MSHAMBULIAJI nyota wa Yanga aliyefanyiwa upasuaji wa goti na kumfanya awe nje kwa muda mrefu, Clement Mzize amelizungumzia bao alilowatungua TP Mazembe katika makundi ya Ligi ya Mabingwa linalowania tuzo ya Bao Bora CAF.
Mzize alifunga bao hilo wakati Yanga ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Mazembe ya DR Congo waliporudiana baada ya awali kutoka sare ya bao 1-1 jijini Lubumbashi ambalo limeingia katika tuzo ya Bao Bora la msimu likichuana na wachezaji wengine 12.
Katika orodha iliyotolewa juzi na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya mchujo wa kupunguza idadi ya wanaowania tuzo hizo, Abdellah Ouazane nyota wa timu ya vijana ya Morocco aliyefunga bao katika mechi dhidi ya Serengeti Boy.
Akizungumza uteuzi wa bao alilofungwa kwa Mazembe, Mzize ameliambia Mwanaspoti kuwa ni jambo zuri kwake na linamuongezea ari ya kupambana kwa kuamini kuwa kuna watu wanaona anachofanya na kukithamini.
“Nilifunga ikiwa sehemu ya kuipambania nembo ya klabu yangu iweze kufikia malengo tuliyojipangia, lakini limedumu na kuwa miongoni mwa mabao yanayowania tuzo. Kwangu hili nimelipokea kwa furaha,” alisema Mzize aliyefunga mabao 14 ya Ligi Kuu Bara.
“Ukiondoa kwangu pia ni heshima kwa timu yangu ya Yanga kutajwa kutokana na uwepo wa jina langu kuwania tuzo hiyo. Nawaomba mashabiki na wadau wa mpira kwa ujumla kunipigia kura ili niibuke mshindi.”
Mzize alisema kuibuka kwake mshindi sio sifa kwake pekee, bali hata kwa taifa kwani ataibeba nchi na timu kwa ujumla kwenye uwakilishi wakati wa kukabidhiwa ushindi.
“Wakati wa kupewa tuzo ikitokea nikashinda sitatajwa kama Mzize bali ni Mtanzania na mchezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars, lakini pia wa Yanga.”
Mbali na Mzize na Ouazane pia wapo Anas Roshdy, mchezaji wa timu ya taifa ya Misri ya vijana chini ya miaka 17, bao lake alilifunga kwenye mchezo wa Afcon kwa vijana dhidi ya timu ya taifa ya Afrika Kusini, Ashraf Tapsoba mchezaji wa timu ya taifa ya Burkina Faso kwenye mechi dhidi ya Cameroon.
Pia yumo Barbra Banda kutoka wa timu ya taifa ya Zambia bao alilofunga dhidi ya Morocco katika WAFCON 2024 limetajwa kuingia kinyang’anyiro hicho, Calvin Fely mchezaji wa timu ya taifa ya Madagascar iliyocheza fainali za CHAN 2024 bao lake dhidi ya Morocco linawania tuzo hiyo.
Vilevile Ghizlane Chebbak, mchezaji wa timu ya taifa ya Morocco ni miongoni mwa wanaowania tuzo hiyo kupitia bao alilofunga dhidi ya Nigeria katika CHAN 2024, Ibrahim Adel mchezaji wa Pyramids anawania tuzo hiyo kupitia bao alilofunga dhidi ya ES Tunis katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wengine ni Jean Claude wa Al Hilal aliyefunga bao dhidi ya MC Alger, Ndabayithethwa Ndlondlo mchezaji wa timu ya taifa ya Afrika Kusini alifunga dhidi ya Uganda, Oussama Lamlioui mchezaji wa timu ya taifa ya Morocco alifunga dhidi ya Madagascar, Refiloe Jane wa timu ya taifa ya Sauzi alifunga katika WAFCON 2024 dhidi ya Mali na Soufian Bayazid wa timu ya taifa ya Algeria alifunga dhidi ya Uganda kupitia CHAN 2024.