Hekaheka hospitali, polisi kusaka ndugu

Dar es Salaam. Hali ya maisha ikiendelea kurejea kawaida, kumekuwa na hekaheka za wananchi kwenye vituo vya polisi na hospitali wakiwatafuta ndugu na jamaa zao ama waliofariki au ambao hawajulikani walipo tangu Oktoba 29, 2025 kulipotokea maandamano yaliyoambatana na vurugu.

Kwa mujibu wa ndugu na jamaa za watu hao, pia wanapata ugumu wa kupata miili ya wapendwa wao ambao wamethibitika wamepoteza maisha huku mamlaka zikielendelea kukaa kimya kuhusu idadi yao.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi wameeleza jitihada ambazo wamefanya kwa zaidi ya siku tisa kuwatafuta, huku ikiwawia ugumu wengine kupata miili licha ya kuwa ndugu zao wamethibitika kuwa wamefariki dunia.

Wakati hayo yakiendelea, washtakiwa takribani 80 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakishtakiwa kwa kosa la uhaini kutokana na matukio yaliyotokea Oktoba 29, yakihusisha pia uharibifu wa miundombinu ya Serikali.

Baadhi ya viongozi wa hospitali wanakiri kupokea miili ya marehemu waliopoteza maisha kutokana na matukio hayo, ingawa hawakuwa tayari kuweka hadharani idadi wakieleza wenye mamlaka ya kuzungumzia hilo ni polisi.

Kwa upande wake, Jeshi la Polisi linasema taarifa kuhusu suala hilo itatolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali.

“Hii itatolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali,” alijibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillus Wambura Novemba 5, 2025 alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo.

Tangu IGP alipoeleza hayo, jitihada za kumpata Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa kuzungumzia suala hilo hazijazaa matunda.

Mke ambaye hakuwa tayari kutajwa jina ameeleza tangu Oktoba 29, mumewe alipokwenda kazini mkoani Arusha hajamuona tena.

Anaeleza taarifa alizopewa na shemeji yake ni kuwa, mume wake amepoteza maisha kwa kupigwa risasi eneo la Kaloleni, mkoani Arusha lakini hajaweza kuupata mwili wake.

Kwa mujibu wa mke huyo, shemeji yake alimweleza kuwa daktari alimpigia simu akamweleza ndugu yake amepigwa risasi na yuko hospitali, na alipokwenda kumuona alikuta ameshafariki dunia.

Hata hivyo, anasema tangu wakati huo wamepata ugumu wa kupata mwili wake wakielezwa wakaombe kibali kwa mkuu wa mkoa.

Anadai walielezwa waende Jumamosi Novemba mosi, lakini hawakukabidhiwa, wakatakiwa kwenda Novemba 4, ambayo pia hawakupewa mwili huo.

Anadai walipangiwa kwenda Novemba 6, wakielekezwa kumtafuta mganga mkuu wa wilaya ili wapewe kibali ili wakabidhiwe mwili.

“Mganga mkuu ametuahidi atatupa kibali, lakini hadi sasa bado hatujaupata mwili na sijajua mume wangu yuko hospitali gani,” amesema.

Kwa upande wake, Hashim Saranyika ameeleza kupotelewa na mdogo wake, Maneno Saranyika tangu Oktoba 29, alipokuwa dukani kwake Salasala, jijini Dar es Salaam.

Ameeleza ametaarifiwa na kutumiwa ushahidi wa video na picha za nduguye akiwa ameanguka chini akitokwa damu baada ya kupigwa risasi, akieleza mashuhuda walimweleza kuwa polisi walimpeleka Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Mwananyamala.

Anasema pamoja na wanafamilia wengine walikweda Mwananyamala lakini hawakumpata, hivyo walizuru hospitali nyingine za mkoani Dar es Salaam pasipo mafanikio.

Anasema kwa sababu wamepata uhakika kuhusu kifo chake, waliweka msiba nyumbani wakiendelea kutafuta mwili wa ndugu yao.

“Tukaanza kuhangaika kila hospitali ya Dar es Salaam, hatukufanikiwa. Kuna siku tukasikia watu wanazika miili, tukaenda tukaambiwa hayupo,” anasema.

Baada ya kushindwa kuupata, anasema wameamua kuahirisha kumtafuta na wanaondoa msiba hadi itakapotokea taarifa ya ulipo mwili wa ndugu yao.

“Kama hatutapewa taarifa yoyote, basi ndio itakuwa imeishia hivi, hatuna namna. Lakini tumehangaika sana bila mafanikio,” amesema.

Eliana Sakayo, mkazi wa Mlandizi, mkoani Pwani ameeleza namna alivyozunguka hospitali na mahabusu kadhaa kumtafuta mume wake.

