Pemba. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amewahimiza wananchi na waumini wa dini ya Kiislamu kuzingatia misingi ya malezi ya kiimani katika kulinda amani na ustawi wa jamii, ili kulinusuru Taifa.
Othman ameyasema hayo jana Ijumaa Novemba 07, 2025, alipojumuika na waumini wa Kiislamu na wananchi, katika ibada ya Ijumaa, iliyofanyika Msikiti wa Mwitani, Mtemani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mwenyekiti huyo, alieleza hayo baada ya kuombwa na waumini hao, kutoa salamu zake, kufuatia kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, uliompa ushindi mgombea wa CCM, Dk Hussein Mwinyi, akifuatiwa na Othman.
Katika maelezo yake, Othman amedai kuwa katika uchaguzi huo aliopata kura 139,399 sawa na asilimia 23.22, kuna mambo hayakwenda sawa, licha ya kuwa kuwepo kwa miongozo, kanuni na sheria ya mchakato huo.
Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar anayemaliza muda wake, amesema endapo kungekuwa na jamii yenye viongozi wanaofuata miongozo ya haki, imani na malezi yenye maadili kasoro katika uchaguzi zisingejitokeza.
“Ifike hatua katika nchi yetu hii, wakati wa uchaguzi kusiwe na hofu, mashaka, wasiwasi wala taharuki.
“Mnapokubaliana na mkaweka miongozo yenu kama binaadamu wastaarabu, hata kama haipo ndani ya msahafu, iikitokea watu wanaikiuka hiyo ni sawa na dhuluma, haikubaliki hata kwa Mungu, ameeleza Othman huku akihimiza umuhimu wa amani ya kweli hapa nchini.
Othman amebainisha kuwa ili kuondokana na sintofahamu katika chaguzi viongozi waliopata dhamana na wananchi wanapaswa kufuata miongozo ya dini, imani, malezi, pamoja na mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W) badala ya kujali masilahi yao binafsi.
Othman ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, amesema kilichotokea Oktoba 29, kinapaswa kuleta mazingatio ya kiimani na si kufumbiwa macho.
“Kinachotakiwa ni kutafutwa suluhisho la kudumu ili kuwa na utulivu, haki na amani ya kweli, inayojali malezi na maadili bora, hasa kwa vijana na vizazi vijavyo,” amesema Othman.
Katika hatua nyingine, Othman amewashukuru wananchi waliompigia kura, akiwaahidi kuendelea kutetea haki katika njia mbalimbali ili kujenga amani ya kweli itakayodumu kwa masilahi ya Zanzibar.
Imamu wa ibada hiyo, Sheikh Ali Abdi Abeid, amesisitiza haja ya waumini wa Kiislamu kuwa na subra na kutokukata tamaa, hasa katika mitihani na utafutaji wa haki.
“Qur-an Tukufu imetuhimiza tusikae kimya katika kupinga dhulma; tusichoke katika kutetea haki zetu, tusikate tamaa na rehma za Allah,” amesema Sheikh Abeid.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kijamii, dini na siasa akiwemo Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Zanzibar Ismail Jussa.
Othman yupo Pemba katika ziara ya siku saba kwa ajili ya kuzungumza na wanachama na wafuasia wa chama hicho, kusikiliza kero na kujadili mustakabali wa Zanzibar.