Singida Black Stars imepunguzwa kasi baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Pamba Jiji kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, huku Kocha wake, Miguel Gamondi akilalamikia uwanja na urefu wa nyasi kuwanyima matokeo mazuri.
Mechi hiyo imechezwa leo Jumamosi Novemba 8, 2025 kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Singida ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 31 likifungwa na Clatous Chama kwa faulo ya moja kwa moja iliyomshinda kipa wa Pamba Jiji, Yona Amosi.
Pamba Jiji ilisawazisha bao hilo kipindi cha pili dakika ya 51 likifungwa na Kelvin Nashon kwa shuti kali baada ya kuumalizia mpira uliokuwa unazagaa eneo la hatari kufuatia kuwababatiza mabeki.
Baada ya matokeo hayo, Pamba Jiji imefikisha alama tisa na kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa imecheza mechi sita ikishinda mbili, sare tatu na kupoteza moja, huku Singida ikiwa nafasi ya tano na alama saba baada ya mechi tatu.
Bao walilofungwa Singida Black Stars na Pamba Jiji ni la kwanza kuruhusu msimu huu kwenye ligi katika mechi tatu ilizocheza, kwani kabla ya hapo ilikuwa imecheza mechi mbili na kushinda zote dhidi ya Mashujaa (1-0) na KMC (1-0).
Mechi ya leo ni ya tatu kuzikutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu, ambapo mbili za msimu uliopita Singida Black Stars ilishinda 1-0 na kulazimishwa sare ya mabao 2-2.
Licha ya kuanza vyema mechi hiyo kwa kutawala dakika 20 za kwanza na kutengeneza nafasi kadhaa za mabao, Pamba Jiji ilikosa utulivu katika eneo la umaliziaji.
Washambuliaji Peter Lwasa, Yonta Camara na Shaphan Siwa katika nyakati tofauti wakiwa kwenye maeneo ya wazi walishindwa kumalizia nafasi zilizopatikana na kuifanya Pamba Jiji kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili, Pamba Jiji ilianza vyema kwa kufanya mashambulizi ya haraka katika lango la Singida Black Stars, ambapo dakika ya 51, Kelvin Nashon akaisawazishia timu hiyo kwa shuti kali akimalizia mpira uliopigwa na Zabona Mayombya na kuwababatiza mabeki wa Singida.
Dakika ya 61, Singida Black Stars ilifanya mabadiliko ya wachezaji ikiwatoa Mukrim Mussa na Hosro Malanga na kuwaingiza Mohamed Damaro Camara na Elvis Rupia. Pia dakika ya 79, wakatoka Diomande Idriss na Marouf Tchakei, wakaingia Andrew Phili na Emmanuel Kayekeh.
Dakika ya 71, Pamba Jiji nayo ilifanya mabadliko ya wachezaji, ikimuingiza mshambuliaji Mathew Tegis akichukua nafasi ya beki Ibrahim Abraham. Dakika ya 79 akatolewa Saphan Siwa na kuingia Samuel Antwi, huku Yonta Camara na Zabona Mayombya wakiwapisha Hassan Kibailo na Paulin Kasindi dakika ya 86.
Akizungumzia matokeo hayo, Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amelalamikia uwanja kuwa na nyasi ndefu na kutofaa jambo ambalo limewanyima nafasi ya kucheza soka lao la kuvutia, huku wapinzani wakipiga mipira mirefu na ya juu ambayo imeharibu mipango yao.
”Lakini yote kwa yote tumecheza michezo 12 kwa ujumla msimu huu hadi sasa, tumeshinda 9 na sare tatu, siyo mbaya ni matokeo mazuri, hivyo tunaona kwamba bado tuna changamoto ya kutotengeneza nafasi, lazima tukaifanyie kazi,” amesema Gamondi.
Kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza amewapongeza vijana wake kwa matokeo hayo huku akiwataka wasibwete bali waendelee kupambana ili wakusanye alama nyingi kwenye mzunguko wa kwanza ili wawe salama mwishoni mwa ligi.
Pamba Jiji: Yona Amosi, Keneth Kunambi, Ibrahim Abraham, Abdulmajid Mangalo, Brian, James Mwashinga, Zabona Mayombya, Kelvin Nashon, Peter Lwasa, Shaphan Siwa na Yonta Camara.
Singida Black Stars: Amas Obasogie, Andy Koffi, Antony Trabi, Mourice Chukwu, Mukrim Issa Abdallah, Iddi Habib, Diomande Idriss, Marouf Tchakei, Horso Malanga, Clatous Chama na Nickson Kibabage.