Fursa, changamoto kusitishwa mwendokasi Kimara na Mbagala

Dar es Salaam. Wakati usafiri wa mwendokasi ukisitishwa kwa muda katika barabara za Morogoro na Kilwa, baadhi ya abiria, madereva wa pikipiki, bajaji na daladala wameeleza fursa na changamoto zinazowakabili.

Tangu Oktoba 29, 2025 yalipofanyika maandamano yaliyozua vurugu katika maeneo kadhaa mkoani Dar es Salaam, usafiri wa mwendokasi Gerezani-Kimara na Gerezani -Mbagala umesitishwa kupisha tathmini ya miundombinu iliyoharibiwa, ikiwamo kuchomwa moto.

Kusitishwa huduma ya mabasi ya mwendokasi kuimeibua fursa kwa madereva ambao baadhi licha ya kutoa huduma wamepandisha nauli tofauti na iliyozoeleka kwa maeneo husika.

Madereva waliozungumza na Mwananchi wameeleza hilo linatokana na uhitaji mkubwa wa huduma hasa kwa abiria wanaokwenda maeneo ya katikati ya mji.

Baada ya kusitishwa kwa usafiri huo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) ilitangaza kutoa vibali kwa daladala 150 ili kupunguza changamoto ya usafiri kwa barabara zilizokuwa zikitegemea zaidi usafiri wa mwendokasi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo, awali kabla ya kusitishwa kwa mabasi ya mwendokasi tayari ilishatoa vibali kwa daladala takribani 148 katika Barabara ya Morogoro.

Hivyo, baada ya kukamilika kutolewa kwa vibali kwa daladala 150 takribani mabasi 298 yatatoa huduma katika barabara hizo.

Akizungumza na Mwananchi, Shabani Athumani, dereva wa bajaji katika Barabara ya Morogoro amesema kumekuwa na abiria wengi nyakati za asubuhi na jioni hivyo kwao ni fursa.

“Nyakati za asubuhi nachukua abiria kutoka Mbezi hadi Posta kwa Sh3,000 kwa kila mmoja hadi kufika jioni naweza kutengeneza kuanzia Sh50,000. Hii kwetu imekuwa fursa tofauti na kukaa tu kijiweni kusubiri abiria,” amesema.

Kazinga John, dereva wa pikipiki katika Barabara ya Morogoro anasema kutokana na kuwapo foleni hasa asubuhi na jioni, usafiri huo umekuwa kimbilio.

“Kutoka Mbezi hadi Kariakoo au Posta napakia abiria kwa Sh5,000 kila mmoja. Kutokana na mahitaji katika barabara hii ninapata abiria si haba,” amesema.

Kwa upande wake dereva wa bajaji, Rogers Machalalya anasema licha ya mwendokasi kusitishwa, bado upatikanaji wa abiria si mkubwa kwa kiwango walichokitarajia.

“Japo tunapata-pata riziki, lakini si kwa ukubwa tulioutarajia baada ya mwendokasi kusitisha huduma, binafsi kwa siku mbili tatu hizi (Novemba 4 na 5) hamna hamna sikosi Sh60,000 hadi Sh70,000 kwa siku,” amesema.

Dereva mwingine wa bajaji eneo la Manzese, Shaban Majaliwa amesema pamoja na uchache wa abiria tangu Novemba 4, 2025 shughuli za kiuchumi ziliporejea, baadhi ya madereva wameitumia kama fursa kwa kupandisha nauli.

“Binafsi nauli ninatoza Sh2,000 kutoka Mbezi hadi Manzese, lakini wapo madereva wanaotoza hadi Sh4,000 kulingana na wingi wa abiria,” amesema.

Amesema si madereva wa bajaji pekee, bali daladala zilizopewa ruhusa ya kupita njia ya Morogoro baada ya mwendokasi kusitisha huduma baadhi zimeongeza bei ya nauli.

“Hizo daladala nazo zinatoza nauli Sh1,000 badala ya Sh600 hadi Sh700,” amesema.

Dereva wa daladala ambaye hakutaka kutajwa jina akizungumzia kuhusu kuongeza nauli amesema ni kutokana na uhaba wa abiria.

“Ile nyomi (wingi) iliyozoeleka kwenye mwendokasi kipindi cha nyuma haipo tena hivi sasa, bado abiria si wengi, hivyo ili upate hesabu, uweke mafuta na ubaki na posho wengi hatuna budi kuongeza nauli,” amesema.

Kwa muda mrefu watumiaji wa barabara ya Kilwa hasa wakazi wa Mbagala wamekuwa wakikumbana na adha ya usafiri hasa nyakati za asubuhi na jioni na kulazimika kupanda mabasi kwa kugombea.

