Kakolanya ana hesabu kali timu ya Taifa

KIPA namba moja wa Mbeya City, Beno Kakolanya amesema bado anaamini ana nafasi ya kurejea katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, huku akiwapongeza makipa wote walioitwa kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Kuwait itakayopigwa Novemba 14, 2025 jijini Cairo, Misri.

Stars itacheza mechi hiyo chini ya benchi jipya la ufundi likiongozwa na Kaimu Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, akisaidiwa na Ahmad Ally.

“Naamini wakati wangu bado haujaisha. Nafanya kazi kwa bidii kila siku, naamini kocha mpya ataona mchango wangu kupitia mechi ninazocheza. Nipo tayari kuipigania Stars muda wowote nitakapohitajika,”  alisema.

Akizungumzia makipa wenzake, Yakoub Suleiman, Hussein Masalanga na Zuberi Foba ambao wameitwa kwa ajili ya mechi hiyo, Kakolanya anaamini wanaweza kulifanya lango la Stars kuwa salama.

“Ujue nchi yetu imebarikiwa kuwa na makipa mengi wazuri tangu na tangu, hawa ambao wameitwa kiukweli kabisa, wote ni makipa wazuri hakuna mtu ambaye anaweza kuwa na shaka juu ya uwezo wao, hivyo naamini tunaweza kufanya vizuri,” alisema.

Katika mechi sita alizocheza msimu huu, Kakolanya ameruhusu mabao sita sawa na wastani wa bao moja huku akiisaidia Mbeya City kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi nane wakicheza mechi sita kabla ya mechi za jana.

Mbeya City ni timu ya sita kwa Kakolanya kuichezea Ligi Kuu Bara, alianza kuwika akiwa na Tanzania Prisons, Yanga, Simba, Singida Fountain Gate na Namungo ambako alitumika kwa mkopo wa mwaka mmoja.