Anasema Oktoba 29, 2025 mumewe ambaye ni mwajiriwa wa kampuni binafsi alitoka kwenda kazini na tangu siku hiyo hadi leo Novemba 7, 2025 hajamtia machoni.

“Nilisikia alijeruhiwa, katika kufuatilia nikaambiwa amepelekwa Muhimbili, alipata jeraha siku ya uchaguzi. Isivyo bahati sikuweza kusafiri kwenda Muhimbili kutokana na njia ya Morogoro kufungwa,” anasema.

Anaeleza Novemba 4, alikwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufuatilia kama kuna mgonjwa huyo bila mafanikio, hadi jioni ya Novemba 6, ndipo akaambiwa aende Kituo cha Polisi Msimbazi.

“Nilifika kweli nikakuta jina la mume wangu lipo kati ya waliokamatwa, lakini sikubahatika kumuona hadi leo,” anasema.

Mbegu Nasoro, mkazi wa Kiluvya Madukani, anasema binti yake alitoka nyumbani Oktoba 29, kwenda kwenye biashara zake, lakini hajaonekana hadi leo.

“Tumeshazunguka mochwari na kwenye wodi katika hospitali mbalimbali za Kibaha na Dar es Salaam hatujafanikiwa kumuona. Simu zake hazipatikani na kwa ndugu wa karibu kote hayupo, tunaomba Mungu tu binti yetu awe salama,” anasema.

Kwa mujibu wa wananchi waliokwenda vituo vya polisi wanaeleza wamekuwa wakikuta orodha ya watu wanaoshikiliwa, hivyo wanapolikosa jina lake hulazimika kwenda vituo vingine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Delilah Kimambo amesema: “Kuhusu wagonjwa tuliowapokea na kama ni miili taarifa zote tumezituma kwa Mganga Mkuu wa Serikali.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Dk Mpoki Ulisubisya amesema taarifa hizo zinapatikana kwa Mganga Mkuu wa Serikali.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mganga Mkuu wa Serikali Dk Grace Magembe amesema atafutwe mkuu wa kitengo cha mawasiliano Wizara ya Afya, Roida Andusamile.

Alipoulizwa Roida amesema: “Hili ni suala la kipolisi. Inapotokea ajali yoyote wao ndio wenye taarifa yao. Hata hivyo, suala hili ni la kitaifa kitengo cha maafa wanaweza kulifafanua zaidi na takwimu ni za Jeshi la Polisi.”

Waliopoteza maisha wahifadhiwe

Akizungumzia tukio hilo, Mtaalamu wa majanga, James Mbatia amesema kilichotokea ni maafa.

“Haya ni maafa si janga, kwenye maafa ya namna hii kunahitajika ukimya wa wote bila kubezana ili muweze kufikiri vizuri. Katika moja ya njia ya kuponya hili ni kuhakikisha miili ya waliouawa inazikwa kwa heshima ili kuondoa maumivu,” amesema na kuongeza:

“Wazikwe kwa heshima kwa sababu ndiyo utamaduni wetu Tanzania, mtu anapewa heshima ili kupunguza maumivu kwa walioathiriwa moja kwa moja.

“Inabidi utulivu wa fikra ni kuwahifadhi wale ambao wameathirika na kutoa kauli ambazo zinaleta matumaini kwa wale waliopoteza ndugu, baadaye ndiyo tuanze kujadili kuhusu upotevu na uharibifu wa mali ambazo zinaweza kutafutwa, ila si uhai wa mtu,” amesema.

Mwanazuoni wa sayansi ya siasa, Dk Conrad Masabo amesema ni muhimu mamlaka zipite mitaani, kuchukua rekodi ya waliopoteza maisha na watu wahifadhiwe kwa mujibu wa imani na tamaduni zao.

“Hicho kitatoa cultural healing (uponyaji kitamaduni). Kwa sababu kwetu mtu kufa ni tatizo lakini litakuwa tatizo zaidi iwapo hatazikwa kwa utaratibu wa kiimani au kitamaduni,” amesema.

Matukio sawa na haya yamemliza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka alipopokea taarifa kutoka kwa wananchi waliopoteza ndugu na jamaa katika vurugu za Oktoba 29.

Mtaka alitokwa machozi alipopokea taarifa hizo katika mkutano na wafanyabishara uliofanyika Novemba 6, 2025 katika Mji wa Makambako.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Sifael Msigala alieleza kuwa vurugu zimesababisha vifo vya wenzao watatu.

Msigala aliiomba Serikali iwapatie miili ya wenzao hao kwa ajili ya kuikabidhi kwa familia na wazikwe kwa mujibu wa mila, imani na tamaduni zao.

