Mikakati ya Singida BS bila Gamondi

UONGOZI wa Singida Black Stars, umesisitiza kwamba Kocha Mkuu, Miguel Gamondi bado yupo sana klabuni hapo, huku ukieleza namna utakavyoishi pale ambapo kocha huyo atatingwa na majukumu ya timu ya taifa.

Novemba 4, 2025, Gamondi aliteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuwa kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars akichukua nafasi ya Hemed Suleman ‘Morocco’ aliyesitishiwa mkataba kwa makubaliano na shirikisho hilo.

Baada ya kuteuliwa, Gamondi ameshaanza kazi kwa kutaja nyota 23 watakaocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Kuwait, Novemba 14, mwaka huu, huku Disemba 2025 akitarajiwa kwenda na Taifa Stars kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) nchini Morocco.

Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, alisema kocha huyo amewahakikishia kwamba ataendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu na pale atakapotingwa ataacha maelekezo kwa wasaidizi wake.

Alisema baada ya kupokea ombi kutoka TFF, klabu hiyo ilikaa chini na Gamondi ili kupata muafaka na kujua hatma ya kikosi chao, hata hivyo, kocha huyo raia wa Argentina aliwahakikishia kwamba ameshaandaa programu zitakazoendelea kufanya kazi hata asipokuwepo na timu. “Majibu yake yalituhakikishia kwamba anaweza kujigawa kulingana na programu na ratiba za mechi zitakavyokuwa, lakini pia anao wasaidizi wengi kwenye benchi letu la ufundi, wapo wataalam wa kutosha,” alisema Massanza.

Ofisa huyo alisema uwepo wa makocha wasaidizi Moussa N’Daw, David Ouma na Muhibu Kanu kunawafanya wajiamini kwani watatekeleza vyema programu za kocha huyo pale ambapo mambo yatakuwa yameingiliana.

“Kipindi hicho ambacho hatAkuwepo ana mpango wa kuacha programu kwa wasaidizi wake na hakuna ambacho kitatetereka, kila anayefanya kazi na Gamondi anajua kocha anataka nini. Ni jambo la kusema tu haya ni maelekezo ya kocha wachezaji wote wanatakiwa kuyafuata,”  alisema Massanza.

“Kwenye hilo hatutatetereka na niwatoe hofu mashabiki, Miguel Gamondi atakuwa anapiga miguu yote Singida na Taifa Stars, hiyo ni fahari kwetu.’