambazo bidhaa zilishindwa kuingizwa.
Wakizungumza kuhusu kadhia hiyo baadhi ya wananchi wamesema huenda gharama za maisha zikapanda zaidi baada ya mafuta kuongezeka bei kwani mambo mengi yanategemea mafuta.
“Hizi ni dalili mbaya kwa kweli, maana mafuta yakishapanda kila kitu kinapanda, na ukiangalia katika mazingira tuliyonayo kwa sasa hata bei za bidhaa nyingine sio rafiki,” amesema Juma Mtumwa Juma mkazi wa Magogoni Zanzibar.
Mwananchi mwingine, Alkadir Mahmoud amesema: “Ndio maana watu wanaishauri kuwa na stock kubwa ya mafuta nchini kuliko kutegemea kuagiza mafuta ya kila mwezi na hizi ndio athari na wanaoumia ni wananchi wa hali ya chini.”