Matumaini yalianza kuonekana Oktoba 12, 2025 yalipoanza kufanya kazi mabasi ya mwendo wa haraka na kutoa huduma ya usafiri kati ya Mbagala-Stesheni na Gerezani hali ambayo kwa kiasi kikubwa ilipunguza adha hiyo.

Hata hivyo, matumaini hayo yameyeyuka kutokana na vurugu zilizotokea Oktoba 29 na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya mradi huo, hivyo usafiri kusitishwa.

Uamuzi huo umeirudisha Mbagala na Barabara ya Kilwa katika adha ya usafiri wa umma na kuwalazimu wengi wao kutafuta usafiri mbadala zikiwamo bodaboda na bajaji.

Mwananchi imeshuhudia abiria wengi wakitumia usafiri wa bodaboda kutoka Mbagala kwenda katikati ya mji na wanaotokea mjini kwenda maeneo mbalimbali ya Mbagala.

Kijiwe cha bodaboda kilichopo jirani na stendi ya Mbagala Rangi Tatu kimekuwa eneo maalumu ambalo vyombo hivyo husimama na kukusanya abiria kama zifanyavyo daladala, kila pikipiki ikibeba abiria wawili.

Akizungumza na Mwananchi, Shani Ngwani, mkazi wa Kisemvule anayefanya shughuli zake Kariakoo amesema kusimamishwa kwa usafiri wa mwendokasi kunafanya bodaboda iwe kimbilio la wengi kutokana na uchache wa daladala.

“Mbagala kuna watu wengi daladala haziwezi kutosha, tulipopata mabasi ya mwendokasi angalau tulipata nafuu unaweza kufika Kariakoo ndani ya muda mfupi lakini sasa mambo yamekuwa magumu, kimbilio letu limekuwa pikipiki za kuchangia, mnapanda wawili hadi Kariakoo kila mtu analipa Sh2,000,” anasema.

Nehemia Kigwatu, mkazi wa Charambe amesema kusimamishwa kwa usafiri wa mwendokasi kunawarudisha gizani watumiaji wa Barabara ya Kilwa.

“Tulikuwa tumeshaanza kupata nuru lakini sasa tunarudi gizani, wamesimamisha hatujui watarudisha lini, gharama za maisha zimeongezeka wakati tulishatoka huko, maana ilikuwa ukiwa na Sh1,500 unaenda mjini na kurudi lakini sasa na hizi foleni za Mbagala lazima upande bodaboda, hivyo uandae Sh4,000,” amesema.

Mbali ya hayo, baadhi ya abiria wamedai kutozwa nauli mara mbili ya ile ya awali, kwa baadhi ikiongezeka kutoka Sh750 kwenye mwendokasi hadi Sh4,500 kwenye bodaboda na bajaji.

Angela Kiseri, anayefanya kazi Gerezani amesema kwa mwendokasi alitumia Sh750 kutoka Shekilango hadi Gerezani.

“Leo (Novemba 5) ndiyo nimeanza kwenda kazini tangu vurugu za Oktoba 29, nimepanda bajaji Sh3,000 ambayo iliishia Msimbazi, kutoka hapo hadi Gerezani nikapanda boda Sh1,500 na hapo bado kurudi,” amesema.

Dalmas Duncan, yeye amesema ametozwa Sh1,000 kutoka Magomeni Kagera hadi Gerezani akiwa kwenye daladala.

“Nauli yake huwa ni Sh500 hadi Sh600 kwa daladala, lakini leo hii naambiwa Sh1,000 karibu mara mbili,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema kwa daladala zilizopewa kibali kutokana na kusitishwa kwa mwendokasi zinapaswa kutoza nauli elekezi na si kujipangia zao.

Amesema ikitokea daladala ikapandisha nauli, abiria atume picha na sauti ili hatua zichukuliwe.

Amesema gari litakalobainika kuongeza nauli, Latra inaweza kulitaka lifunge mfumo wa tiketi za kielektroniki.

“Watu wanapaswa kuendelea kuheshimu sheria, bei elekezi ya daladala inafahanika kwa kilomita zisizozidi 10 ni Sh600. Kilomita 11- 15 ni Sh700 na kwa kilomita 16-20 ni Sh800 na hiyo njia haizidi kilomita 20,” amesema.

Amewashauri abiria wanapopandishiwa nauli waungane kwa pamoja kutokubali.

“Waungane na kupeleka gari kituo cha polisi, wanaofanya hivyo adhabu zake ni kubwa zinajulikana ikiwamo faini ya Sh100,000 hadi Sh250,000,” amesema.

Imeandikwa na Imani Makongoro, Elizabeth Edward na Mariam Mbwana