Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amemuapisha Hemed Suleiman Abdulla kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Hemed ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa mara ya pili katika Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mara ya kwanza aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya Uchaguzi Mkuu wa Novemba 2020. Wakati anateuliwa kushika wadhifa huo, wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, hivyo kwanza aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kisha akateuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais.
Lakini kipindi hiki Hemed amegombea na kushinda kuwa Mjumbe wa Baraza la Uwakilishi katika Jimbo la Kiwani.
Makamu wa Pili wa Rais pamoja na kuwa ndiye mshauri na msaidizi mkuu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi, pia ndiye Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Serikali ndani ya Baraza la Wawakilishi. Hemed ameapishwa leo Novemba 8, 2025 Ikulu Zanzibar.
Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Mawasiliano ya Rais Ikulu, Hemed ameeleza mwelekeo wa Serikali alipozungumza baada ya kuapishwa.
Hemed ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii kubwa, uadilifu na maarifa yake yote kwa kushirikiana na viongozi wenzake chini ya uongozi wa Rais Mwinyi, kuhakikisha malengo yote ya Serikali kipindi cha pili yanatekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaongozwa na ilani ya CCM ambayo kipindi cha kwanza miaka mitano ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa hadi kuvuka malengo yaliyopangwa katika baadhi ya sekta kwa zaidi ya asilimia 150.
Kwa mujibu wa Hemed, mafanikio hayo ni ushahidi wa kazi kubwa iliyofanywa chini ya uongozi thabiti wa Dk Mwinyi na kwamba, katika awamu ya pili, Serikali imejipanga upya kuhakikisha inafanya mambo makubwa zaidi.
“Ilani hii mpya imebeba mambo mengi ya msingi yanayolenga kuwaletea wananchi maendeleo endelevu, kama tulivyofanya kwenye awamu ya kwanza,” amesema.
Amesema Serikali imeandaa mikakati mahususi ya kuhakikisha utekelezaji wa miradi iliyoainishwa kwenye ilani hiyo inakwenda kwa kasi kubwa kama walivyofanya kwa awamu ya kwanza.
“Mkakati wetu ni kuhakikisha tunafanya zaidi ya kilichoelezwa kwenye ilani, kama tulivyovuka malengo katika awamu ya kwanza, ndivyo tunavyodhamiria kufanya mara hii, kufanya kazi kwa kasi, weledi na ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha Zanzibar inazidi kupiga hatua,” amesema.
Ametaja baadhi ya miradi mikubwa ambayo Serikali inatekeleza kwa sasa kuwa ni pamoja na wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, ambao unatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta ya usafiri wa anga, ikiwamo ujenzi wa Terminal IV katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Uwanja wa Ndege wa Pemba na Uwanja wa Ndege Kigunda, miradi ambayo inalenga kuboresha huduma za usafiri wa anga na kukuza utalii.
“Ipo miradi mingi mikubwa tunakwenda kuisimamia kwa karibu na dhamira yetu kuhakikisha miradi hii inakamilika ndani ya kipindi hiki cha pili cha Serikali ya awamu ya nane, kama ambavyo kaulimbiu ya Rais Dk Mwinyi: Yajayo ni neema zaidi,” amesema.
Hemed amesema ameupokea uteuzi huo kwa moyo wa furaha, shukrani na unyenyekevu.
“Namshukuru Rais kwa kuniamini tena, hii ni heshima kubwa na ni ishara ya kuendelea kuniamini kutokana na kazi tuliyofanya kwa pamoja katika awamu ya kwanza, namuahidi kuendeleza bidii ileile na zaidi, katika kutekeleza malengo aliyokusudia kuyafikia katika kipindi hiki cha pili,” amesema.
Amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, hasa katika kipindi cha kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Hemed amesema hali hiyo ya utulivu ni ya kipekee katika historia ya Zanzibar, kwani muda mrefu kulikuwa na changamoto za kisiasa baada ya chaguzi, lakini safari hii wananchi wameonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa na uzalendo wa hali ya juu.
“Kwa sasa Wazanzibari wanaendelea vizuri, tumeshuhudia uchaguzi uliojaa amani na utulivu, jambo ambalo ni heshima kubwa kwa nchi yetu na kwa Rais Mwinyi, hii ni ishara ya maendeleo ya kisiasa na kijamii ambayo lazima tuihifadhi,” amesema.
Amewaomba wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuendelea kudumisha amani ili nchi iendelee kupiga hatua za kimaendeleo na kujizolea sifa duniani.
“Amani ndiyo nguzo ya kila kitu, tukidumisha amani yetu, basi uchumi utaimarika, wananchi watanufaika na nchi yetu itaendelea kujizolea heshima duniani,” amesema.
Hafla ya uapisho imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wale wa dini, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na wanafamilia.