Matukio ya Oktoba 29 yalivyoathiri sherehe, watoa huduma

Dar es Salaam. Baadhi ya shughuli za harusi zilizopangwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba na mwanzoni mwa Novemba zimeahirishwa kutokana na maandamano yaliyozua vurugu Oktoba 29, 2025.

Kuahirishwa huko kumevuruga ratiba za washehereshaji, wapambaji na watoa huduma wengine wakiwamo wa chakula, keki, mapambo na kumbi.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya watoa huduma wamejikuta katika mgogoro na wateja ambao wamesogeza mbele tarehe za shughuli zao, hivyo kugongana na ratiba zao zingine zilizokuwa zimepangwa.

Mshehereshaji (MC), Oyite Tungaraja anasema baada ya shughuli za kijamii na kiuchumi kusimama kwa muda wa takribani siku sita, wamejikuta wakipata changamoto za mwingiliano wa ratiba.

Akitoa mfano, anasema ameshindwa kusherehesha shughuli za wateja wake Oktoba 31, 2025 na Novemba mosi, 2025 jambo lililoleta changamoto kati yake na wao kuhusu namna watakavyosogeza mbele shughuli hizo.

“Mmoja wao tarehe anayoitaka tayari mimi ninatakiwa kumuhudumia mteja mwingine na yeye anasema hawezi kubadili kutokana na ratiba za ukumbi. Tumelijadili kwa siku kadhaa, tukaamua kusogeza sherehe yake hadi Desemba,” anasema na kuongeza:

“Mwingine aliniambia anataka kurudishiwa malipo yake ya awali kwa kuwa amesogeza sherehe yake hadi mwanzoni mwa mwaka ujao.”

Abdul Kilumbi, fundi wa ushonaji wa nguo za sherehe jijini Dar es Salaam anasema kuna baadhi ya wateja walitakiwa kwenda kujaribu nguo zao katika kipindi hicho lakini ilishindikana.

“Baadhi yao walikuwa na hofu ya kutoka nje, hivyo ililazimu tupange siku za mbeleni, wengine walishindwa kuchukua nguo kutokana na kusogeza sherehe zao mbele,” amesema.

Betner John, mpambaji na mpishi wa keki anasema changamoto hiyo imesababisha baadhi ya wateja kusogeza shughuli zao mbele kwa kuwa zinagongana na tarehe za sherehe za wateja wengine, ambao muda mrefu walishatoa oda ya kupata huduma.

“Nilichokifikiria sasa ni kuongeza vijana wa kunisaidia kazi hata kwa muda mfupi, ili niweze kukamilisha kazi za wateja wangu wasikose huduma,” anasema.

Tilly Chizenga, mshehereshaji jijini Arusha, anasema kati ya Oktoba 29 hadi Novemba 2, 2025 sherehe zilizokuwa zifanyike ziliahirishwa.

“Mimi nilikuwa na sherehe ya send-off Novemba mosi ila iliahirishwa na wateja wangu wamepeleka katikati ya wiki ijayo, hii imeleta changamoto kwangu kama mtoa huduma na mteja wangu,” amesema na kuongeza:

“Hii haijagongana na shughuli nyingine ila mtiririko wangu wa kiuchumi kwani nilitegemea kumalizia malipo siku hiyo.”

Chizenga ametaja athari nyingine iliyojitokeza kwao ni katazo la muda lililokuwa limetolewa na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Hilo liliwaathiri wengine wengi ambao wateja wao hawakuahirisha shughuli hivyo kulazimika kufanya shughuli ndani ya muda mfupi kabla ya saa 12:00 jioni. Hadi mtu amalize na kufunga vyombo vyake ilikuwa changamoto kubwa,” anasema.

Amesema katika kipindi hicho sherehe zijazo au vikao ambavyo vilipangwa kufanya uamuzi wa kuwapa kazi viliahirishwa, hivyo kuwaathiri kiuchumi.

“Kwa kweli hali ile imeathiri maandalizi ya sherehe zijazo na hiyo imetuathiri moja kwa moja katika maisha yetu. Kwa mfano, kama nilikuwa nategemea hela kwa ajili ya kulipa ada shuleni imeshindikana,” amesema.

Greyson Kijo maarufu MC Chinaa, naye anaeleza alivyokwama:

“Mimi mbali na kuwa MC ninapika, napiga muziki na kupamba. Nilikuwa na kazi Novemba mosi ila iliahirishwa na bahati mbaya wateja walisogeza mbele hadi Novemba 8, 2025, tena bila kunishirikisha wakati nina kazi nyingine Novemba 9, wilayani Babati mkoani Manyara,” amesema na kueleza:

“Ninalazimika kukodi vifaa vya muziki kwa ajili ya kutumia Novemba 8 ili nilivyonavyo vitangulie na vijana wangu Babati kuandaa kule kwa ajili ya kazi ya Novemba 9, 2025. Ninaingia gharama ya kwenda na magari mawili Babati maana nikimaliza kazi Arusha usiku huohuo naenda Babati.”

Mpishi wa keki jijini Arusha, Hilda Rupia anaeleza jinsi vurugu zilizotokea zilivyosababisha kupoteza wateja na kupata hasara.

“Oktoba 30, 2025 nilikuwa natakiwa kumpelekea mteja keki ya send-off ila kutokana na vurugu zile mteja hakuja kuchukua na hajawahi kunipigia hadi leo, keki nilishaitengeneza na kuimaliza na tulikubaliana kuitengeneza kwa Sh300, 000,” amesema.

Anaeleza: “Licha ya kunipa advance (kianzio) ila nimeishia kupata hasara maana hajaja kuchukua keki. Wengine wa keki za birthday (siku ya kuzaliwa) walikuja wakachukua ila wananiambia tugawane hasara, imebidi nifanye hivyo ila tumepoteza wateja.”

Emmanuel Pascal, aliyetarajia kufunga harusi Novemba 8, 2025 amesema kutokana na vurugu zilizotokea Oktoba 29 jijini Mwanza, vibali vya mikusanyiko vilisitishwa kutolewa hivyo kuathiri shughuli yake.

“Kutokana na hali ilivyokuwa ndani ya nchi vibali vya kuruhusu matukio ya mikusanyiko vilikuwa havitolewi, hatukuwa na uhakika hali itapoa lini ikatulazimu tusogeze mbele wiki ijayo ambayo itakuwa Novemba 16,” amesema.

Khadija Salum, anasema walifunga ndoa kimya kimya Novemba mosi kutokana na hali ya usalama ilivyokuwa, akieleza imeathiri shughuli na mipango ya harusi yake.

“Mikusanyiko ilikuwa haitakiwi, nikajikuta naolewa ndoa iliyoshuhudiwa na watu wachache, ni kama ya mkeka tu maana tulikuwa watu kama 10 hivi,” amesema na kuongeza:

“Kumbuka kulikuwa na sare watu wameshona wapendeze, watu walikuwa wamechanga michango wanataka kutuona na kututunza ukumbini… nina vyama vya wanawake wote walitaka kunisapoti lakini kwa kuwa kulikuwa na hali tata ya kiusalama hayo yote yakayeyuka.”

Amesema pamoja na yote, anashukuru ndoa yake ilifanikiwa japo kuna mipango ambayo haikwenda kama ilivyopaswa kuwa.

Mshehereshaji ndani na nje ya Jiji la Mwanza, Swaumu Mrisho amesema japo kulikuwa na zuio la mikusanyiko lililosababisha baadhi ya shughuli kusogezwa mbele, lakini harusi na sherehe zinaweza kufanyika hata kama zimesogezwa, ikilinganishwa na athari za maafa yaliyotokea.