“Mioyo yetu itakuwa vizuri tukisikia wamerejeshwa nyumbani kuhifadhiwa…,” amesema.

Miongoni mwa wananchi hao, wapo walioonyesha wasiwasi wa kuzungumza zaidi kwa kile walichodai kufanya hivyo kunawaweka katika hatari ya kupotezwa, huku wengi wakilia kuomba miili ya ndugu zao wakabidhiwe ili kuwahifadhi.

Mtaka aliwahakikishia wananchi kuhusu kuimarika kwa hali ya amani na usalama mkoani humo.

Aliwataka wasisite kutoa taarifa, wakati wowote watakapohisi au kuona viashiria vya uvunjifu wa amani ili hatua zichukuliwe.

“Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga, wananchi wajibu wenu ni kutoa taarifa pale mnapoona kuwapo viashiria vya uvunjifu wa amani ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema huku akisisitiza watu waendelee na shughuli zao.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi ameiomba Serikali ya Tanzania kuhakikisha usalama wa raia wake wanaoishi nchini na isichukue hatua zozote zitakazokiuka haki zao.

Kauli ya Mudavadi imetolewa kukiwa na madai kuwa Wakenya wanaishi kwa hofu nchini kutokana na vitisho vya kuhusishwa na maandamano hayo.

Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Nation, hofu imesababisha baadhi ya familia nchini Kenya zionyeshe wasiwasi wa usalama wa ndugu zao waliopo Tanzania.

Familia moja nchini humo, imedai kupokea taarifa kutoka chanzo cha kuaminika kuwa ndugu yao aliyekuwa mwalimu jijini Dar es Salaam ameuawa lakini mwili haujulikani ulipo.

Imeelezwa kuna taarifa kuwa Wakenya wengi wanatafuta msaada kutoka ubalozi wa nchi hiyo uliopo Dar es Salaam ili kurudi makwao.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isaac Njenga Jumatano ya Novemba 5, 2025 aliliambia Daily Nation kuwa yeyote anayetaka kuondoka Tanzania kurudi Kenya yuko huru.

Inaelezwa Novemba 6, Mudavadi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mahmoud Thabit Kombo walikutana.

“Katika mkutano wetu, tumesisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama na ulinzi wa raia wa kigeni, wakiwemo Wakenya, ambao wanaendelea na shughuli zinazochangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia biashara halali na huduma za kitaaluma,” alisema Mudavadi.

Kwa mujibu wa wizara hiyo nchini Kenya, hadi Mei mwaka huu, takribani Wakenya 250,000 walikuwa wanaishi, kufanya kazi na biashara nchini Tanzania.

Balozi Kombo alipotafutwa ili kuzungumzia suala hilo, simu yake iliita pasipo kupokewa. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi huakujibiwa.

Kanisa kuombea waliofariki

Wakati huo huo, Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya limetangaza nia maalumu ya kuwaombea watu waliopoteza maisha au kujeruhiwa wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.

Siku hiyo katika uchaguzi ulioambatana na maandamano na vurugu katika baadhi ya maeneo, watu ambao idadi yao haijafahamika waliuawa, kujeruhiwa na wengine hawajulikani walipo.

Katika mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 4, 2025 kupitia kwa katibu wa kanisa hilo, Padri Henry Mwalyenga, parokia zote za jimbo kuu zinaagizwa kuwa na nia maalumu ya kuwaombea marehemu na majeruhi.

Maombi hayo yanatarajia kufanyika Novemba 9, 2025 ambayo ni Dominika ya 32 ya mwaka C, ambapo siku hiyo alasiri, kutakuwa na misa maalumu ya kijimbo kwa ajili ya kuwaombea waathirika hao katika Kanisa la Hija Mwanjelwa jijini Mbeya.

“Tunawaomba maparoko wote na mapadri mnaofanya utume ndani ya Dekania ya Mbeya, Mbalizi na Mporoto muwahamasishe waamini pamoja na nyinyi kufika katika misa itakayohudhuriwa na Askofu Mkuu na Askofu Msaidizi,” imesema taarifa hiyo na kuongeza:

Akizungumza kwa njia ya simu, Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Gervas Nyaisonga amethibitisha kuwepo maombi hayo, akieleza lengo ni kuliombea Taifa na wale waliopata madhila wakati na baada ya uchaguzi.

 “Ni kweli barua ni rasmi, tumetangaziana, lengo ni kuliombea Taifa na wale waliopata madhila, kila parokia litafanya ibada hiyo na wale walio karibu na Mbeya tutafanyia kanisa la Mwanjelwa, wananchi wenye kuhitaji kushiriki wanakaribishwa,” amesema askofu huyo.